41. Ukitaka kujua kuwa Jahmiy anamsemea uwongo Allaah anapodai kuwa Yuko kila mahali

Ukitaka kujua kuwa Jahmiy anamsemea uwongo Allaah pale anaposema eti Allaah yuko kila mahali na kwamba hawi sehemu moja tofauti na nyingine, basi muulize si kuna wakati Allaah alikuwepo pasi na kuweko kitu kingine. Atajibu ndio. Kisha muulize: Wakati alipowaumba viumbe, aliwaumba ndani Yake au nje Yake? Hapa hana budi isipokuwa kujibu majibu matatu. Akisema kuwa Allaah aliwaumba viumbe ndani ya nafsi Yake, anakufuru, kwa sababu atakuwa anadai kuwa majini, watu na mashaytwaan wako ndani ya Allaah. Na akisema kuwa aliwaumba nje ya nafsi Yake kisha baadaye Akaingia ndani yao, anakufuru, kwa sababu itakuwa na maana kwamba Allaah atakuwa ameingia mahali ambapo ni pachafu na penye taka. Akisema kuwa aliwaumba nje ya nafsi Yake kisha hakuingia ndani yao, atakuwa amejirejea kikamilifu kutokana na maoni yake – na haya ndio maoni ya Ahl-us-Sunnah[1].

[1] Ibn ´Aqiyl al-Hanbaliy amesema:

”Imaam Ahmad (Rahimahu Allaah) ameandika kitabu kinachoitwa ”ar-Radd ´alaal-Jahmiyyah waz-Zanaadiqah wal-Qadariyyah.” (al-Aadaab ash-Shar´iyyah (1/274))

Ibn Taymiyyah amesema:

”Kama alivosema Imaam Ahmad katika kitabu chake ”ar-Radd ´alaaz-Zanaadiqah wal-Jahmiyyah.”  (Tafsiyr Suurat-il-Ikhlaasw, uk. 239)

Ibn Kathiyr amesema:

”… na hivo ndivo alivosema Ahmad bin Hanbal katika kitabu ”ar-Radd ´alaal-Jahmiyyah” (Tafsiyr al-Qur-aan al-´Adhwiym (3/304))

Ibn Hajar al-´Asqalaaniy amesema:

”Amesema waziwazi Ahmad katika kitabu “ar-Radd ´alaal-Jahmiyyah.” (Fath-ul-Baariy (13/598))

  • Muhusika: Imaam Ahmad bin Hanbal (afk. 241)
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: ar-Radd ´alaal-Jahmiyyah waz-Zanaadiqah, uk. 155-156
  • Imechapishwa: 29/04/2024