Waliposhindwa hoja wakakubali kuwa Allaah anazungumza, lakini hata hivyo maneno yake ni kiumbe. Tukasema kuwa wanadamu maneno pia yameumbwa. Kwa hivo mmemfananisha Allaah na viumbe Wake pale mliposema kuwa maneno Yake ni kiumbe. Kwa mujibu wa ´Aqiydah yenu kuna kipindi fulani alikuwa hazungumzi mpaka alipoyaumba maneno. Vivyo hivyo wanadamu walikuwa hawazungumzi mpaka Allaah alipoyaumba maneno yao. Kwa hivyo mmekusanya kati ya kufuru na ushabihishaji – Allaah ametakasika kutokana na sifa hii! Bali tunasema kuwa Allaah daima ni Mwenye kuzungumza, pale anapotaka. Hatusemi kuwa hakuwa Mwenye kuongea mpaka alipoyaumba maneno. Hatusemi kuwa alikuwa si Mwenye kujua mpaka alipoumba elimu, ambapo akajua baada ya hapo. Hatusemi kuwa alikuwa si Mwenye uwezo mpaka alipojiumbia Yeye Mwenyewe uwezo. Hatusemi kuwa alikuwa hana nuru mpaka Alipojiumbia Yeye Mwenyewe nuru. Wala hatusemi kuwa alikuwa anakosa utukufu mpaka alipojiumbia Yeye Mwenyewe utukufu.

Ndipo Jahmiyyah wakasema kuwa wakati tunapomthibitisha Allaah nuru, uwezo na utukufu Wake, basi tunasema yaleyale yaliyosemwa na manaswara waliodai kuwa Allaah na nuru na uwezo Wake ni vya milele. Hatuyasemi hayo, bali tunachosema ni kwamba Allaah ni wa milele na uwezo Wake na nuru Yake, pasi na kumuwekea kikomo cha wakati na kumfanyia namna.

Wakasema kuwa kamwe hatuwezi kuwa wapwekeshaji mpaka tuamini kuwa alikuwepo Allaah pekee na hakukuwepo na kingine. Mambo ni hivyo sisi tunasema kuwa Allaah pekee alikuwepo na hakukuwepo na kingine, lakini si tunamsifu Mungu mmoja pekee tunaposema kuwa Allaah daima alikuwepo na sifa Zake zote? Tukawapa mfano wa hilo. Tuelezeni juu ya mtende; je, si una shina, mzizi, majani, matawi na moyo wa mtende? Bado ni kitu kimoja, licha ya sifa zake zote. Vivyo hivyo Allaah – na Allaah ana wasifu wa juu kabisa – Yeye ni Mungu mmoja na sifa Zake zote. Hatusemi kuwa kuna kipindi fulani alikuwa hana uwezo mpaka alipoumba uwezo Wake. Kwani asiyekuwa na uwezo si muweza. Hatusemi kuwa kuna kipindi fulani alikuwa hajui mpaka alipoumba ujuzi, akajua baada ya hapo. Isitoshe ambaye hajui ni mjinga. Hata hivyo tunachosema ni kwamba Allaah daima alikuwa Mwenye kujua na muweza, pasi na kumuweka kikomo cha wakati wala kumfanyia namna. Allaah amesema kuhusu bwana mmoja kafiri kwa jina al-Waliyd bin al-Mughiyrah al-Makhzuumiy:

ذَرْنِي وَمَنْ خَلَقْتُ وَحِيدًا

”Niache Mimi na yule Niliyemuumba pekee.”[1]

Bwana huyu, ambaye Allaah amemuumba pekee, alikuwa na macho, masikio, ulimi, midomo, mikono, miguu na viungo vyengine vingi. Licha ya hivo Allaah amemwita kuwa ni pekee. Vivyo hivyo Allaah – na ana wasifu wa juu – Yeye ni Mungu mmoja pamoja na sifa Zake zote[2].

[1] 74:11

[2] Ibn ´Aqiyl al-Hanbaliy amesema:

”Imaam Ahmad (Rahimahu Allaah) ameandika kitabu kinachoitwa ”ar-Radd ´alaal-Jahmiyyah waz-Zanaadiqah wal-Qadariyyah.” (al-Aadaab ash-Shar´iyyah (1/274))

Ibn Taymiyyah amesema:

”Kama alivosema Imaam Ahmad katika kitabu chake ”ar-Radd ´alaaz-Zanaadiqah wal-Jahmiyyah.”  (Tafsiyr Suurat-il-Ikhlaasw, uk. 239)

Ibn Kathiyr amesema:

”… na hivo ndivo alivosema Ahmad bin Hanbal katika kitabu ”ar-Radd ´alaal-Jahmiyyah” (Tafsiyr al-Qur-aan al-´Adhwiym (3/304))

Ibn Hajar al-´Asqalaaniy amesema:

”Amesema waziwazi Ahmad katika kitabu “ar-Radd ´alaal-Jahmiyyah.” (Fath-ul-Baariy (13/598))

  • Mhusika: Imaam Ahmad bin Hanbal (afk. 241)
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: ar-Radd ´alaal-Jahmiyyah waz-Zanaadiqah, uk. 138-141
  • Imechapishwa: 28/04/2024