34. Walichoamrishwa watu na majini na kuumbwa kwacho

Shaykh-ul-Islaam Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab (Rahimahu Allaah) amesema:

Hilo ndilo Allaah Amewaamrisha watu wote na Amewaumba kwa lengo hilo. Allaah (Ta´ala) Amesema:

وَمَا خَلَقْتُ الْجِنَّ وَالْإِنسَ إِلَّا لِيَعْبُدُونِ

“Sikuumba majini na watu isipokuwa waniabudu.”[1]

MAELEZO

Hilo ndilo Allaah… – Ishara inarudi katika maneno yake:

“Kumwabudu Allaah pekee hali ya kumtakasia Yeye dini.”

Allaah amewaamrisha viumbe wote kumwabudu Allaah hali ya kumtakasia Yeye dini. Allaah amewaamrisha watu wote – mwarabu kwa asiyekuwa mwarabu, mweupe kwa mweusi – watu wote kuanzia kipindi cha Aadam mpaka mtu wa mwisho duniani wameamrishwa kumwabudu Yeye pamoja na kumtakasia nia katika ´ibaadah. Allaah (Ta´ala) amesema:

يَا أَيُّهَا النَّاسُ اعْبُدُوا رَبَّكُمُ الَّذِي خَلَقَكُمْ وَالَّذِينَ مِن قَبْلِكُمْ لَعَلَّكُمْ تَتَّقُونَ الَّذِي جَعَلَ لَكُمُ الْأَرْضَ فِرَاشًا وَالسَّمَاءَ بِنَاءً وَأَنزَلَ مِنَ السَّمَاءِ مَاءً فَأَخْرَجَ بِهِ مِنَ الثَّمَرَاتِ رِزْقًا لَّكُمْ ۖ فَلَا تَجْعَلُوا لِلَّـهِ أَندَادًا وَأَنتُمْ تَعْلَمُونَ

“Enyi watu! Mwabuduni Mola wenu ambaye amekuumbeni na wale wa kabla yenu mpate kumcha. Ambaye amewafanyieni ardhi kuwa ni tandiko na mbingu kuwa ni paa na akateremsha kutoka mbinguni maji, akawatolea kwayo matunda kuwa ni riziki zenu. Hivyo basi, msimfanyie Allaah waliolingana naye na hali ya kuwa nyinyi mnajua.”[2]

Kwamba hana mwenza, hana mshirika wala anayelingana Naye. Haya ni makatazo ya ushirikina mkubwa na ushirikina mdogo. Allaah amewaamrisha hilo watu wote kuanzia wa mwanzo wao mpaka wa mwisho wao.

Amewaumba kwa lengo hilo – Bi maana kumwabudu Yeye hali ya kuwa pekee yake hana mshirika. Wameumbwa kwa ajili hiyo. Hayo ni kama ilivyo katika maneno Yake (Ta´ala):

وَمَا خَلَقْتُ الْجِنَّ وَالْإِنسَ إِلَّا لِيَعْبُدُونِ

“Sikuumba majini na watu isipokuwa waniabudu.”

Pia wameamrishwa hilo katika maneno Yake (Ta´ala):

يَا أَيُّهَا النَّاسُ اعْبُدُوا رَبَّكُمُ الَّذِي خَلَقَكُمْ

“Enyi watu! Mwabuduni Mola wenu ambaye amekuumbeni… “[3]

Hii ndio maana ya maneno ya Shaykh:

“Wameumbwa kwa lengo hilo na wakaamrishwa nalo.”

Amekusanya amri mbili hizo kwa kusema:

“Hilo ndilo Allaah amewaamrisha watu wote na amewaumba kwa lengo hilo.”

Amesema (Ta´ala):

وَمَا خَلَقْتُ الْجِنَّ وَالْإِنسَ إِلَّا لِيَعْبُدُونِ

“Sikuumba majini na watu isipokuwa waniabudu.”

