39. Mtazamo wa Salaf juu ya visa na wapiga visa

Nitataja mifano miwili juu ya njia za kulingania ambazo, licha ya kuwa zina manufaa, Salaf walizikemea vikali kwa sababu tu hazikuwa ni miongoni mwa njia za ulinganizi wa kinabii. Mifumo hio ilizuliwa baada ya kufariki Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Hilo tu atambue mwanafunzi ya kwamba Salaf walikuwa wakiona kuwa ulinganizi ni lazima uwe umejengeka juu ya Qur-aan na Sunnah.

Kitu cha kwanza ni visa. Ibn-ul-Jawziy amesema:

“Mpiga visa ni yule ambaye anasimulia na kufafanua visa vya kale. Hili mara nyingi huhusiana na visa vya zamani. Jambo hili lenyewe kama lenyewe halisimangwi, kwa sababu kusimulia khabari za watu waliotangulia ndani yake kuna mazingatio kwa mwenye kuzingatia na kufuata yaliyo ya sawa kwa anayetaka kufata. Salaf walichukizwa na visa kutokana na sababu sita. Sababu moja wapo ni kwamba wao wenyewe walikuwa wakifuata na kuigiliza. Walikuwa wakiona mtu anafanya kitu ambacho kinatofautiana na njia ya Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), basi wanamkemea.”[1]

Haafidhw Zayn-ud-Diyn al-´Iraaqiy (Rahimahu Allaah) amesema:

“Miongoni mwa mambo yaliyozuliwa baada ya kufa kwake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ni yale waliyozua wapiga visa, jambo ambalo lilipingwa na kikosi cha Maswahabah wengi. ´Aaishah (Radhiya Allaahu ´anhaa) amesimulia kuwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Yeyote atakayezua katika amri yetu hii kile kisichokuwemokitarudishwa.”[2]

Ibn Maajah amepokea kwa cheni ya wapokezi nzuri kwamba ´Abdullaah bin ´Umar (Radhiya Allaahu ´anhumaa) amesema:

“Hakukuweko visa katika zama za Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), zama za Abu Bakr wala zama za ´Umar.”

Imaam Ahmad na at-Twabaraaniy wamepokea kuwa as-Saaib bin Yaziyd amesema:

“Hakukuwa kunapigwa visa katika zama za Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), zama za Abu Bakr wala zama za ´Umar.”

at-Twabaraaniy amepokea kwamba ´Amr bin Zaraarah amesema:

“´Abdullaah bin Mas´uud alisimama juu yangu wakati niko napiga visa akasema: “Hakika, ee ´Amr, umezua Bid´ah na umepotea au umeongoka zaidi kuliko Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na Maswahabah zake.”[3]

Ibn Wadhdhwaah amempokea adh-Dhwahhaak ambaye amesema:

“Nimemuona ´Umar bin ´Abdil-´Aziyz akiwafunga wapiga visa na wale wanaowasikiliza.”[4]

Ibn Wadhdhwaah amepokea tena kutoka kwa Hammaam bin al-Haarith at-Taymiy ambaye amesema:

“Wakati Ibraahiym at-Taymiy alipoanza kupiga visa, baba yake alimtoa nje ya nyumba yake na akasema: “Nini hichi ulichozua?”

Ibn Wadhdhwaah amepokea pia kutoka kwa Mu´aawiyah bin Qurrah ambaye amesema:

“Tulikuwa tunapomuona mtu anapiga visa, basi tunasema kuwa ni mzushi.”

Katika kitabu hichohicho imekuja kwamba ´Amr bin al-´Alaa´ al-Yamaniy alimuuliza Sufyaan ath-Thawriy:

“Ee Abu ´Abdillaah! Tuwaelekee wapiga visa?” Akasema: “Zigeuzieni Bid´ah mgongo wenu.”

Zingatia namna ambavoSalaf waliwakaripia wapiga visa, wakawatahadharisha na kuwatia katika Bid´ah kwa sababu tu ya kule kuzua kwao kitu kipya ndani ya dini ya Allaah. Licha ya kuwa visa vinaweza kumkumbusha aliyeghafilika na mtenda dhambi akaacha kutenda dhambi, lakini muda wa kuwa mifumo hiyo haiko katika Sunnah za Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), ndipo madhara yake yakawa makubwa zaidi kuliko manufaa yake na wenye kuzifanya wakawa wamezua katika Shari´ah ya Allaah (Ta´ala)[5].

[1] Kitaab-ul-Qusswaswwal-Mudhakkiriyn, uk. 66

[2]Muslim (1718).

[3] Tazama ”Tahdhiyr-ul-Khawaassw min Akaadhiyb-il-Qusswaasw”, uk. 170, ya as-Suyuutwiy.

[4] Ibn Wadhdhwaah katika ”al-Bid´a wan-Nahiy ´anhaa”, uk. 19-21.

[5] Wakati fulani neno visa linaweza kutumika juu ya mawaidha na ukumbusho. Mambo yakiwa hivo sicho tunachozungumzia. Kwa ajili hiyo baadhi ya Salaf walikuwa wanaweza kuhimiza visa, navyo ni mawaidha na ukumbusho. Zingatia hilo.

  • Mhusika: Shaykh ´Abdus-Salaam bin Barjas Aal ´Abdil-Kariym
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-Hujaj al-Qawiyyah ´alaa anna Wasaa-il-ad-Da´wah Tawqiyfiyyah, uk. 46-48
  • Imechapishwa: 21/05/2023