39. Kupinga kwa Jahmiyyah uwepo wa Allaah juu ya ´Arshi

Tukawauliza ni kwa nini wanapinga Allaah kuwepo juu ya ´Arshi ilihali Allaah (Ta´ala) anasema:

الرَّحْمَـٰنُ عَلَى الْعَرْشِ اسْتَوَىٰ

”Mwingi wa rehema amelingana juu ya ´Arshi.”[1]

هُوَ الَّذِي خَلَقَ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضَ فِي سِتَّةِ أَيَّامٍ ثُمَّ اسْتَوَى عَلَى الْعَرْشِ

”Yeye Ndiye Aliyeumba mbingu na ardhi katika siku sita, kisha Akalingana juu ya ´Arshi.”[2]

Wakajibu kwa kusema kuwa Yuko chini ya ardhi ya saba kama alivyo juu ya ´Arshi. Yuko juu ya ´Arshi, ndani ya mbingu, juu ya ardhi na kila mahali. Hakuna mahali anakosa. Hawi sehemu moja pasi na nyingine. Aidha wakatumia hoja kwa Aayah ndani ya Qur-aan:

وَهُوَ اللَّهُ فِي السَّمَاوَاتِ وَفِي الْأَرْضِ

“Naye ndiye Allaah katika mbingu na katika ardhi.”[3]

Tukasema kuwa waislamu wanajua maeneo mengi ambayo sio matukuzo inapokuja kwa Mola. Walipouliza ni maneo gani hayo, tukasema miili yao, matumbo yao, matumbo ya nguruwe, vyoo na sehemu zingine chafu ambazo sio matukuzo inapokuja kwa Mola. Isitoshe Allaah ametueleza ya kwamba Yuko juu ya mbingu. Amesema:

أَأَمِنتُم مَّن فِي السَّمَاءِ أَن يَخْسِفَ بِكُمُ الْأَرْضَ

“Je, mnadhani mko katika amani na aliyeko juu mbinguni kwamba hatokudidimizeni ardhini?”[4]

إِلَيْهِ يَصْعَدُ الْكَلِمُ الطَّيِّبُ وَالْعَمَلُ الصَّالِحُ يَرْفَعُهُ

“Kwake pekee linapanda neno zuri na kitendo chema anakiinua juu.”[5]

يَا عِيسَى إِنِّي مُتَوَفِّيكَ وَرَافِعُكَ إِلَيَّ

“Ee ‘Iysaa! Hakika Mimi ni Mwenye kukuchukua na Mwenye kukupandisha Kwangu.”[2]

بَل رَّفَعَهُ اللَّـهُ إِلَيْهِ ۚ وَكَانَ اللَّـهُ عَزِيزًا حَكِيمًا

”Bali Allaah alimnyanyua Kwake. Allaah daima ni Mwenye kushinda, Mwenye hekima.”[6]

وَلَهُ مَن فِي السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ ۚ وَمَنْ عِندَهُ لَا يَسْتَكْبِرُونَ عَنْ عِبَادَتِهِ وَلَا يَسْتَحْسِرُونَ يُسَبِّحُونَ اللَّيْلَ وَالنَّهَارَ لَا يَفْتُرُونَ

“Na ni Vyake pekee vyote vilivyomo katika mbingu na ardhi na wale walio Kwake hawatakabari na ‘ibaadah Yake na wala hawachoki. Wanasabihi usiku na mchana wala hawazembei.”[7]

يَخَافُونَ رَبَّهُم مِّن فَوْقِهِمْ وَيَفْعَلُونَ مَا يُؤْمَرُونَ

“Wanamkhofu Mola wao Aliye juu yao na wanafanya yale wanayoamrishwa.”[8]

مِّنَ اللَّـهِ ذِي الْمَعَارِجِ تَعْرُجُ الْمَلَائِكَةُ وَالرُّوحُ إِلَيْهِ فِي يَوْمٍ كَانَ مِقْدَارُهُ خَمْسِينَ أَلْفَ سَنَةٍ

“… kutoka kwa Allaah Mwenye njia za kupandia. Malaika na Roho wanapanda Kwake katika siku kadiri yake ni miaka khamsini elfu.”[9]

وَهُوَ الْقَاهِرُ فَوْقَ عِبَادِهِ ۚ وَهُوَ الْحَكِيمُ الْخَبِيرُ

“Naye yu juu ya waja Wake, Naye ni Mwenye hekima, Mwenye khabari za ndani kabisa.”[10]

وَهُوَ الْعَلِيُّ الْعَظِيمُ

“Naye yujuu kabisa, Ametukuka.”[11]

Haya ni maelezo ya Allaah. Ametueleza kuwa Yuko juu ya mbingu. Tunaona jinsi kila kitu kilicho duni naye kimesimangwa. Amesema (´Azza wa Jall):

