Inajuzu kwa msafiri kuswali swalah zote za Sunnah akiwa juu ya kipando chake hata kama si upande wa Qiblah. Hii imethibitishwa katika Sunnah kutoka kwa kundi la Maswahabah. Miongoni mwao Hadiyth ya ´Aamir bin Rabiy´ah (Radhiya Allaahu ´anh) ambaye ameeleza:

“Nilimwona Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akiwa juu ya mnyama wake akiswali ambapo anaashiria kwa kichwa chake kuelekea upande wowote unapoelekea, lakini Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) hakuwa akifanya hivyo katika swalah za faradhi.”

Ameipokea al-Bukhaariy (1097) na Muslim (701).

Ikiwa msafiri atataka kuswali swalah ya Sunnah juu ya mnyama wake, basi anaanza kwa kumwelekeza Qiblah wakati wa kuanza kisha anaendelea kuelekea popote mnyama wake atampeleka. Kama ilivyo katika Hadiyth ya Anas bin Maalik (Radhiya Allaahu ´anh) kwa Abu Daawuud (1225):

“Hakika Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikuwa anaposafiri na akataka kuswali swalah ya kujitolea, basi alikuwa akielekeza ngamia wake Qiblah kisha anaanza kwa Takbiyr, kisha anaswali akiwa ameelekea upande atakao.”

Haafidhw Ibn Hajar amesema katika ”Buluugh-al-Maraam”: ”Cheni yake ya wapokezi ni nzuri.”

Shaykh wetu ´Abdul-´Aziyz bin Baaz (Rahimahu Allaah) amesema katika maelezo yake ya chini (1/176):

“Mambo ni kama alivosema mtunzi. Wanaume wake ni Swahiyh na hawana neno. Hivyo Hadiyth hii ni ya kuainisha kutokana na Hadiyth nyingine zilizoachiwa ambazo zinaonyesha Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikuwa akiswali kuelekea alikokuwa akielekea wakati wa safari.”

  • Muhusika: ´Allaamah ´Abdul-Muhsin bin Hamad al-´Abbaad
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Shuruwt-is-Swalaah, uk. 41-42
  • Imechapishwa: 01/06/2026