Mwanamke ana nyudhuru maalum zinazomruhusu kuacha kufunga Ramadhaan na kuja kulipa baadaye yale aliyokula kwa sababu ya nyudhuru hizo. Nyudhuru hizo ni:

1 – Hedhi na damu ya uzazi. Ni haramu kwa mwanamke kufunga wakati wa viwili hivyo na ni lazima kwake kulipa katika masiku mengine. al-Bukhaariy na Muslim wamepokea katika “as-Swahiyh” zao kupitia kwa ´Aaishah (Radhiya Allaahu ´anhaa) aliyesema:

“Tulikuwa tukiamrishwa kulipa swawm na hatuamrishwi kulipa swalah.”

Alisema hivo wakati alipoulizwa na mwamamke: “Vipi kuhusu mwanamke mwenye hedhi analipa swawm na halipi swalah?” Ndipo akabainisha (Radhiya Allaahu ´anhaa) ya kwamba jambo hilo ni miongoni mwa mambo yenye kukomeka ambayo kunafuatwa dalili.

Hekima ya hilo: Shaykh-ul-Islaam Ibn Taymiyyah (Rahimahu Allaah) amesema katika “Majmuu´-ul-Fataawaa”:

“Damu zinazomtoka mwenye hedhi ndani yake anatokwa na damu ya hedhi. Mwenye hedhi anaweza kufunga wakati mwingine usiokuwa wa damu katika hali ambayo haitoki damu yake. Ikawa swawm yake katika hali hiyo ni swawm inayolingana sawa na hali yake ambapo hatokwi na damu inayoupa nguvu mwili ambayo ndio maumbile yake. Kufunga katika wakati wa hedhi yake inawajibisha kutoka damu yake ambayo ndio damu yake ya maumbile yake na hivyo itapelekea upungufu wa mwili wake na kuudhoofisha na swawm yake kutoka nje ya usawa. Ndipo akaamrishwa kufunga katika wakati usiokuwa wa hedhi.”[1]

2 – Mjamzito na mwenye kunyonyesha ambaye wanapatwa na madhara kwa mwanamke, mtoto au kwa wote wawili. Watakula katika hali ya ujauzito na unyonyesha. Ikiwa madhara yaliyowafanya kula ni kwa sababu ya mtoto na si nyingine, basi watalipa zile siku walizokula na watalisha masikini kwa kila siku moja iliyowapita. Na ikiwa madhara waliyochelea ni juu ya nafsi zao, basi itatosha kulipa. Hayo ni kwa sababu mjamzito na mnyonyeshaji wanaingia ndani ya maneno Yake (Ta´ala):

وَعَلَى الَّذِينَ يُطِيقُونَهُ فِدْيَةٌ طَعَامُ مِسْكِينٍ

”Na kwa wale wanaoiweza lakini kwa mashaka na kutaabika watoe fidia; kulisha masikini.”

Haafidhw Ibn Kathiyr (Rahimahu Allaah) amesema katika “Tafsiyr” yake:

“Yanayoingia katika maana hii ni mjamzito na mnyonyeshaji watapochelea juu ya nafsi zao wenyewe au juu ya watoto wao.”[2]

Shaykh-ul-Islaam Ibn Taymiyyah (Rahimahu Allaah) amesema katika “Majmuu´-ul-Fataawaa”:

“Ikiwa mjamzito amechelea juu ya mtoto wake, basi atakula na atalipa kwa kila siku moja kumlisha masikini ratili ya mkate.”[3]

[1] (25/251).

[2] (01/379).

[3] (25/318).

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Tanbiyhaat, uk. 86-88
  • Imechapishwa: 07/11/2019