إِنَّ الْمُنَافِقِينَ فِي الدَّرْكِ الْأَسْفَلِ مِنَ النَّارِ

“Hakika wanafiki watakuwa katika tabaka la chini kabisa katika Moto.”[12]

وَقَالَ الَّذِينَ كَفَرُوا رَبَّنَا أَرِنَا اللَّذَيْنِ أَضَلَّانَا مِنَ الْجِنِّ وَالْإِنسِ نَجْعَلْهُمَا تَحْتَ أَقْدَامِنَا لِيَكُونَا مِنَ الْأَسْفَلِينَ

”Watasema wale waliokufuru: ”Mola wetu! Tuonyeshe wale waliotupotoa miongoni mwa majini na watu; ili tuwaweke chini ya miguu yetu ili wawe miongoni mwa wa walio chini kabisa!”[13]

Nyinyi simnajua kuwa Ibliys na mashaytwaan walikuwa sehemu zao? Allaah hawezi kuwa sehemu hiyohiyo aliyokuweko Ibliys. Aayah isemayo:

وَهُوَ اللَّهُ فِي السَّمَاوَاتِ وَفِي الْأَرْضِ

“Naye ndiye Allaah katika mbingu na katika ardhi.”

maana yake ni kwamba Yeye ndiye mwenye kuabudiwa mbinguni na ardhini. Sambamba na hilo Yuko juu ya ´Arshi na ujuzi Wake umekizunguka kila kitu kilicho chini ya ´Arshi. Hakuna maeneo ambapo unakosekana ujuzi Wake. Ujuzi wa Allaah hauwi sehemu moja pasi na kwengine. Hiyo ndio tafsiri ya maneno Yake (Ta´ala):

لِتَعْلَمُوا أَنَّ اللَّـهَ عَلَىٰ كُلِّ شَيْءٍ قَدِيرٌ وَأَنَّ اللَّـهَ قَدْ أَحَاطَ بِكُلِّ شَيْءٍ عِلْمًا

”… ili mjue kwamba Allaah juu ya jambo ni Muweza na kwamba Allaah amekizunguka kila kitu kwa Ujuzi.”[14]

Miongoni mwa mafunzo katika hayo ni kwamba endapo mtu atashika mkononi mwake chupa ilio wazi, ilio na kinywaji kilicho wazi,  basi macho ya mtu huyo yatalizunguka chupa hilo bila ya macho yake kuwa ndani yake. Allaah ana wasifu wa juu zaidi –  Allaah amewazunguka viumbe Wake wote bila ya Yeye kuwa ndani ya chochote katika viumbe Wake.

Mfano mwingine ni kwamba endapo mtu atajenga nyumba kamili kisha baadaye akafunga mlango na akatoka nje ya nyumba. Mtu huyo anajua ni vyumba vingapi viko katika nyumba hiyo na  vyumba vyote vina ukubwa kiasi gani bila ya yeye kuhitaji kuwa ndani ya nyumba hiyo. Allaah ana wasifu wa juu kabisa – amewazunguka viumbe Wake wote, anajua namna walivyo na wako vipi bila ya Yeye kuwa ndani ya chochote katika vilivyoumbwa[15].

[1] 20:5

[2] 57:4

[3] 6:3

[4] 67:16

[5] 35:10

[6] 4:158

[7] 21:19-20

[8] 16:50

[9] 70:3-4

[10] 6:18

[11] 2:255

[12] 4:145

[13] 41:29

[14] 65:12

[15] Ibn ´Aqiyl al-Hanbaliy amesema:

”Imaam Ahmad (Rahimahu Allaah) ameandika kitabu kinachoitwa ”ar-Radd ´alaal-Jahmiyyah waz-Zanaadiqah wal-Qadariyyah.” (al-Aadaab ash-Shar´iyyah (1/274))

Ibn Taymiyyah amesema:

”Kama alivosema Imaam Ahmad katika kitabu chake ”ar-Radd ´alaaz-Zanaadiqah wal-Jahmiyyah.”  (Tafsiyr Suurat-il-Ikhlaasw, uk. 239)

Ibn Kathiyr amesema:

”… na hivo ndivo alivosema Ahmad bin Hanbal katika kitabu ”ar-Radd ´alaal-Jahmiyyah” (Tafsiyr al-Qur-aan al-´Adhwiym (3/304))

Ibn Hajar al-´Asqalaaniy amesema:

”Amesema waziwazi Ahmad katika kitabu “ar-Radd ´alaal-Jahmiyyah.” (Fath-ul-Baariy (13/598))

  • Mhusika: Imaam Ahmad bin Hanbal (afk. 241)
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: ar-Radd ´alaal-Jahmiyyah waz-Zanaadiqah, uk. 142-150
  • Imechapishwa: 28/04/2024