Kitu kingine kinachotilia mkazo uwajibu wa ujumuishaji huo ni kwamba Ibn ´Abbaas na Ibn Mas´uud (Radhiya Allaahu ´anhumaa) wamesema kuhusu Aayah:

وَالْقَوَاعِدُ مِنَ النِّسَاءِ اللَّاتِي لَا يَرْجُونَ نِكَاحًا فَلَيْسَ عَلَيْهِنَّ جُنَاحٌ أَن يَضَعْنَ ثِيَابَهُنَّ

“Na wale wanawake wazee waliokatika hedhi ambao hawataraji kuolewa, basi hapana neno juu yao kupunguza baadhi ya nguo zao.”[1]

”Bi maana jilbaab zao.”[2]

Hii ni dalili ya wazi kwamba wanawake wote wanapaswa kuvaa jilbaab juu ya shungi isipokuwa tu wale wanawake wazee ambao hawatamaniki kutokana na utuuzima wao. Je, si imefika wakati kwa wanawake wote wema wazindukane, wamche Allaah na waweke jilbaab juu ya shungi zao?

Kutokana na ninavyojua ni kuwa hakuna yeyote katika wale wote walioandika kuhusu mada hii aliyebainisha hukumu hii iliyotajwa waziwazi ndani ya Qur-aan na Sunnah, jambo ambalo linashangaza. Baadhi yao wameingia kwa undani kuzungumzia juu ya kwamba uso wa mwanamke ni uchi, licha ya kwamba kuna maoni tofauti juu ya hilo na sahihi ni kwamba uso sio uchi, kama unavyoona kwa upambanuzi ndani ya kitabu hiki.

[1] 24:60

[2] Abu Daawuud kwa cheni ya wapokezi nzuri na kupitia kwake al-Bayhaqiy. Upokezi wa Ibn Mas´uud uko kwa Ibn Jariyr.

  • Mhusika: Imaam Muhammad Naaswir-ud-Diyn al-Albaaniy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Jilbaab-ul-Mar-ah al-Muslimah, uk. 85-86
  • Imechapishwa: 18/09/2023