40. Mtazamo wa Salaf juu ya Anaashiyd na waimbaji

Mfumo wa pili ni nyimbo. Nyimbo ni uimbaji wa mashairi kwa lengo la kuzitengeneza nyoyo, kuwaongoza waliopotea na kuwavutia wale walioghafilika kwenda katika kheri na wema. Shaykh-ul-Islam Ibn Taymiyyah (Rahimahu Allaah) amesema kuhusu aina hii ya nyimbo:

“Kuhusu kukusanyika kwa ajili ya kusikiliza mashairi yanayoimbwa kwa ajili ya kuzitengeneza nyoyo – ima nyimbo hizo zikawa hazina zana za muziki au zimeambatana na kupiga makofi na mfano wake – ni kitendo kilichozuliwa ndani ya Uislamu. Kimezuliwa baada ya kumalizika zile karne tatu, ambazo zimesifiwa na Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Karne bora ni ile karne niliyotumilizwa kwao. Kisha wale watakaofuatia, kisha wale watakaofuatia.”

Watu mashuhuri katika Ummah wamechukizwa na kitendo hicho, Mashaykh wakubwa hawakuyahudhuria. ash-Shaafi´iy (Rahimahu Allaah) amesema:

“Baghdaad nimeacha kitu kilichozuliwa na mazanadiki. Wanakiita Taghbiyr. Kwacho wanawafukuza watu mbali na Qur-aan.”[1]

Imaam Ahmad aliulizwa juu ya kitu hicho ambapo akasema:

“Ni kitu kilichozuliwa. Nakichukia.” Akaambiwa: “Kinalainisha moyo.” Akasema: “Usiketi nao.” Akaambiwa: “Wakatwe?” Akajibu: “Hawafikii yote haya.”

Akabainisha kuwakitendo hicho ni Bid´ah ambayo haikufanywa na zile karne bora, si Hijaaz, Shaam, Misri, ´Iraaq wala Khuraasaan. Laiti kingekuwa ni kitu kinachowanufaisha waislamu katika dini yao, basi Salafwangelikuwa wa kwanza kuzisikiliza.”

Mpaka alipofikia kusema (Rahimahu Allaah):

“Muumini anatakiwa kutambua kuwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) hakuacha kitu chochote kinachokurubisha Pepo isipokuwa amekihadithia wala chochote kinachoweka mbali na Moto isipokuwa amekihadithia. Kama kungelikuwa na manufaa katika nyimbo hizi basi angeziweka Allaah na Mtume Wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) katika Shari´ah. Kwani Allaah (Ta´ala) amesema:

الْيَوْمَ أَكْمَلْتُ لَكُمْ دِينَكُمْ وَأَتْمَمْتُ عَلَيْكُمْ نِعْمَتِي وَرَضِيتُ لَكُمُ الْإِسْلَامَ دِينًا

”Leo nimekukamilishieni dini yenu na nimekutimizieni neema Yangu na nimekuridhieni kwenu Uislamu uwe ndio dini yenu.”[2]

Hata kama zinauathiri moyo lakini kusipatikane dalili yake katika Qur-aan na Sunnah, basi zinapuuzwa. Sahl bin ´Abdillaah at-Tustariy amesema:

“Kila jambo ambalo halifahamishwi na Qur-aan na Sunnah ni batili.”

Abu Sulaymaan ad-Daaraaniy amesema:

“Wakati mwingine nasikia suala la kielimu kutoka kwa watu linalonasa moyo wangu. Silikubali isipokuwa kwa mashahidi wawili waadilifu kutoka katika Qur-aan na Sunnah wanaokishuhudia.”

Abu Sulaymaan amesema tena:

“Haifai kwa mtu ambaye amefikiria kufanya kitendo cha kheri kukifanya mpaka akithibitishe kwa dalili. Akifanya hivo basi inakuwa nuru juu ya nuru.”[3]

[1] Aadaab ash-Shaafi´iy, uk. 310, ya Ibn Abiy Haatim, Hilyat-ul-Awliyaa’ (9/146) ya Abu Nu´aym, Manaaqib-ush-Shaafi´iy (1/283) ya al-Bayhaqiy, Talbiys Ibliys, uk. 230, ya Ibn-ul-Jawziy na Siyar A´laam-in-Nubalaa’ (10/91) ya adh-Dhahabiy.

[2] 5:3

[3] Majmuu´-ul-Fataawaa (11/591).

  • Mhusika: Shaykh ´Abdus-Salaam bin Barjas Aal ´Abdil-Kariym
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-Hujaj al-Qawiyyah ´alaa anna Wasaa-il-ad-Da´wah Tawqiyfiyyah, uk. 48-50
  • Imechapishwa: 21/05/2023