Iwapo mtu ataingia kwenye makaburi yaliyopambwa na kurembwa hatoweza kupambanua kati ya aliye na furaha na mla khasara. Allaah peke yake ndiye mwenye kujua hayo. Kunaweza kuwepo kaburi ambalo athari yake imeshapotea na linakanyagwa na wanyama ilihali mwenye nalo yuko katika Pepo ya juu kabisa. Kunaweza kuwa kaburi lililopambwa na kuba lililoinuliwa na kitambaa cha hariri ilihali yule aliyezikwa ndani yake yuko Motoni. Bali mtu anapoingia makaburini hawezi kupambanua kati ya kaburi la mwanaume na mwanamke, mzee na kijana, aliyehuru na mtumwa. Vipi tutaweza kupambanua kati ya aliye na furaha na mla khasara ikiwa hata hatuwezi kufanya hivo kwa hawa ambao tofauti yao iko wazi kabisa duniani?

Usiku ulipokuwa unaingia ´Atwaa´ as-Sulamiy alikuwa akienda makaburini na kusema:

“Enyi watu wa makaburini! Mmekufa! Mmepata matendo yenu. Kesho ´Atwaa´ naye atakuwa ndani ya kaburi.”

Anaendelea kubaki katika hali hiyo mpaka alfajiri inaingia.

Sufyaan ath-Thawriy amesema:

“Atayekithirisha kukumbuka kaburi basi ataona kuwa ni bustani miongoni mwa mabustani ya Peponi. Atayeghafilika kuyakumbuka basi ataona kuwa ni shimo miongoni mwa mashimo ya Motoni.”

´Aliy bin Abiy Twaalib alipita pembezoni na makaburi akasimama kidogo na kusema:

“Amani iwe juu yenu, enyi wakazi katika upweke na utupu! Nyinyi mmetutangulia na sisi tuko nyuma yenu. Karibu tutajiunga na nyinyi. Ee Allaah! Tughufirie sisi na wao. Tusamehe sisi na wao. Pepo kwa yule mwenye kuyakumbuka mauti, akatenda kwa ajili ya hesabu, akakinaika na kuridhika na Allaah kwa hali zote! Enyi wakazi! Wake zenu wameshaolewa. Manyumba yenu wanakaa watu wengine. Mali zenu zimeshagawanywa. Haya ndio tunayoweza kukukhabarisheni. Nyinyi mna nini ya kutukhabarisha?” Halafu anageuka na kwenda kwa watu wake na kusema: “Lau wangeliweza kusema basi wangesema: “Tumeona kuwa bora ya masurufu ni uchaji Allaah.”

Imepokelewa kuwa kuna mwanaume alikuja kwa ´Umar bin ´Abdil-´Aziyz (Rahimahu Allaah) na akapendezwa na jinsi alivyobadilika kutokana na wingi wa ´ibaadah. ´Umar akamwambia:

“Ee mwana wa ndugu yangu! Ni kipi kimechokupendeza kwangu? Ungelisema nini baada ya kuniona siku tatu ndani ya kaburi langu? Mboni ya jicho imetoka mpaka kwenye mashavu. Midomo imekatika na imefunguka kutoka kwenye meno. Minyoo inatoka puani na kinywani mwangu. Tumbo langu limevimba juu ya kifua. Ungeniona hivo ungeshangazwa zaidi kuliko unavyoniona sasa.”

Yule mwenye kujua kuwa ataingia kwenye giza na shimo lililo tupu hajali kupamba uinje wake. Anajau yanayosubiri kiwiliwili kizuri, muonekano mzuri na ngozi laini. Hakika karibu atatupwa ndani ya shimo ambalo atakatana na nduguze na hali yake kubadilika. Halafu ataanza kuoza na kunuka mpaka jamaa yake aliyekuwa ni mpenzi zaidi kwake anamkimbia.

Mja akitafakari vizuri juu ya yale makaburi mazuri ya watu basi ataona kuwa ni kana kwamba hawakuwahi hata siku moja kuwepo duniani na kuishi maisha ya raha na mazuri. Ninaapa kwa Allaah hivi sasa wanapewa adhabu, mitihani na wadudu juu ya viwiliviwili vyao. Mbora na mwenye furaha ni yule aliyesalimishwa na adhabu ya Allaah (´Azza wa Jall). Thaabit al-Bunaaniy amesema:

“Niliingia makaburini. Pindi nilipotaka kutoka nikasikia sauti ikisema: “Ee Thaabit! Usighurike na kimya cha makaburi. Kuna wengi wanaoadhibiwa ndani yake.”

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Muhammad al-Hanbaliy al-Manbajiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Tasliyatu Ahl-il-Maswaa-ib, uk. 193-195
  • Imechapishwa: 03/12/2016