34. Maelezo kuhusu du´a ya kufungulia swalah

Maana ya:

سُبْحَانَكَ اللَّهُمَّ

“Kutakasika ni Kwako, ee Allaah… ”

ni kwamba ninakutakasa kutokamana na kasoro zote kwa namna inayolingana na Utukufu Wako. Kwa msemo mwingine ni kwamba nakutakasa, ee Allaah, utakasifu unaolingana na utukufu Wako.

Maana ya:

وَبِحَمْدِكَ

“… na himdi zote ni Zako.”

ni kuwa Unahimidiwa. Kwa msemo mwingine ni kwamba nakuhimidi na nakusanya kati ya kukutakasa na kukuhimidi. Nakusifu na nakuhimidi kutokana na yale majina mazuri mno na sifa kuu mno na kwa yale Uliyowaneemesha waja Wako. Kwa hivyo maana ya:

سُبْحَانَكَ اللَّهُمَّ وَبِحَمْدِكَ

“Kutakasika ni Kwako, ee Allaah, kutokamana na kasoro zote na himdi zote ni Zako.”

ni kwamba nakukusanyia kati ya kukusabihi na kukuhimidi.

Maana ya:

وتَبَارَكَ اسْمُكَ

“Limetukuka jina Lako… “

ni kuwa baraka hufikiwa kwa kutajwa Kwako. Baraka zinafikiwa kwa kutajwa Kwako, ee Allaah.

Neno (تَبَارَكَ) hii ni sifa ya Allaah. Amesema (Ta´ala):

تَبَارَكَ الَّذِي إِن شَاءَ جَعَلَ لَكَ خَيْرًا مِّن ذَٰلِكَ

“Amebarikika Ambaye akitaka atakujaalia kheri kuliko hayo.”[1]

تَبَارَكَ الَّذِي جَعَلَ فِي السَّمَاءِ بُرُوجًا

“Amebarikika Ambaye amejaalia nyota katika mbingu.”[2]

تَبَارَكَ الَّذِي بِيَدِهِ الْمُلْكُ

”Amebarikika Ambaye mkononi Mwake umo ufalme.”[3]

Neno (فتبارك) hutumiwa juu ya haki ya Mola na halitumiwi kwa viumbe. Baadhi ya watu wanapotembelewa na watu wanasema:

“ Umetubariki.”

Hili ni kosa. Kwa sababu hii ni miongoni mwa sifa za Allaah. Unachotakiwa kusema ni:

“Nimepata baraka kwa kututembelea.”

au pia unaweza kusema:

“Wewe ni mtu uliyebarikiwa.”

endapo atakuwa ni mwema. Vilevile unaweza kusema:

“Haya ni katika baraka zako.”

Ukikusudia ni katika baraka ambazo Allaah ameweka kwako.

Allaah ndiye Mwenye kubariki na mja Wake akawa mwenye kubarikiwa. Amesema (Ta´ala) juu ya ´Iysaa (´alayhis-Salaam):

وَجَعَلَنِي مُبَارَكًا أَيْنَ مَا كُنتُ

“Amenijaalia kuwa mwenye ni kubarikiwa popote nitakapokuweko.”[4]

al-Bukhaariy na Muslim wamepokea kupitia kwa ´Aaishah, mkewe Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ambaye ameeleza:

