37. Ni ipi hukumu ya uigizaji wa Kiislamu na Anaashiyd za Kiislamu ambayo hufanywa na baadhi ya vijana katika kambi za kiangazi?

Swali 37: Ni ipi hukumu ya uigizaji wa Kiislamu na Anaashiyd za Kiislamu ambayo hufanywa na baadhi ya vijana katika kambi za kiangazi?

Jibu: Sioni kuwa uigizaji[1] unafaa kutokana na sababu zifuatazo:

1 – Ni kuwapumbaa[2] hadhira wanaomwangalia mwigizaji na kucheka[3]. Mara nyingi lengo la uigizaji ni burudani peke yake na kufanya hadhira wakapumbaa na hakuna jengine.

2 – Pengine wale watu wanaoigilizwa ni katika watu wenye shakhsia wakubwa wa Kiislamu kwa mfano Maswahabah. Huku kunahesabika ni kumtia upungufu[4] ni mamoja mtu amelihisi hilo au hakulihisi. Kwa mfano haijuzu kwa mtoto au mtumzima mwenye muonekano mbaya kumwigiliza mwanachuoni miongoni mwa wanazuoni au mmoja katika Maswahabah kwa sababu ni kumtia upungufu moja katika shakhsia za Kiislamu kupitia mtu ambaye ni mtenda dhambi au mwigizaji anayesimangwa.

Je, wewe unaridhia awepo mtu anayekuigiliza katika namna ya kutembea au uzungumzaji wako? Au utachukulia hivo ni kukutia upungufu? Hata kama yule mwigizaji atadai kuwa anakusudia kheri, lakini watu hawaridhii watu wawatie mapungufu.

3 – Sababu hii ni khatari zaidi, nayo ni kuwa baadhi yao wanaigiliza shakhsia za makafiri, kama vile Abu Jahl na Fr´awn, na wanazungumza maneno yao ya kikafiri. Wanadai kuwa wanataka kuwaraddi au kuonyesha namna ilivyokuwa katika kipindi kabla ya kuja Uislamu. Huku ni kujifananisha na wao na Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amekataza kujifananisha na washirikina na makafiri[5]. Hiajalishi kitu ni kujifananisha katika shakhsia zao au katika maneno yao.

4 – Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) hakulingania kwa njia hiyo. Wala sio katika mwongozo wa Salaf wala waislamu wa kale.

Maigizo haya hayatambuliki isipokuwa kutoka nje, kutoka kwa makafiri. Tumepenyezewa nazo kupitia jina la ulinganizi wa Kiislamu. Si sahihi kuzizingatia kuwa ni katika njia za ulinganizi. Njia za ulinganizi zinapaswa kuafikiana na Qur-aan na Sunnah[6]. Hazihitaji mfumo huu. Katika zama zote ulinganizi ulikuwa wenye kufanikiwa pasi na maigizo haya. Maigizo haya hawakuwanufaisha na wala hayakuwaathiri kitu. Hayo yanafahamisha kuwa ni hasi, hakuna ndani yake faida bali yana madhara.

Pengine akawepo mtu mwenye kusema kuwa Malaika hujionyesha katika umbile la mwanadamu, ni kwa sababu mtu hawezi kumwangalia Malaika anapokuwa katika umbile lake la asili. Hili ni kwa manufaa ya mwanadamu. Endapo Malaika wangelikuja katika maumbile yao ya asili basi mwanadamu asingeweza kuwazungumzisha wala kuwatazama[7]. Lengo la Malaika wanapojigeuza sio kuigiza, kama wanavomaanisha hawa. Malaika hujigeuza katika umbile la kimtu kwa ajili ya manufaa ya mtu mwenyewe kwa sababu Malaika wanayo maumbile yanayotofautiana na maumbile ya mwanadamu. Lakini ni kwa nini mwanadamu ajigeuze umbile la mtu mwingine? Kuna faida gani ya kufanya hivo?

