Maneno yake:

“Wala havuki kile alichoandikiwa katika Ubao ulioandikwa.”

Kila kitu kimeandikwa kwenye Ubao uliohifadhiwa ambao Allaah ameiamrisha kalamu ikaandika ndani yake kila kitachokuweko mpaka siku ya Qiyaamah. Hayo yalifanyika miaka elfu khamsini kabla ya kuumba mbingu na ardhi na ´Arshi Yake ilikuwa juu ya maji. Kila kitu kimeandikwa, kimekadiriwa na kimepangwa. Vilevile ni lazima kitokee katika wakati wake. Wewe umeamrishwa kufanya sababu. Usijizuie na kusema kuwa wewe utajizuia kwa mujibu wa mipango na makadirio ya Allaah. Kitendo hichi hakijuzu kabisa isipokuwa kutoka kwa mtu mwendawazimu. Mwenye busara hawezi kukaa, akapuuza sababu na kusema kwamba kitatokea kile ambacho ameandikiwa.

Maoni sahihi ni kwamba kitu hichi kimeandikwa ukifanya sababu. Lakini usipofanya sababu hufikii kitu. Usipooa huwezi kupata watoto. Kuoa ni sababu ya kupata watoto. Vivyo hivyo ndivo zinakuwa sababu zengine. Kwa hiyo mja anachotakiwa ni yeye kufanya sababu. Kuhusu natija ni jambo liko kwa Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala). Usihuzunike usipofikia natija. Bali ridhia mipango na makadirio ya Allaah na useme:

قدر الله وما شاء فعل

“Qadar ya Allaah; akitakacho huwa.”

Pengine jambo hilo lina kheri na wewe na usilichukie. Maneno yake:

“… katika Ubao ulioandikwa.”

Ndani yake kumeandikwa makadirio ya kila kitu. Kuna makadirio ya kisehemu yanayochukuliwa kutoka katika Ubao uliohifadhiwa. Kwa mfano kipomoko tumboni mwa mama yake kunapotimiza miezi minne kinapuliziwa roho, kinatumiwa Malaika na anaamrishwa aandike mambo mane; riziki yake, muda wake wa kuishi, matendo yake, atakuwa mwema au muovu. Makadirio kama haya yanachukuliwa kutoka katika Ubao uliohifadhiwa katika makadirio yaliyotangulia.

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh ´Aqiydat-il-Imaam Mujaddid Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab, uk. 61-62
  • Imechapishwa: 23/03/2021