“Tulitoka pamoja na Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) katika baadhi ya safari zake mpaka tulipofika al-Baydaa´ au Dhat-il-Jaysh kilikatika kidani changu. Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akabaki kwa ajili ya kukitafuta na watu wakabaki pamoja naye hali ya kuwa hawako katika eneo lenye maji na wala hawana maji. Watu wakamwendea Abu Bakr as-Swiddiyq na kusema: “Je, huoni alichofanya ´Aaishah ambaye amebaki na Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na watu ilihali hawako eneo lenye maji na wala hawana maji?” Abu Bakr akaja na akamkuta Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ameweka kichwa chake juu ya paja langu ambapo amelala ambapo akasema: “Umemzuia Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na watu ilihali hawako katika eneo lenye maji na wala hawana maji. ´Aaishah amesema: “Abu Bakr akanilaumu na akazungumza kile alichotaka Allaah yeye kukizungumza na akawa ananitomasatomasa kwa mkono wake kiunoni kwangu. Hakuna kilichokuwa kinanizuia kuondoka isipokuwa ni kutokana maeneo pa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) paja langu. Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akanyanyuka wakati kulipopambazuka akiwa hana maji. Ndipo Allaah akateremsha Aayah ya Tayammum. Usayd bin al-Khudhwayr akasema: “Hii si baraka ya mwanzo kwenu nyinyi kizazi cha Abu Bakr.” ´Aaishah amesema: “Tukamsaka yule ngamia ambaye mimi nilikuwa juu yake na tahamaki kile kidani kilikuwa chini yake.”[5]

Maana ya:

وَتَعَالى جَدُّكَ

”… ufalme Wako ni mkubwa.”

ni kuwa Utukufu Wako ni Mkubwa. Husemwa neno (الجدُّ) kwa kuachia na kukakusudiwa maana nyingi; linapotajwa kwa kuachia hukusudiwa babu na wakati mwingine hukusudiwa utukufu kama ilivyo katika Hadiyth hii. Pia inaweza kuwa na maana ya cheo na nafasi. Miongoni mwazo ni ile Dhikr baada ya kumaliza kuswali:

اللّهُـمَّ لا مانِعَ لِما أَعْطَـيْت، وَلا مُعْطِـيَ لِما مَنَـعْت، وَلا يَنْفَـعُ ذا الجَـدِّ مِنْـكَ الجَـد

“Ee Allaah! Hakuna awezaye kuzuia ulichokitoa na wala kutoa ulichokizuia na wala cheo cha mtu hakimnufaishi mwenye cheo mbele Yako.”[6]

Makusudio ya (الجدُّ) ni cheo na nafasi; kama mfano wa utukufu, nafasi na mali. Maana yake ni kwamba ambaye yuko na cheo hakimnufaishi cheo chake mbele Yake. Kinachomnufaisha na kumfanya aokoke ni matendo mema.

Maana ya:

وَلا إِله غَيْرُكَ

“Hapana mungu mwengine asiyekuwa Wewe.”

ni kwamba hakuna mwabudiwa wa haki katika ardhi wala mbinguni isipokuwa ni Wewe, Allaah. Jua, mwezi, nyota, Malaika, Mitume na waja wema wameabudiwa. Lakini kuabudiwa kwavyo ni batili. Si venginevyo kuabudiwa kwa haki kunakuwa kwa Allaah. Yule mwenye kumwabudu asiyekuwa Allaah ´ibaadah yake ni batili. Haijalishi kitu hata kama atakuwa Mtume. Kwa sababu Allaah ana haki Yake na Mtume ana haki yake. Haki ya Allaah ni kuabudiwa. Haki ya Mtume ni kumwamini, kumfata, kusadikisha maelezo yake na kutekeleza hukumu zake.

Kidokezo

Baadhi ya watu huongeza baada ya du´aa ya kufungulia swalah wakasema:

و لا معبود سواك

“… na wala hakuna mwabudiwa mwengine asiyekuwa Wewe.”

Ziada hii haikuwekwa katika Shari´ah. Bali wameitoa vichwani mwao. Sio sehemu katika du´aa ya kufungulia swalah.

[1] 25:10

[2] 25:61

[3] 67:01

[4] 19:31

[5] al-Bukhaariy (744) na Muslim (598) na tamko ni lake.

[6] al-Bukhaariy (844) na Muslim (593).

  • Mhusika: ´Allaamah ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah ar-Raajihiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Shuruwt-is-Swalaah, uk. 58-60
  • Imechapishwa: 09/06/2022