Na jua kwamba Allaah (Subhaanah) kwa Hekima Yake hakutuma Mtume yeyote kwa Tawhiyd hii isipokuwa alimuwekea maadui, kama alivyosema (Ta´ala):

وَكَذَٰلِكَ جَعَلْنَا لِكُلِّ نَبِيٍّ عَدُوًّا شَيَاطِينَ الْإِنسِ وَالْجِنِّ يُوحِي بَعْضُهُمْ إِلَىٰ بَعْضٍ زُخْرُفَ الْقَوْلِ غُرُورًا

”Na hivyo ndivyo Tumefanya kwa kila Nabii anao maadui nao ni shayaatwiyn katika watu na majini wakidokezana wenyewe kwa wenyewe maneno ya kupambapamba na ya udanganyifu.” (al-An´aam 06 : 112)

Na yawezekana maadui wa Tawhiyd wakawa na elimu kubwa, vitabu na hoja. Kama alivyosema (Ta´ala):

فَلَمَّا جَاءَتْهُمْ رُسُلُهُم بِالْبَيِّنَاتِ فَرِحُوا بِمَا عِندَهُم مِّنَ الْعِلْمِ

”Basi walipowajia Mitume wao kwa hoja za wazi, walifurahia kwa yale waliyokuwa nayo katika elimu.” (al-Ghaafir 40 : 83)

MAELEZO

Hekima ya Allaah (Ta´ala) imefupika katika mambo mawili:

La kwanza: Hakutuma Mtume yeyote isipokuwa alimfanya kuwa na maadui katika washirikina, kama ilivyo katika Aayah iliyotajwa na mwandishi na kama ilivyo katika Aayah:

وَكَذَٰلِكَ جَعَلْنَا لِكُلِّ نَبِيٍّ عَدُوًّا مِّنَ الْمُجْرِمِينَ ۗ وَكَفَىٰ بِرَبِّكَ هَادِيًا وَنَصِيرًا

“Hivyo ndivyo Tumemfanyia kila Nabii kuwa na adui miongoni mwa wahalifu na Mola wako anatosheleza kuwa ni Mwenye kuongoa na Mwenye kunusuru.” (25:31)

Allaah ana hekima ya kufanya hivo: ili aweze kutambulika mkweli na mwongo, mtiifu na mwenye kuasi. Anapowatuma Mitume wenye kulingania katika uongofu anafanya kunawepo walinganizi wapotevu kwa ajili ya kuwapa mtihani watu na kutazama ni nani atakayewafuata Mitume na ni nani atayewafuata walinganizi wapotevu. Mambo yasingelikuwa hivo basi watu wote wangelikuwa wanawafuata Mitume ijapokuwa kwa nje tu na kusibainike ni nani mkweli katika kufuata kwake na mnafiki. Hili ni kwa sababu Mitume wanafuatwa na muumini wa kweli na mnafiki mwongo. Kinachopambanua hayo mawili ni mitihani na majaribio. Majanga ndio yanayopambanua kati ya mkweli na mwongo. Allaah kufanya Mitume kuwa na maadui ni kwa hekima kwa sababu ya mitihani na majaribio:

لِيَمِيزَ اللَّـهُ الْخَبِيثَ مِنَ الطَّيِّبِ وَيَجْعَلَ الْخَبِيثَ بَعْضَهُ عَلَىٰ بَعْضٍ

“Ili Allaah apambanue waovu na wema na aweke waovu juu ya waovu wengine.” (08:37)

Hii ndio hekima ya Allaah (Jalla wa ´Alaa) kumuwekea kila Mtume maadui katika watu na majini.

Shaytwaan ni asi na mtenda dhambi. Kila mwenye kuasi kutokamana na kumtii Allaah ni shaytwaan. Ni mamoja akawa miongoni mwa majini au watu. Mpaka wale wanyama wa miguu wane waasi huitwa shaytwaan. Kwa hiyo mashaytwaan wanakuwa katika ulimwengu wa majini na katika ulimwengu wa watu.

Msingi katika mapambo ni dhahabu. Maneno ya kupambapamba ni yale yenye kurembwa na ya kuzua kwa lengo la kutaka kuwaghuri watu. Maneno ya kupambwapambwa ni yale ya uongo yalio na kitu katika ukweli. Huu ni mtihani mkubwa. Batili ingelikuwa iko wazi isingelikubaliwa na yeyote. Lakini yakifunikwa na kitu katika ukweli yanakubaliwa na watu wengi na wanadanganyika na upambwaji huu. Kwa msemo mwingine ni batili ilio kwa sura ya ukweli:

وَلَوْ شَاءَ رَبُّكَ مَا فَعَلُوهُ

“Na lau angetaka Mola wako wasingeliyafanya hayo.” (06:112)

Allaah ni muweza wa kuwazuia na hayo. Lakini hata hivyo ametaka wayafanye kwa ajili ya majaribio na mtihani. Ikiwa hali ni kama hii kwa Mitume ni vipi kwa wengine katika walinganizi wanaolingania kwa Allaah na wanachuoni wa Tawhiyd? Wafuasi wa Mitume na wao wanakuwa na maadui katika walinganizi wa batili. Inahusinana na kila zama na sehemu. Hili ni jambo lenye kuendelea katika viumbe kuwepo kwa walinganizi wa haki na pambezoni mwao kuwepo walinganizi wa batili katika kila zama na mahali.

La pili: Jambo la kushangaza ni kuona walinganizi wa batili wanakuwa na elimu, vitabu na hoja wanazowajadili kwazo Ahl-ul-Haqq. Amesema (Ta´ala):

فَلَمَّا جَاءَتْهُمْ رُسُلُهُم

”Basi walipowajia Mitume wao kwa hoja za wazi.”

Bi maana walipowajia makafiri kwa uhakika wa wazi na elimu yenye manufaa:

فَرِحُوا بِمَا عِندَهُم مِّنَ الْعِلْمِ

“… walifurahia kwa yale waliyokuwa nayo katika elimu.”

Walioirithi kutoka kwa mababu na mababa zao. Hapa ni zile ibara juu ya vitabu vyao na hoja zao walizorithi. Huu ndio uhakika wa mambo hivi sasa.

Hii leo kunapatikana vitabu vingapi vilivyoandikwa na watu wa batili! Kama mfano wa vitabu vya Jahmiyyah, Mu´tazilah, Ashaa´irah na vya Shiy´ah. Vitabu vyao ni vingi. Wana hoja zilizopambwapambwa zenye kumghuri yule asiyekuwa na uimara katika elimu. Wameegemea katika elimu ya falsafa na elimu ya mantiki na wameifanya kuwa ndio elimu sahihi yenye kufidisha yakini.

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Kashf-ish-Shubuhaat, uk. 56-57
  • Imechapishwa: 02/12/2016