39. Dalili kuthibitisha kuwa kurejea ni ´ibaadah

Shaykh-ul-Islaam Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab (Rahimahu Allaah) amesema:

Dalili ya kurejea ni Kauli Yake (Ta´ala):

وَأَنِيبُوا إِلَىٰ رَبِّكُمْ وَأَسْلِمُوا لَهُ مِن قَبْلِ أَن يَأْتِيَكُمُ الْعَذَابُ ثُمَّ لَا تُنصَرُونَ

“Rejeeni kwa Mola wenu na jisalimisheni Kwake kabla haijakufikieni adhabu kisha hamtonusuriwa.”[1]

Dalili ya kutaka msaada ni Kauli Yake (Ta´ala):

إِيَّاكَ نَعْبُدُ وَإِيَّاكَ نَسْتَعِينُ

”Wewe Pekee tunakuabudu na Wewe Pekee tunakuomba msaada.”[2]

Katika Hadiyth pia imekuja:

“… unapotaka msaada, basi mtake msaada Allaah.”[3]

MAELEZO

Kurejea maana yake ni kurudi kwa Allaah hali ya kutubia na kumtakasia nia. Mtu anarejea kwa Allaah pekee. Kwa maana nyingine haifai kwa mtu kurejea kwa mwingine asiyekuwa Allaah katika viumbe na wala asitubie kwake na akamuomba amsamehe madhambi yake, kama wanavofanya manaswara. Manaswara hutubu kwa mapadiri ambapo kwa madai yao wakawasamehe na wakawapa kadi za kuingia Peponi. Vivyo hivyo baadhi ya Shiy´ah hurejea kwa Mashaykh zao ambapo kwa madai yao eti wakawasamehe madhambi yao, kitendo ambacho ni cha shirki. Amesema (Ta´ala):

 وَمَن يَغْفِرُ الذُّنُوبَ إِلَّا اللَّـهُ

”Na nani anayesamehe madhambi isipokuwa Allaah.”[4]

Maneno Yake (Ta´ala):

إِيَّاكَ نَعْبُدُ وَإِيَّاكَ نَسْتَعِينُ

”Wewe Pekee tunakuabudu na Wewe Pekee tunakuomba msaada.”

Ametanguliza kiwakilishi kabla ya kitenzi ili ifidishe ufupikaji. Kwa maana nyingine Aayah inasema kuwa tunakuabudu Wewe, ee Allaah, na wala hatumuabudu mwingine na tunakutaka msaada Wewe na hatumtaki msaada mwingine. Ndio maana ya hapana mungu isipokuwa Allaah. Hili linafahamika kwa kutanguliza kielezi. Kwa sababu kilicholengwa ni ule upekee. Lau ingelikuwa:

نعبدك

“Tunakuabudu.”

au:

نستعينك

“Tunakuomba msaada.”

unaondoka ule upekee. Lakini ilipokuja kama ilivyo maana yake ikawa tunakuabudu Wewe pekee ndiye tunakuabudu na wala hatumuabudu mwingine asiyekuwa Wewe, na Wewe pekee ndiye tunakuomba msaada na wala hatumuombi msaada mwingine asiyekuwa Wewe. ´Ibaada ya kuombwa msaada ni haki ya Allaah. Kama ambavyo anayemwabudu Allaah ameingia katika shirki basi vivyo hivyo kuomba msaada. Yule mwenye kumuomba msaada asiyekuwa Allaah ameshirikisha.

Kutanguliza ´ibaadah kabla ya kuomba msaada ni kwa kwa njia ya kutanguliza kilichoenea zaidi kabla ya kitu maalum. Pia ni kutilia mkazo juu ya kutanguliza haki Yake kabla ya haki ya mwingine. Ametaja kuomba msaada baada ya ´ibaadah – licha ya kwamba kuomba msaada kunaingia ndani ya ´ibaadah – kwa sababu mja katika ´ibaadah zake zote anahitaji kumtaka msaada Allaah (Ta´ala). Kwani Allaah asimpomsaidia basi hatoyafikia yale anayoyataka katika kufanya yaliyoamrishwa na kujiepusha na yaliyokatazwa. Hayo yamesemwa na Shaykh ´Abdur-Rahmaan as-Sa´diy (Rahimahu Allaah)[5].

Mtunzi wa kitabu (Rahimahu Allaah) amesema:

Katika Hadiyth pia imekuja:

“… unapotaka msaada, basi mtake msaada Allaah.”

Makusudio ya msaada hapa ni kwa njia ya ´ibaadah. Hapana vibaya mtu kuomba msaada katika mambo ya kawaida. Kwa mfano hapana vibaya ukamuomba mwenzako akusaidie kutengeneza gari yako, kupalilia shamba lako na kukulipia deni lako. Kwa sharti huyo unayemuomba yuko hai, mbele yako na anaweza kukusaidia. Kumeshatangulia upambanuzi juu ya suala hili.

[1] 39:54

[2] 01:05

[3] at-Tirmidhiy (2516) ambaye amesema:

”Hadiyth ni nzuri na Swahiyh.”

[4] 03:135

[5] Tazama ”Taysiyr-ul-Kariym-ir-Rahmaan” (01/32).

  • Mhusika: ´Allaamah ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah ar-Raajihiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Thalaathat-il-Usuwl, uk. 63-64
  • Imechapishwa: 11/02/2023