[1] Shaykh Bakr Abu Zayd amesema:

”Wahakiki wengi wamefikia kwamba uigizaji ni miongoni mwa ´ibaadah za kipagani kwa wagiriki.” (at-Tamthiyl, uk. 18)

Shaykh-ul-Islaam Ibn Taymiyyah amesema wakati alipokuwa akitaja matendo ya manaswara katika jumapili ya mitende:

”Wanatoa nje majani ya mzeituni na mfano wake na wanadai kuwa kufanya hvio ni kujifananisha na yale yaliyompitikia al-Masiyh.” (Iqtidhwaa’-us-Swiraatw al-Mustaqiym, uk. 191)

Haya yamenukuliwa na Shaykh Bakr Abu Zayd katika ”at-Tamthiyl”. Shaykh Bakr Abu Zayd amesema tena katika kitabu hichohicho:

”Ukishajua kuwa uigizaji haukuwepo kati ya vile vizazi bora vya Uislamu, zilikuja baadaye na kwamba zilipokelewa na kumbi za pumbao na sinema katika karne ya 14 H kisha baadaye zikajipenyeza kutoka katika makanisa ya manaswara na kwenda kwa watu walioziita ”maigizo ya kidini” katika mashule na baadhi ya makundi ya Kiislamu, basi utambue pia kuwa kanuni na misingi ya Shari´ah inayowapindisha wenye nayo katika ngazi ya utukufu na heshima zinayatupilia mbali mambo hayo.

Ni jambo linalotambulika kuwa matendo ima yawe ´ibaadah au desturi. Msingi ni kwamba ´ibaadah haiwi Shari´ah isipokuwa yale yaliyowekwa katika Shari´ah na Allaah na msingi katika mambo ya desturi hayakatazwi isipokuwa yale yaliyokatazwa na Allaah… Kujengea juu ya hilo haijuzu kumwabudu Allaah kwa maigizo ya kidini au kuyafanya kwa njia ya kujistarehesha nayo. Hakuna hoja yoyote ya ki-Shari´ah juu ya maigizo ya kidini. Ni mfumo uliyozuliwa. Moja mionogoni mwa istilahi za Uislamu zilizokusanya ni maneno yake Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

”Yule atakayefanya kitendo kisichoafikiana na amri yetu, atarudishiwa mwenyewe.” (Muslim (1718))

Ukishajua msingi wa uigizaji, kwamba zimejitokeza kati ya waislamu pasi na dalili inayokubalika katika Shari´ah, kwamba ni miongoni mwa ´ibaadah za waabudia masanamu wa kigiriki na wa kinaswara, utajua pia kuwa yale maigizo ya kidini unayoyaona katika baadhi ya mashule na vyuo vikuu si jengine isipokuwa ni uigizaji uliyozuliwa. Kwa sababu hazina msingi kabisa ndani ya Uislamu. Kwa hivyo ni uzushi. Kila kitu kilichozuliwa ndani ya dini ni uzushi unaokinzana na Shari´ah. Kwa ajili hiyo ni sahihi kabisa kuziita ”uigizaji wa kizushi”.

Kuhusu uigizaji wa kidesturi, huko ni kujifananisha na maadui wa Allaah makafiri. Kwa sababu maigizo hayatambuliki isipokuwa kupitia wao na tumekatazwa kujifananisha na wao.

Mfano wa makundi yanayoashiriwa hapo juu ni al-Ikhwaan al-Muslimuun.

Yale yanayoitwa maigizo ya Kiislamu yanayochezwa katika kambi za kiangazi na katika mashule yanazingatiwa ni moja katika njia za kulingania na zinawaathiri vijana walionao. Huo ni mtazamo wao, lakini unakataliwa na Shari´ah. Njia na mifumo ya ulinganizi ni lazima iafikiane na Qur-aan na Sunnah. Haifai kwa yeyote kujizushia chochote kutoka kwake.

Mtu akisema kuwa njia za ulinganizi zinatokana na manufaa yaliyoachiwa, basi tutamuuliza kama kuna manufaa ambayo Shari´ah imepuuza juu ya waja? Shaykh-ul-Islaam Ibn Taymiyyah anajibu swali hili na kusema:

” Shari´ah kamwe haipuuzi manufaa yoyote yale. Bali Allaah (Ta´ala) ametukamilishia dini yetu na akatuacha katika njia ya wazi kabisa usiku wake ni kama mchana wake. Hakuna anayepinda kutokana nayo isipokuwa mwangamivu.” (al-Hujaj al-Qawiyyah ´alaa anna Wasaa-il-ad-Da´wah Tawqiyfiyyah, uk. 40, ya Shaykh ´Abdus-Salaam bin Barjas)