Maneno Yake:

وَمَا خَلَقْتُ الْجِنَّ وَالْإِنسَ

“Sikuumba majini na watu… “

Allaah ndiye Muumbaji. Yeye ndiye kawaumba viumbe wote wakiwemo majini na watu, akawapa akili na akawafaradhishia kumwabudu Yeye mmoja wa pekee hali ya kuwa hana mshirika. Amewakhusisha kwa amri ya kumwabudu. Kwa sababu Allaah amewapa akili na akawapa kile wanachoweza kupambua kwacho kati ya chenye kudhuru na chenye kunufaisha, haki na batili. Ameviumba vitu vyote kwa ajili ya maslahi na manufaa yao. Amesema (Ta´ala):

وَسَخَّرَ لَكُم مَّا فِي السَّمَاوَاتِ وَمَا فِي الْأَرْضِ جَمِيعًا مِّنْهُ

”Amekutiishieni vilivyomo mbinguni na vilivyomo ardhini vyote humo.”[4]

Yote yamewepesishwa kwa wanaadamu ili waweze kuyatumia kwa kile walichoumbiwa kwa ajili yake; nacho ni kumwabudu Allaah (Subhanaahu wa Ta´ala):

وَمَا خَلَقْتُ الْجِنَّ وَالْإِنسَ إِلَّا لِيَعْبُدُونِ

“Sikuumba majini na watu isipokuwa waniabudu.”

Majini ni walimwengu wasioonekana. Sisi hatuwaoni. Wao pia wamekalifishwa ´ibaadah. Wamekatazwa shirki na maasi kama ilivyo kwa wanaadamu. Lakini wanatofautiana na wanaadamu inapokuja katika maumbile. Inapokuja katika maamrisho na makatazo wao ni kama wanaadamu ambapo wameamrishwa na wamekatazwa. Majini ni walimwengu wasioonekana. Lakini wapo.

Watu ndio wanaadamu. Wameitwa watu (الإنس) kwa sababu baadhi yao wanaanasika kwa wengine, wanakusanyika na wanaungana.

Majini wameitwa hivo kutokana na kujificha (الاجتنان). Kunaingia pia kipomoko (الجنين) tumboni kwa sababu kimejificha. Majini wamejificha nasi hatuwaoni. Hata hivyo ni walimwengu waliopo. Ambaye atawakanusha ni kafiri. Kwa sababu ni mwenye kumkadhibisha Allaah, Mtume Wake na maafikiano ya waislamu. Allaah (´Azza wa Jall) amebainisha kwamba hawakuumba majini na watu kwa jambo jengine isipokuwa wamwabudu Yeye. Hakuwaumba ili wamdhuru au wamnufaishe, ajitukuze kutokamana na udhalili au awe na vingi kutokana na uchache. Kwani Yeye ni mkwasi kutokamana na walimwengu. Wala hakuwaumba kwa sababu anawahitajia. Hakuwaumba ili wamruzuku au wamchumie mali:

مَا أُرِيدُ مِنْهُم مِّن رِّزْقٍ وَمَا أُرِيدُ أَن يُطْعِمُونِ إِنَّ اللَّـهَ هُوَ الرَّزَّاقُ ذُو الْقُوَّةِ الْمَتِينُ

“Sitaki kutoka kwao riziki yoyote, na wala Sitaki wanilishe. Hakika Allaah Ndiye Mwingi wa kuruzuku, Mwenye nguvu Madhubuti.”[5]

Allaah hana haja ya viumbe. Watu na majini wameumbwa kwa lengo moja pekee; wamwabudu.

Isitoshe Yeye hana haja ya ´ibaadah zao. Wao ndio wenye kuzihitajia. Kwa sababu wakimwabudu Allaah atawakirimu na kuwaingiza Peponi. Manufaa ya ´ibaadah yanarudi kwao na madhara ya maasi yanarudi kwao. Ama Allaah (Jalla wa ´Alaa) hadhuriki kwa utiifu wa mwenye kutii wala maasi ya mwenye kuasi. Amesema (Subhaanahu wa Ta´ala):

إِن تَكْفُرُوا أَنتُمْ وَمَن فِي الْأَرْضِ جَمِيعًا فَإِنَّ اللَّـهَ لَغَنِيٌّ حَمِيدٌ

“Mkikufuru nyinyi na wote walioko ardhini, basi hakika Allaah ni mkwasi, Mwenye kustahiki kuhimidiwa.”[6]

Allaah hadhuriki na maasi ya mwenye kuasi na wala hadhuriki kwa utiifu wa mwenye kutii. Mambo haya yanarudi kwa viumbe wenyewe. Wakimtii watanufaika na wakimwasi watadhurika kwa maasi yao.

[1] 51:56

[2] 02:21-22

[3] 02:21

[4] 45:13

[5] 51:57

[6] 14:08

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Thalaathat-il-Usuwl, uk. 75-78
  • Imechapishwa: 09/12/2020