207 – Muhammad ametuhadithia: Yahyaa bin Bustwaam amenihadithia: Muhammad bin ´Abdillaah bin Sumay´ al-Azdiy ametuhadithia:

”Kuna kiongozi mmoja alimwalika Shumayt al-´Ansiy kwenye chakula, ambapo akaomba udhuru na wala hakuja. Alipoulizwa sababu ya hilo, akasema: ”Kwangu mimi ni bora kukosa chakula kuliko kuitoa kafara dini yangu kwao. Tumbo la muumini halitakiwi kuwa kitu chenye utukufu zaidi kuliko dini yake.”

208 – Daawuud bin ´Amr ametuhadithia, kutoka kwa Hafsw bin Ghiyaath, kutoka kwa Hishaam bin ´Urwah, ambaye ameeleza:

”Hakiym bin Hizaam alisema kuwaambia familia yake: ”Nimiminieni maji.” Wakasema: ”Umeshakunywa leo mara moja.” Ndipo akasema: ”Basi hapana.”

209 – Abu Khaythamah ametuhadithia: Muhammad bin Yaziyd bin Khunays ametuhadithia, kutoka kwa Wuhayb bin Ward, ambaye amesema:

”Mwanachuoni mmoja alikutana na mwanachuoni mwingine akasema: ”Allaah akurehemu! Nieleze kuhusu chakula kisichokuwa israfu.” Akasema: ”Kinachoondosha njaa bila kushiba.”

210 – Surayj bin Yuunus amenihadithia: Hushaym ametuhadithia, kutoka kwa Mansuur, kutoka kwa al-Hasan, ambaye amesema:

”Luqmaan alisema kumwambia mwanawe: ”Usile wakati umeshiba. Yatupe mabaki yako kumpa mbwa.”

211 – Ibraahiym bin Sa´iyd al-Jawhariy amenihadithia: Abul-Yamaan ametuhadithia, kutoka kwa Ismaa´iyl bin ´Ayyaash, kutoka kwa Muhammad bin Twalhah, kutoka kwa ´Uthmaan bin Yahyaa, kutoka kwa Ibn ´Abbaas, ambaye amesema:

”Mara ya kwanza kusikia kunazungumziwa Faaluudhah[1] ilikuwa pale ambapo Jibriyl alikuja kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akasema: ”Ummah wako watafunguliwa ardhi. Dunia itafurika kwao kiasi ambacho watakula Faaluudhah.” Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akasema: ”Ni nini Faaluudhah?” Akasema: ”Watachanganya siagi na asali.” Ndipo Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akashusha pumzi ndefu.”[2]

212 – ´Amr bin Muhammad ametuhadithia: ´Affaan ametuhadithia, kutoka kwa Yaziyd bin Ibraahiym, kutoka kwa Yuusuf, mpwa wa Ibn Siyriyn, ambaye ameeleza kuwa Abu Qilaabah amesema kuhusu maneno Yake (Ta´ala):

ثُمَّ لَتُسْأَلُنَّ يَوْمَئِذٍ عَنِ النَّعِيمِ

”Kisha bila shaka mtaulizwa Siku hiyo kuhusu neema!”[3]

”Bi maana watu kutoka katika ummah wangu ambao wanachanganya siagi na asali na wakala kwa mkate safi.”

213 – Muhammad bin al-Husayn amesema: as-Swalt bin Hakiym amenihadithia: ´Abu ´Aaswim al-´Abbaadaaniy amenihadithia:

”Siku moja ´Abdul-Waahid bin Zayd alinambia: ”Allaah hahitaji waja wajiadhibu kwa njaa na kiu. Lakini muumini ndiye mwenye kuhitaji hayo, ili apate kumuona Bwana wake hali ya kuwa na kiu na amechoka, mwenye njaa, amevunjika moyo na amechoka kwa ajili Yake. Huenda Akamtazama kwa huruma na akamlipa malipo makubwa kutokana na njaa na kiu chake.” Halafu akasema: ”Unajua ni yepi malipo makubwa? Ni kuachwa huru kutokana na Moto.”

[1] Tamtam iliyotengenezwa kwa maziwa, maji na asali.

[2] Ibn Maajah (3340). Batili na isiyokuwa na msingi kwa mujibu wa Ibn-ul-Jawziy katika “al-Mawdhwu´aat” (3/21-22), isiyokuwa na msingi kwa mujibu wa ash-Shawkaaniy katika “al-Fawaa’id al-Majmuu´ah”, uk. 179, na iliyotungwa kwa mujibu wa al-Albaaniy katika “Dhwa´iyf Sunan Ibn Maajah” (664).

[3] 102:8

  • Mhusika: Imaam Abu Bakr ´Abdullaah bin Muhammad bin Abiyd-Dunyaa
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Kitaab-ul-Juu´, uk. 132-135
  • Imechapishwa: 30/07/2023