Swali: Ni ipi hukumu ya kilichookotwa msikiti Mtakatifu wa Makkah? Je, inafaa kukitoa kwa ajili ya mafukara ama kwa mfano kukitoa kwa ajili ya kujenga msikiti?

Jibu: Kilicho cha wajibu kwa yule mwenye kuokota kitu msikiti Mtakatifu wa Makkah basi asikitoe kwa ajili ya kujenga msikiti, asiwape mafukara wala wengineo. Bali daima anatakiwa akitangaze pale Haram katika mikusanyiko ya watu hali ya kuwa ni mwenye kuita kwa sauti ni nani mwenye pesa hizo, ni nani mwenye dhahabu hiyo na mfano wa hivo. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

”Hakihalaliki kilichookotwa isipokuwa baada ya kukitangaza… ”

Katika upokezi mwingine imekuja:

”… isipokuwa kwa yule mtangazaji… ”

Bi maana ambaye amekitangaza.

Hivyo hivyo msikiti Mtakatifu wa al-Madiynah. Ni sawa pia akikiacha mahali pake. Akikipeleka katika kamati rasmi iliyotengwa na nchi kwa ajili ya kuhifadhi vilivookotwa basi dhimma yake itakuwa imetakasika.

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Majmuu´-ul-Fataawaa (06/499)
  • Imechapishwa: 14/12/2020