39. Ulazima wa walinganizi kusimama kidete kukemea shirki na kutonyamaza

Shirki Allaah ameshahukumu kuwa hatoisamehe. Vivyo hivyo mtenda madhambi muda wa kuwa ana madhambi makubwa chini ya shirki basi Pepo haiharamishwi kwake. Mafikio yake ya mwisho ni Pepo. Ima Allaah pale mwanzoni tu akamsamehe na akamwingiza Peponi na ima akamwondosha Motoni baada ya kumuadhibu na akamwingiza Peponi. Muumini vovyote atavyokuwa na madhambi chini ya shirki basi hakati tamaa kunako rehema za Allaah, haharamishiwi Pepo na anaingia chini ya msamaha kwa matakwa ya Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala). Mshirikina ameharamishiwa vyote hivo. Kwa hiyo ni dalili inayoonyesha kuwa shirki ndio dhambi kubwa. Amesema (Ta´ala):

إِنَّ الشِّرْكَ لَظُلْمٌ عَظِيمٌ

“Hakika shirki ni dhuluma kubwa mno!”[1]

وَمَن يُشْرِكْ بِاللَّـهِ فَقَدِ افْتَرَىٰ إِثْمًا عَظِيمًا

“Na yeyote atakayemshirikisha Allaah basi hakika amebuni dhambi kuu.”[2]

Yote haya yanafahamisha kuwa shirki ndio dhambi kubwa. Ikishakuwa shirki ndio dhambi kubwa hivyo basi ni lazima kwa wanachuoni na wanafunzi kuikataza na kuionya na kutonyamazia kutahadharisha shirki na kwamba ni lazima kuwafanyia jihaad washirikina kukiwepo na uwezo, kama ambavo Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alivowafanyia jihaad. Amesema (Ta´ala):

فَاقْتُلُوا الْمُشْرِكِينَ حَيْثُ وَجَدتُّمُوهُمْ وَخُذُوهُمْ وَاحْصُرُوهُمْ وَاقْعُدُوا لَهُمْ كُلَّ مَرْصَد

“Waueni washirikina popote muwakutapo, wafanyeni mateka na wahusuruni na wakalieni katika kila sehemu ya uvamizi.”[3]

Ni lazima kutahadharisha shirki na kuwabainishia nayo watu mpaka wajiepushe nayo. Hili ndio jambo la wajibu. Lakini kunyamazia shirki na kuwaacha watu wakatangatanga ndani ya kumwabudu asiyekuwa Allaah na wakati huohuo wakadai kuwa ni waislamu na hakuna yeyote anayewakataza na kuwatahadharisha ni jambo la khatari sana.

Wako watu wenye kujishughulisha kukataza ribaa, uzinzi na uharibikaji wa tabia. Ni kweli kwamba mambo haya ni haramu na ni maharibifu. Lakini shirki ni kubwa zaidi. Ni kwa nini hawatilii mkazo kukataza shirki, kutahadharisha kutokamana na shirki na kubainisha yale wanayotumbukia watu ndani yake katika shirki kubwa ilihali huku wanadai kuwa ni waislamu? Ni kwa nini wanachukulia wepesi suala hili la shirki na kupumbaa kwalo na kuwaacha watu wakatumbukia ndani yake ilihali wanachuoni wapo bali wanaishi pamoja na watu hawa na wakawanyamazia? Kwa hiyo ni lazima kujishughulisha kwanza na kukataza khatari hii kubwa iliyouangamiza Ummah vibaya sana. Kila dhambi iliochini yake ni ndogo kuliko hiyo. Lililo la wajibu ni kuanza na la muhimu zaidi kisha kuyaendea ya muhimu mengine baada ya hilo.

[1] 31:13

[2] 04:48

[3] 09:05

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Thalaathat-il-Usuwl, uk. 86-87
  • Imechapishwa: 14/12/2020