Swali 41: Unasemaje kuhusu ambaye anaswali faradhi nyuma ya ambaye anaswali swalah iliyopendekezwa?

Jibu: Hapana neno swalah ya anayeswali faradhi nyuma ya ambaye anaswali swalah iliyopendekezwa. Imethibiti kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) juu ya baadhi ya aina za swalah ya khofu kwamba aliwaswalisha kundi la watu Rak´ah mbili kisha akatoa salamu. Kisha akawaswalisha kundi lingine Rak´ah mbili kisha akatoa salamu. Ile swalah ya kwanza juu yake ilikuwa ni faradhi na ya pili ilikuwa imependekezwa. Kuhusu wanaoswali nyuma yake ni wenye kuswali faradhi.

Vilevile imethibiti kwa al-Bukhaariy na Muslim kupitia kwa Mu´aadh (Radhiya Allaahu ´anh) kwamba alikuwa akiswali na Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) swalah ya ´Ishaa kisha anarudi kwa watu wake anawaswalisha swalah hiyohiyo. Kwa hivyo juu yake inakuwa yenye kupendeza na kwa wale wengine inakuwa ya faradhi.

Mfano wa hayo ni kama mtu atafika katika Ramadhaan akawakuta wanaswali Tarawiyh ilihali yeye hajaswali faradhi ya ´Ishaa. Katika hali hiyo ataswali pamoja nao faradhi ya ´Ishaa ili aweze kupata fadhilah za mkusanyiko. Pindi imamu atapotoa salamu atasimama na kukamilisha swalah yake.

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Fataawaa Muhimmah, uk. 48
  • Imechapishwa: 29/08/2022