Swali 39: Muhammad bin Qutwb ameandika katika kitabu chake ”Hawl Tatwbiyq-ish-Shariy´ah” ya kwamba ”hapana mungu wa haki isipokuwa Allaah” maana yake ni kuwa hapana mwabudiwa isipokuwa Allaah na kwamba hakuna hakimu isipokuwa Allaah[1]. Je, tafsiri hii ni sahihi?

Jibu: Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala) amebainisha maana ya shahaadah ndani ya Kitabu Chake. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) pia amebainisha maana yake. Allaah (Ta´ala) amesema:

وَاعْبُدُوا اللَّـهَ وَلَا تُشْرِكُوا بِهِ شَيْئًا

“Mwabuduni Allaah na wala msimshirikishe na chochote.”[2]

وَلَقَدْ بَعَثْنَا فِي كُلِّ أُمَّةٍ رَّسُولًا أَنِ اعْبُدُوا اللَّـهَ وَاجْتَنِبُوا الطَّاغُوتَ

“Hakika Tulituma katika kila ummah Mtume [awaamrishe watu wake] kwamba: “Mwabuduni Allaah na jiepusheni na Twaaghuut.””[3]

وَمَا أُمِرُوا إِلَّا لِيَعْبُدُوا اللَّـهَ مُخْلِصِينَ لَهُ الدِّينَ حُنَفَاءَ وَيُقِيمُوا الصَّلَاةَ وَيُؤْتُوا الزَّكَاةَ

“Hawakuamrishwa jengine isipokuwa wamuabudu Allaah pekee hali ya kumtakasia yeye dini, wenye kupondoka kwenye haki na kuiacha batili, na wasimamishe swalah na watoe zakah.”[4]

Allaah (Ta´ala) amesema kuhusu Ibraahiym (´alayhis-Salaam):

وَإِذْ قَالَ إِبْرَاهِيمُ لِأَبِيهِ وَقَوْمِهِ إِنَّنِي بَرَاءٌ مِّمَّا تَعْبُدُونَ إِلَّا الَّذِي فَطَرَنِي فَإِنَّهُ سَيَهْدِينِ

“Ibraahiym alipomwambia baba yake na watu wake: “Hakika mimi ni mwenye kujiweka mbali kabisa na yale mnayoyaabud. Isipokuwa Ambaye ameniumba, basi hakika Yeye ataniongoza.”[5]

Hii ndio maana ya ´hapana mungu isipokuwa Allaah`. Allaah (Ta´ala) amesema:

وَمَا خَلَقْتُ الْجِنَّ وَالْإِنسَ إِلَّا لِيَعْبُدُونِ

“Na Sikuumba majini na wanadamu isipokuwa waniabudu.”[6]

Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

”Nimeamrishwa kuwapiga watu vita mpaka washuhudie ya kwamba hapana mungu  wa haki isipokuwa Allaah.”

Imekuja katika upokezi mwingine:

”Nimeamrishwa kuwapiga watu vita mpaka wampwekeshe Allaah.”[7]

Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akabainisha kuwa maana ya ´hapana mungu isipokuwa Allaah` maana yake ni kumpwekesha Allaah kwa aina zote za ´ibaadah na si hukumu peke yake. Kwa hivyo maana ya ´hapana mungu isipokuwa Allaah` ni kwamba hapana mwabudiwa wa haki isipokuwa Allaah. Maana yake ni kumtakasia ´ibaadah Allaah pekee. Kunaingia ndani yake kuhukumu kwa Shari´ah. Maana ya ´hapana mungu wa haki isipokuwa Allaah` ni yenye kuenea na kubwa zaidi kuliko hukumu peke yake. Muhimu zaidi ni kuondosha shirki katika uso wa ardhi na kumwabudu Allaah pekee (Subhaanah) kuliko kuhukumu kwa Shari´ah katika magomvi. Hii ndio tafsiri sahihi.

Kuifupisha maana yake katika hukumu peke yake ni tafsiri pungufu. Si maana pekee ya shahaadah. Ama kufasiri ´hapana mungu wa haki isipokuw Allaah´ kwamba maana yake ni kuwa hapana muumbaji isipokuwa Allaah, ni tafsiri batili na haikufupika katika hilo peke yake. Kwa sababu ´hapana mungu wa haki isipokuw Allaah´ haikuja kuthibitisha kuwa hapana muumbaji isipokuwa Allaah. Kwani hili linakubaliwa na washirikina. Endapo maana yake ingelikuwa ni hapana muumbaji isipokuwa Allaah basi washirikina wangelikuwa wapwekeshaji. Allaah (Ta´ala) amesema:

وَلَئِن سَأَلْتَهُم مَّنْ خَلَقَهُمْ لَيَقُولُنَّ اللَّهُ

“Ukiwauliza: “Ni nani kawaumba?” Bila shaka watasema: “Allaah.”[8]

Maana yake ni kwamba Abu Jahl na Abu Lahab ni wapwekeshaji.

Vivyo hivyo kufasiri ya kwamba maana yake ni kuwa hapana mwabudiwa isipokuwa Allaah ni tafsiri batili pia. Tafsiri kama hiyo inapelekea katika ile imani ya kuona kila kilichopo ni mungu. Kuna waungu wengi wanaoabudiwa kukiwemo masanamu na makaburi. Je, kuabudiwa kwa vitu hivyo anaabudiwa Allaah?

Tafsiri ya wajibu ni kusema kwamba hapana mwabudiwa wa haki isipokuwa Allaah. Allaah (Ta´ala) amesema:

ذَٰلِكَ بِأَنَّ اللَّـهَ هُوَ الْحَقُّ وَأَنَّ مَا يَدْعُونَ مِن دُونِهِ هُوَ الْبَاطِلُ وَأَنَّ اللَّـهَ هُوَ الْعَلِيُّ الْكَبِيرُ

“Hivyo ni kwa kuwa Allaah ndiye wa haki na kwamba vile wanavyoomba badala Yake ndiyo batili na kwamba Allaah ndiye Aliye juu kabisa, Mkubwa.”[9]

[1] Anasema hivo sehemu mbili katika kitabu kilichotajwa. Tazama kurasa 81-82. Ameikariri maana hiyo katika kitabu chake ”Waaqi´unaa al-Mu´aaswir” na anasema kuhusu kile anachokiita ´Jaaliyyah ya leo`:

”Watu wanahitaji kulinganiwa katika Uislamu. Lakini mara hii hawalinganiwi katika Uislamu kwa sababu wamekataa kutamka shahaadah, kama walivofanya mara ya kwanza. Mara hii wanalinganiwa kwa sababu wanakataa kile kinachopelekea katika shahaadah hiyo, nayo ni kuhukumu kwa Shari´ah.”  (Waaqi´unaa al-Mu´aaswir, uk. 29)

[2] 4:36

[3] 16:36

[4] 98:5

[5] 43:26-27

[6] 51:56

[7] al-Bukhaariy (1335) na (2786) na at-Tirmidhiy (2606).

[8] 43:87

[9] 22:62

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-Ajwibah al-Mufiydah ´an As-ilat-il-Manaahij al-Jadiydah, uk. 116-118
  • Imechapishwa: 26/02/2024
  • taaliki: Shaykh Jamaal bin Furahyaan al-Haarithiy