Abu Ja´far at-Twahaawiy (Rahimahu Allaah) amesema:

68 – Hatumkufurishi yeyote katika wanaoswali kuelekea Qiblah muda wa kuwa hajaihalalisha.

MAELEZO

Bi maana kuhalalisha kimoyo na kiitikadi. Vinginevyo kila mtenda dhambi ameihalalisha dhambi yake kimatendo. Kwa ajili ni lazima kupambanua kati ya yule ambaye anahalalisha kiitakidi, ambaye ni kafiri kwa maafikiano, na ambaye anahalalisha kimatendo na si kwa kuitakidi, ambaye ni mtenda dhambi na anastahiki adhabu inayolingana naye ispokuwa ikiwa kama Allaah atamsamehe. Baada ya hapo imani yake ni yenye kumuokoa.

Khawaarij na Mu´tazilah wanaona kinyume. Wanaona kuwa ni mwenye kudumishwa Motoni milele, ingawa wanatofautiana kama ni kafiri au mnafiki. Leo kumezuka kundi jipya linalowafuata watu hawa ambapo wanawakufurisha waislamu wote, watawala na wananchi. Baadhi wako Syria, wengine Makkah na wengine maeneo mengine. Wanazo hoja tata kama za Khawaarij, kukiwemo yale maandiko yanayosema kuwa mwenye kufanya jambo fulani anakufuru. Mshereheshaji Ibn Abiyl-´Izz (Rahimahu Allaah) amewataja baadhi hapa. Amewanukuu Ahl-us-Sunnah wanaosema kuwa imani ni maneno na matendo, inazidi na inapungua, kwamba dhambi ni kufuru ya kimatendo na si ya kiitikadi na kwamba kufuru, ni kama imani, iko katika ngazi mbalimbali, ikiwa ni pamoja na kufuru ndogo. Kisha akataja mfano muhimu, ambao wameghafilika kulifahamu kundi hili jipya, na akasema:

”Hapa kuna jambo ambalo inapasa kulielewa vyema: Kuhukumu kinyume na yale aliyoteremsha Allaah kunaweza kuwa kufuru, inayomtoa mtu nje ya Uislamu, dhambi, kubwa au ndogo. Kunaweza pia kuwa ni kufuru, ima ya kimafumbo au kufuru ndogo, kwa mujibu wa yale maoni mawili yaliyotajwa. Inategemea na yule hakimu. Ikiwa anaona kuwa si lazima kuhukumu kwa Shari´ah ya Allaah, kwamba ni jambo linalopendeza peke yake au amelidharau pamoja na kujua kuwa ni hukumu ya Allaah, hii ni kufuru kubwa. Na ikiwa anaona kuwa ni lazima kuhukumu kwa yale aliyoteremsha Allaah, akajua yale anayoyasema kwa hali hii na baadaye akapondoka nayo na wakati huohuo akatambua kuwa anastahiki kuadhibiwa, ni mtenda dhambi na ni kafiri kwa njia ya mafumbo, au kufuru ndogo. Na ikiwa hajui hukumu ya Allaah katika hali fulani na akafanya ijtihada yake yote katika kuijua hukumu lakini akakosa, huyu analipwa thawabu kwa ijtihaad yake na ni mwenye kusamehewa kwa kosa lake.”[1]

[1] Sharh al-´Aqiydah at-Twahaawiyyah, uk. 446

  • Mhusika: Imaam Muhammad Naaswir-ud-Diyn al-Albaaniy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-´Aqiydah at-Twahaawiyyah – Sharh wa Ta´liyq, uk. 61-63
  • Imechapishwa: 01/10/2024