Unapoingia mwezi wa Ramadhaan basi unawajibika kwa kila muislamu mwanaume na mwanamke mmojammoja, wenye afya njema na wakazi. Yule ambaye atakuwa mgonjwa au msafiri katikati ya mwezi wa Ramadhaan basi ataacha kufunga na atalipa idadi ya zile siku alizokula katika masiku mengine. Allaah (Ta´ala) amesema:

 فَمَن شَهِدَ مِنكُمُ الشَّهْرَ فَلْيَصُمْهُ ۖ وَمَن كَانَ مَرِيضًا أَوْ عَلَىٰ سَفَرٍ فَعِدَّةٌ مِّنْ أَيَّامٍ أُخَرَ

“Basi atakayeshuhudia miongoni mwenu mwezi mpya na afunge . Atakayekuwa mgonjwa au safarini basi atimize idadi katika siku nyinginezo.”[1]

Kama ambavyo yule atayefikiwa na mwezi na ni mtumzima asiyeweza kufunga, ni mgonjwa ana ugonjwa usiyotarajiwa kupona au maradhi yenye kuendelea maradhi yasiyotarajiwa kumuondokea katika wakati wowote – sawa ni mwanaume au mwanamke – basi atakula na kulisha kwa kila siku moja kumpa masikini nusu pishi kutoka katika chakula kinacholiwa sana katika mji. Allaah (Ta´ala) amesema:

وَعَلَى الَّذِينَ يُطِيقُونَهُ فِدْيَةٌ طَعَامُ مِسْكِينٍ

”Na kwa wale wanaoiweza lakini kwa mashaka na kutaabika watoe fidia; kulisha masikini.”[2]

´Abdullaah bin ´Abbaas (Radhiya Allaahu ´anhumaa) amesema:

“[Aayah] hiyo ni kwa mtumzima ambaye hatarajiwi kupona kwake.”

Ameipokea al-Bukhaariy.

Mgonjwa ambaye maradhi yake hayatarajiwi kupona ana hukumu moja kama ya mtumzima na wala haiwalazimu kulipa kwa kutokuwa na uwezo wa kufanya hivo. Maana ya “wanaoiweza” kujikalifisha.

[1] 02:185

[2] 02:184

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Tanbiyhaat, uk. 86
  • Imechapishwa: 07/11/2019