38. Ni yepi maoni yenu kwa wale vijana ambao wanawatukana watawala wa nchi hii katika vikao vyao?

Swali 38: Ni yepi maoni yenu kwa wale vijana ambao wanawatukana watawala wa nchi hii katika vikao vyao?

Jibu: Haya yanatambulika kuwa ni batili. Hawa ima wanakusudia shari au wameathirika na wengine miongoni mwa wale watu wa linganizi zinazopotosha ambao wanachotaka ni kuondoka neema hizi ambazo tunaishi ndani yake.

Sisi tunawaamini watawala wetu. Tunaamini ule mfumo ambao tunafuata. Hiyo haina maana kuwa tumekamilika au kwamba hatuna mapungufu. Bali tuna mapungufu, lakini tuko tunayarekebisha na kuyatatua – Allaah akitaka – kwa njia zilizowekwa katika Shari´ah.

Wakati wa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) walikuwepo wezi. Walikuwepo wanaozini na walikuwepo wanaokunywa pombe. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) aliwasimamishia adhabu zilizowekwa katika Shari´ah. Sisi tunasimamisha adhabu zilizowekwa katika Shari´ah kwa wale wanaozistahiki. Tunawaua wauaji. Hili ni jambo la kheri ingawa kuna mapungufu[1]. Mapungufu ni lazima yawepo kwa sababu ndio maumbile ya mwanadamu. Tunamuomba Allaah azitengeneze hali zetu, atusaidie juu ya nafsi zetu, atuongoze na ayakamilishe mapungufu yetu kwa msamaha Wake.

Ama kutumia mapungufu na makosa ya watawala kuwa ni fursa ya kuwatia upungufu, kuwatukana au kuwafanya raia kuwachukia sio katika njia za Salaf na Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah[2]. Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah wanahimiza kumtii mtawala wa waislamu, kuwafanya raia kumpenda na kuwa na umoja. Mambo yanatakiwa kuwa namna hii. Kuwatukana watawala ni katika usengenyi na umbea. Madhambi hayo mawili ni miongoni mwa madhambi khatari zaidi baada ya shirki na khaswa ikiwa wanaosengenywa ni wanazuoni na watawala. Madhambi hayo ni khatari zaidi kutokana na yale madhara yanayopelekea kukiwemo kufarikisha umoja, kuwadhania vibaya watawala na kueneza ukataji tamaa ndani ya nyoyo za watu[3].

[1] Hili linaonekana katika nchi yetu na linafanyiwa kazi katika mahakama zetu. Hakuna anayelipinga isipokuwa yule ambaye Allaah amempofosha macho yake au mtu ambaye moyoni mwake kuna ugonjwa na matamanio.

[2] ´Allaamah ´Abdul-´Aziyz bin Baaz (Rahimahu Allaah) aliulizwa swali lifuatalo:

”Je, ni miongoni mwa mfumo wa Salaf kuwakosoa watawala juu ya mimbari? Ni upi mfumo wa Salaf katika kuwanasihi watawala?”

Akajibu (Rahimahu Allaah):

”Si katika mfumo wa Salaf kuzianika kasoro za watawala na kuyataja hayo juu ya mimbari. Kwa sababu jambo hilo linapelekea katika vurugu ambazo zinadhuru na wala hazinufaishi.

Mfumo ambao ni wenye kufuatwa kwa Salaf ni kumnasihi kwa siri, kumwandikia na kuwasiliana na wanazuoni ambao wanaweza kumnasihi ili wamwongoze katika kheri.” (Muhadhara ”Aafaat-ul-Lisaan”, 1413-02-29)

Shaykh Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn (Rahimahu Allaah) amesema:

”Miongoni mwa haki za watawala kwa wananchi ni kuwanasihi, kuwaongoza na wasitumie makosa yao pindi wanapokosoa kuwa ni fursa ya kuwatukana na kueneza kasoro zao kati ya watu. Hayo yanasababisha watu kuwakimbia na kuwachukia na kuyachukia yale matendo wanayofanya hata kama yatakuwa ya haki. Aidha kitendo hicho kinasababisha kutosikilizwa na kutiiwa. Jambo la wajibu kwa kila mwenye kutoa nasaha, na khaswa yule anayewanasihi watawala, atumie hekima katika nasaha zake na alinganie katika njia ya Mola wake kwa hekima na mawaidha mazuri.” (Huquuq-ur-Raa´iy war-Ra´iyyah, uk. 11)

Wanazuoni hawa watukufu wameyajenga maneno yao juu ya mwongozo wa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na juu ya ufahamu wa Salaf. Mfano wa Hadiyth hizo Swahiyh ni Hadiyth ya ´Iyaadh bin Ghunm (Radhiya Allaahu ´anh) kutoka kwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ambaye amesema:

”Yeyote ambaye yuko na nasaha kwa mtawala basi asiseme hadharani. Badala yake amshike mkono wake na akae naye chemba. Akikubali amekubali na vinginevyo ametekeleza jukumu lake na haki yake.” (Ahmad (3/404), Ibn Abiy ´Aaswim (1096) na al-Haakim katika ”al-Mustadrak” (3/290). al-Haythamiy ameitaja katika ”Majma´-uz-Zawaa-id” (5/229) kwa tamko lisemalo: ”Yule anayetaka kumnasihi.. ”Tamko hilo limepokelewa na al-Haakim na ni nzuri.)

al-Bukhaariy amepokea katika ”as-Swahiyh” yake kupitia kwa Abu Waa-il Shaqiyq na pia Muslim:

”Usaamah bin Zayd aliambiwa: ”Ni kwa nini humwendei ´Uthmaan?” Akajibu: ”Nyinyi mnaona kuwa mimi simzungumzishi mpaka nikusikilizisheni. Mimi namzungumzisha kwa siri.”