Ni kwa nini mlinganizi aende katika mifumo ambayo haikutajwa katika Shari´ah ikiwa kuna wengi katika watu ambao wametubia kutokana na kufuru, madhambi na maasi kupitia njia zilizowekwa katika Shari´ah? Yale yaliyopo katika Shari´ah ni yenye kutosheleza ili kuyafikia malengo ya ulinganizi,  nayo ni kumfanya mtenda dhambi kutubia na mpotofu kuongoka. Wale wanaolingania kwa Allaah watosheke na yale yaliyomtosheleza Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na Maswahabah zake (Radhiya Allaahu ´anhum). Walifanya kila kitu kwa elimu. Ibn Mas´uud (Radhiya Allaahu ´anh) amesema:

”Enyi watu! Hakika mtakuja kuzusha na mtakuja kuzushiwa. Mtakapoona kilichozuliwa, basi lazimianeni na lile jambo la kwanza.”

Amesema tena:

“Na nakutahadharisheni na mambo ya uzushi, nakutahadharisheni na kuchupa mipaka, nakutahadharisheni na kuingia ndani zaidi. Lazimiane na lile jambo la kwanza.” (Twabaqaat-ul-Hanaabilah (1/69-71))

Shaykh ´Abdus-Salaam amesema:

“Ni vigumu kuweka kikomo cha manufaa katika jambo fulani. Mtazamaji anaweza kufikiri kuwa kitu fulani ni manufaa lakini mambo yakawa sivo hivyo. Kwa ajili hiyo wanazuoni pekee na wenye upeo wa kufanya Ijtihaad na ambao wako na uadilifu na uoni wa mbali juu ya hukumu za Shari´ah na manufaa ya kilimwengu ndio wanaostahiki kuamua ni kipi chenye manufaa yaliyoachiwa. Kwa sababu uwezo huo unahitaji “hadhari ya hali ya juu na uangalifu mkubwa wa kuzidiwa na matamanio. Mara nyingi matamanio huyapambia madhara ambapo yakayaona ni manufaa, na mara nyingi hudanganyika kwa mambo ambayo madhara yake ni makubwa zaidi kuliko manufaa yake. Ni vipi mtu anayefuata kichwa mchunga atadai dhana kubwa kwamba manufaa haya yanafikia malengo ya dini na kwamba hakuna katika dini kinachopingana nayo wala kitu kinachojulisha kutosihi kwake? Ijapokuwa hakufanya utafiti kwenye dalili wala hakutafiti yaliyomo ndani yake. Ni kitu gani hiki kama sio kuwa na ujasiri juu ya dini na kuiparamia hukumu ya Shari´ah pasi na yakini?”

Amemnukuu Shaykh Hamuud bin ´Abdillaah at-Tuwayjiriy (Rahimahu Allaah) ambaye amesema:

“Kuigiza wakati wa kulingania kwa Allaah (Ta´ala) sio katika Sunnah za Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) wala Sunnah za makhaliyfah wake waongofu na walioongozwa. Maigizo ni miongoni mwa mambo yaliyozuliwa katika zama zetu. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ametahadharisha mambo yaliyozuliwa na akaeleza kurudishwa kwake nyuma na akaeleza kuwa ni maovu na upotofu.” (al-Hujjaj al-Qawiyyah, uk. 54-55)

[2] Ni kupoteza muda pia. Muislamu anawajibika juu ya wakati wake. Anapaswa kuuhifadhi na kufaidika nao katika yale yanayomridisha Allaah (´Azza wa Jall) na kumnufaisha duniani na Aakhirah. Abu Barzah al-Aslamiy (Radhiya Allaahu ´anh) amesimulia kuwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Haitovuka miguu ya mja siku ya Qiyaamah mpaka aulizwe juu ya mambo manne: umri wake aliuteketeza katika mambo gani, elimu yake aliifanyia nini, mali yake aliipata kivipi na akaitumia wapi na mwili wake aliutumia vipi?”  (at-Tirmidhiy (2417) ambaye pia ameisahihisha).

[3] Mara nyingi uigizaji ni uwongo. Bali uigizaji ni uwongo mtupu ima kwa sababu ya kutaka kuamsha hisia za hadhira na kuwaathiri watazamaji au kutaka kuwachekesha. Uigizaji unatokana na visa vya kutungatunga. Kumepokelewa matishio makali kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kwa ambaye anasema uwongo ili kutaka kuwachekesha watu. Mu´aawiyah bin Haydah (Radhiya Allaahu ´anh) amesimulia kuwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Ole wake yule anayesema uwongo ili awachekeshe watu. Ole wake! Ole wake!” (Ahmad (5/3-5), at-Tirmidhiy (2315) na al-Haakim (1/46)).

