42. Kutosihi kwa swalah ya anayeswali peke yake katika safu

Swali 42: Ni ipi hukumu ya anayeswali peke yake nyuma ya safu? Afanye nini anapoingia mtu na asipate mahali nyuma ya safu? Akimpata mtoto ambaye hajabaleghe apange safu pamoja naye?

Jibu: Hukumu ya mtu kusimama peke yake nyuma ya safu ni kubatilika. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Hakuna swalah ya anayeswali peke yake nyuma ya safu.”

Isitoshe imethibiti kutoka kwake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kwamba alimwamrisha ambaye ameswali nyuma ya safu peke yake airudie swalah yake. Hakumuuliza kama alipata maeneo pa kujipenyesha au hakupata. Kwa hiyo ikafaamisha kuwa hapana tofauti kati ya ambaye amepata upenyo katika safu na ambaye hakupata safu kwa ajili ya kufunga njia ya kuchukulia wepesi jambo la mtu kuswali nyuma ya safu peke yake.

Lakini akija ambaye amechelewa akamkuta imamu amerukuu ambapo akarukuu nje ya safu kisha akajiunga na safu kabla ya kusujudu kutasihi kufanya hivo. Hayo ni kutokana na yale yaliyothibiti katika “as-Swahiyh” ya al-Bukhaariy (Rahimahu Allaah) kutoka kwa Abu Bakrah ath-Thaqafiy (Radhiya Allaahu ´anh):

“Ya kwamba alikuja kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akamkuta amerukuu ambapo na yeye akarukuu nje ya safu. Kisha akajiunga ndani ya safu. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akamwambia baada ya kutoa salamu:

“Allaah akuzidishie pupa na usirudie.”

Hakumwamrisha kulipa Rak´ah nyingine.

Kuhusu ambaye atakuja akamkuta imamu yuko ndani ya swalah na asipate upenyo katika safu basi anatakiwa kusubiri mpaka pale atakapopata ambaye atapanga naye safu hata akiwa ni mtoto ameshafikisha miaka isiyopungua saba. Anaweza vilevile kusogea mbele na kupanga safu kuliani mwa imamu kwa ajili ya kutendea kazi Hadiyth zote.

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Fataawaa Muhimmah, uk. 49-50
  • Imechapishwa: 29/08/2022