Imekuja kwa Muslim:

”Ni kwa nini humwendei ´Uthmaan umzungumzishe?” Akajibu: ”Naapa kwa Allaah nimezungumza naye katika yale yaliyoko kati yangu mimi na yeye pasi na kufungua mlango ambao sipendi kuwa wa kwanza kuufungua.” (al-Bukhaariy (3094) na (6675) na Muslim (2989))

Haafidhw Ibn Hadjar (Rahimahu Allaah) amesema:

”al-Muhallab amesema: ”Walitaka Usaamah amzungumzishe ´Uthmaan. Alikuwa ni mmoja katika watu wake wa karibu na ambaye alikuwa anazumgumza naye kuhusiana na jambo la al-Waliyd bin ´Uqbah ambaye alikuwa anatambulika kwa harufu ya mvinyo. Bwana huyu alikuwa ni ndugu yake na ´Uthmaan upande wa mama yake na alikuwa akimwajiri. Usaamah akamjibu: ”Nimezumgumza naye kwa siri pasi na kufungua mlango.” Bi maana mlango wa kuwakaripia viongozi hadharani kwa kuchelea kusitokee mpasuko.”

´Iyaadhw amesema: ”Alichokusudia Usaamah ni kuwa hataki kufungua mlango wa kuwakaripia hadharani viongozi kwa kuchelea matokeo yanayopelekea huko. Bali mtu anatakiwa kuwafanyia upole na kuwanasihi kwa siri. Kufanya hivo kuna asilimia kubwa ya wao kukubali nasaha.” (Fath-ul-Baariy (13/52))

Imamu wa Ahl-us-Sunnah Imaam Ahmad bin Hanbal (Rahimahu Allaah) alipigwa mijeledi, akaburuzwa na akafungwa wakati wa mtihani wa kuumbwa kwa Qur-aan. Licha ya hivyo hatupati upokezi hata mmoja ijapo dhaifu akihimiza kufanya uasi kwa mtawala mtenda dhambi na mwenye kudhulimu. Bali mapokezi kutoka kwake yanayoamrisha kulazimiana na subira, kutii na mkusanyiko yanatambulika na ni mengi mno. Isitoshe alikuwa akisema ”Ee kiongozi wa waumini!” Je, alikuwa akifanya hivo kinafiki au kwa woga? Je, sisi hatuna kiigizo chema kwa Salaf? Au sisi ni wajuzi na wajasiri zaidi kuliko wao?

Imaam Ibn Rajab al-Hanbaliy (Rahimahu Allaah) amesimulia kuwa Ibn-us-Swalaah amesema:

”Kuwatakia mema viongozi wa waislamu maana yake ni kuwasaidia katika haki, kuwatii juu yake, kuwakumbusha nayo, kuwazindua kwa upole na urafiki, kuepuka kuwashambulia, kuwaombea kufanikiwa na kuwahimiza watu wenye ghera juu ya jambo hilo.” (Jaamiy´-ul-´Uluum wal-Hikam, uk. 113)

Imaam ash-Shawkaaniy amesema:

”Imethibiti ndani ya Kitabu kitukufu amri ya kumtii mtawala. Allaah ameamrisha mtawala kutiiwa baada ya kuamrisha kumtii Yeye (Subhaanah) na kumtii Mtume Wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Katika Sunnah iliyotakasika kuna mapokezi tele yanayoashiria kuwa ni wajibu kuwatii na kusubiri juu ya dhuluma zao. Baadhi ya Hadiyth zinazoamrisha kuwatii watawala zinasema:

”Msikilize na umtii kiongozi hata kama atakupiga mgongo wako na kuchukua mali yako.”

Imesihi kutoka kwake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kuwa amesema:

”Wapeni kilicho chao na muombeeni Allaah kilicho chenu.” (Raf´-ul-Asaatwiyn fiy Hukm-il-Ittiswaal bil-Salaatwin, uk. 81-82)

[3] Baadhi ya wale wanaojinasibisha na elimu na kujiteua wao wenyewe kuwa ni walinganizi wameeneza shaka juu ya wanazuoni na watawala wetu. Matokeo yake baadhi ya vijana wajinga na waliodanganyika nao wakapotea kuiacha njia ya sawa. Wakawapa mgongo wanazuoni kama mfano wa Kibaar-ul-´Ulmaaa nchini mwetu kwa kiasi cha kwamba pindi mtu anaposema kuwa Shaykh fulani amesema au ametoa fatwa ya kitu fulani, basi wanajibu kwamba hao ni wanazuoni wa utawala na wanaojikombakomba au kwamba hao wana shinikizo kutoka serikalini. Katika zama za mwisho watu wajinga ndio watakuwa wakiyazungumzia mambo yanayohusu ummah.

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-Ajwibah al-Mufiydah ´an As-ilat-il-Manaahij al-Jadiydah, uk. 112-116
  • Imechapishwa: 26/02/2024
  • taaliki: Shaykh Jamaal bin Furahyaan al-Haarithiy