230 – Muhammad bin Idriys amenihadithia, kutoka kwa Abu Ishaaq at-Twaliqaaniy, kutoka kwa al-Fudhwayl bin ´Iyaadh, ambaye amesema:

”Maalik bin Diynaar aliletewa Faaluudhah[1], ambapo akaimbia nafsi yake: ”Hebu!” Bi maana usiionje.”

231 – Muhammad bin al-Husayn amesema: Hakiym bin Ja´far ametukhabarisha: Abu ´Umar as-Swaffaar ametuhadithia, kutoka kwa Abu Sinaan, kutoka kwa Wahb, ambaye amesema:

”Nimesoma katika vitabu vya kale kwamba utamu wa dunia ni uchungu wa Aakhirah na hakika uchungu wa dunia ni utamu wa Aakhirah, na kwamba kiu cha dunia ni kukata kiu cha Aakhirah, kukata kiu cha dunia ni kiu cha Aakhirah, na njaa ya dunia ni shibe ya Aakhirah, shibe ya dunia ni njaa ya Aakhirah, huzuni ya dunia ni furaha ya Aakhirah, furaha ya dunia ni huzuni ya Aakhirah. Yule mwenye kutanguliza mbele kitu, basi atakipata Aakhirah.”

Hakika waja wa Allaah hawaishi maisha ya kifahari. Nawaambieni kwa haki kabisa ya kwamba muovu wenu zaidi anayetenda ni mwanazuoni anayeipenda dunia na akaipa kipaumbele juu ya elimu yake. Lau angeliweza, basi angeliwafanya watu wote wafanye kama yeye.”

232 – Yuusuf bin Muusa ametuhadithia: ´Ubaydullaah bin Muusa ametuhadithia: Qatwariy al-Khashshaab ametukhabarisha, kutoka kwa Mudrik Abu Ziyaad, ambaye amesema:

”Tulikuwa kwenye bustani ya Ibn ´Abbaas, akaja al-Hasan na al-Husayn na wakaanza kuizunguka bustani ile. al-Hasan akasema: ”Je, uko na chakula cha mchana, ee Mudrik?” Nikasema: ”Chakula cha watoto.” Nikamletea siki, mkate, kunde na chumvi.” Akavila kisha baadaye akaletewa chakula chake. Chakula chake kilikuwa kingi na kizuri. Akanambia: ”Ee Mudrik,  wakusanye watoto kwenye bustani.” Wakala, lakini yeye hakula. Wakati nilipomuuliza sababu, akanambia: ”Natamani zaidi haya kuliko hicho.”

233 – ´Abdur-Rahmaan bin ´Abdillaah bin Qurayb ametuhadithia: Ami yangu amenihadithia: al-´Alaa’ bin Aslam ametuhadithia:

”Wakati ´Abdul-Kariym al-Maaziniy alipoajiriwa huko Bahrain, aliishi ardhi yenye visima vingi na akapana karamu. Katika ardhi hiyo kulikuwa mzee mmoja ambaye amejitenga. Akasimama kutoa adhaana na kuswali. Baadaye akaja mke wake na sahani yenye tende. Akala, akaja akaenda kwenye kisima, akavuta ndoo na kunywa. ´Abdul-Kariym akamtuma mjumbe aje katika karamu yetu. Bwana yule akasema: ”Nimechukua chenye kunitosha mpaka kesho  mchana.”

234 – Muhammad bin Salaam al-Jamhiy ametuhadithia:

”al-Hasan alimwalika bwana mmoja katika chakula, akasema: ”Nimeshakula na siwezi kula tena.”  Ndipo al-Hasan akasema: ”Allaah ametakasika kutokana na mapungufu! Hivi kweli muumini anakula kiasi cha kwamba hawezi kula tena?”

235 – Muhammad bin Daawuud al-Qantwariy amenihadithia:

”Tulisimama pamoja na Abu ´Abdir-Rahmaan al-Muqriy´ karibu na mzee mmoja Makkah akasema: ”Waeleze kile kisa.” Akawaeleza kisa kwa mlolongo wa wapokezi na akasema: ”Tahadharini na chakula cha wafalme. Chakula chao kina mtihani kama mtihani wa al-Masiyh ad-Dajjaal. Mwenye kukila, basi husababisha moyo wake kurudi nyuma.”

236 – Haaruun ametuhadithia: Sayyaar ametuhadithia: ´Ubaydullaah bin Shumaytw ametuhadithia: Nimemsikia Shumaytw bin ´Ajlaan akisema: Nimemsikia al-Hasan akisema:

”Yakini ya muumini ni yenye kubadilika. Kinamtosha kile kinachomtosha mbuzi mdogo; konzi moja ya tende na glasi ya maji.”

[1] Tamtam iliyotengenezwa kwa maziwa, maji na asali.

  • Mhusika: Imaam Abu Bakr ´Abdullaah bin Muhammad bin Abiyd-Dunyaa
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Kitaab-ul-Juu´, uk. 142-146
  • Imechapishwa: 31/07/2023