Hadiyth ni nzuri.

Shaykh-ul-Islaam Ibn Taymiyyah amesema baada ya Hadiyth hii:

”Ibn Mas´uud amesema:

”Uwongo haufai katika hali ya kumaanisha kweli au mzaha.”

Ikiwa uwongo huo pia unaleta mashambulizi dhidi ya waislamu na kuidhuru dini basi uharamu wake unakuwa khatari zaidi. Kwa hali yoyote anayefanya hivo (yaani anayewachekesha watu kwa kutumia uwongo) anastahiki adhabu ya Kishari´ah itayomfanya kukoma kutokana na jambo hilo.” (Majmuu´-ul-Fataawaa (32/256))

Ama yanayohusiana na visa, Salaf wamechukiza jambo hilo na vikao vya visa. Wametahadharisha jambo hilo kwa ukali na wakawapiga vita wapiga visa kwa njia mbalimbali. Tazama ”al-Mudhakkir wat-Tadhkiyr wadh-Dhikr”, uk. 26, cha Ibn Abiy ´Aaswim kwa ukaguzi wa Khaalid ar-Raddaadiy.

Ibn Abiy ´Aaswim amepokea kwa cheni ya wapokezi Swahiyh ya kuwa ´Aliy (Radhiya Allaahu ´anh) alimuona bwana mmoja alisimulia visa. Akamuuliza: ”Je, wewe una elimu juu ya chenye kufuta na kilichofutwa?” Bwana yule akasema: ”Hapana.” Ndipo ´Aliy akasema: ”Umeangamia na kuangamiza wengine.”  (al-Mudhakkir wat-Tadhkiyr wadh-Dhikr, uk. 82)

Maalik amesema:

”Mimi nachukia visa msikitini.”

Maalik amesema tena:

”Sioni kuwa inafaa mtu kukaa kwa wapiga visa. Visa ni Bid´ah.”

Saalim amesema:

”Ibn ´Umar alikuwa nje ya msikiti akasema: ”Hakuna kilichonitoa nje isipokuwa sauti ya mpiga visa wenu huyu.”

Imaam Ahmad amesema:

”Waongo wakubwa ni wapiga visa na waombaji.” Akaulizwa: ”Je, wewe ulikuwa unahudhuria vikao vyao?” Akajibu: ”Hapana.” (al-Bid´a wal-Hawaadith, uk. 109-122, ya at-Tartwushiy)

[4] Miongoni mwa majina ya kumuiga mtu. Ipo Hadiyth Swahiyh inayokemea na kukataza kuigiliza. ´Aaishah (Radhiya Allaahu ´anhaa) amesimulia kuwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

”Mimi sipendi kumuigiliza mtu hata kama nitapata kitu fulani na kitu fulani.” (Ahmad (6/136) na at-Tirmidhiy (2503))

[5] Hadiyth zinazoharamisha kujifananisha na washirikina na makafiri zimehifadhiwa. Miongoni mwazo:

”Wakhalifuni mayahudi na manaswara… ” (Ibn Hibbaan (2186))

”Wakhalifuni washirikina… ” (Muslim (259))

”Wakhalifuni waabudia Moto… ” (Muslim (260))

[6] Kumetoka kitabu kwa jina ”al-Hujaj al-Qawiyyah ´alaa anna Wasaa-il-ad-Da´wah Tawqiyfiyyah” cha Shaykh ´Abdus-Salaam bin Barjas Aal ´Abdil-Kariym. Kinazungumzia maudhui haya kwa uzuri na tunapendekeza kisomwe.

[7] Jengine ni kwamba Malaika hawanakili maneno ya mtu ambaye wanamuigiliza wala hawaigi kutembea kwake na mengineyo ambayo yanafanywa wa waigizaji hii leo. Tazama ”Iyqaaf-un-Nabiyl ´alaa Hukm-it-Tamthiyl” cha Shaykh ´Abdus-Salaam bin Barjas.

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-Ajwibah al-Mufiydah ´an As-ilat-il-Manaahij al-Jadiydah, uk. 105-112
  • Imechapishwa: 26/02/2024
  • taaliki: Shaykh Jamaal bin Furahyaan al-Haarithiy