33. Nguzo ya pili ya swalah: Takbiyr ya kufungulia swalah

Shaykh-ul-Islaam na Imaam Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab (Rahimahu Allaah) amesema:

Nguzo ya pili ni kuleta Takbiyr ya kufungulia swalah. Dalili ni Hadiyth inayosema:

“Uharamu [ufunguzi] wake ni Takbiyr na uhalali [ufungwaji] wake ni Tasliym.”[1]

Baada ya hilo kunakuja du´aa ya kufungulia, ambayo ni Sunnah, kwa kusema:

سُبْحَانَكَ اللَّهُمَّ وَبِحَمْدِكَ وتَبَارَكَ اسْمُكَ وَتَعَالى جَدُّكَ وَلا إِله غَيْرُكَ

“Kutakasika ni Kwako, ee Allaah, kutokamana na kasoro zote na himdi zote ni Zako. Limetukuka jina Lako, ufalme Wako ni mkubwa na hapana mungu wa haki mwengine asiyekuwa Wewe.”[2]

Maana ya:

سُبْحَانَكَ اللَّهُمَّ

“Kutakasika ni Kwako, ee Allaah… ”

ni kwamba ninakutakasa kutokamana na kasoro zote kwa namna inayolingana na Utukufu Wako.

Maana ya:

وَبِحَمْدِكَ

“… na himdi zote ni Zako.”

ni kuwa Unahimidiwa.

Maana ya:

وتَبَارَكَ اسْمُكَ

“Limetukuka jina Lako… “

ni kuwa baraka hufikiwa kwa kutajwa Kwako.

Maana ya:

وَتَعَالى جَدُّكَ

”… ufalme Wako ni mkubwa.”

ni kuwa Utukufu Wako ni Mkubwa.

Maana ya:

وَلا إِله غَيْرُكَ

“Hapana mungu mwengine asiyekuwa Wewe.”

ni kwamba hakuna mwabudiwa wa haki katika ardhi wala mbinguni isipokuwa ni Wewe, Allaah.

MAELEZO

Nguzo ya pili ya swalah katika nguzo za swalah ni Takbiyr ya kuingilia ndani ya swalah.

Nguzo ya Takbiyr ya kufungulia swalah imekuwa ni nguzo ya kipekee miongoni mwa nguzo zengine kwa sababu swalah haifungiki kwa kuiacha. Maneno yake:

Dalili ni Hadiyth inayosema:

“Uharamu [ufunguzi] wake ni Takbiyr na uhalali [ufungwaji] wake ni Tasliym.”

Ni kana kwamba mswaliji kwa Takbiyr hii ya kuingia ndani ya swalah anakuwa amekatazwa kuongea na kutenda mambo ambayo yako nje ya swalah. Takbiyr imeitwa hivo kwa sababu inamzuia mwenye kuswali kutokamana na mambo hayo. Ndio maana ikaitwa kuwa ni “Takbiyrat-ul-Ihraam.” Bi maana maharamisho ya swalah[3].

Uhalali [ufungwaji] wake ni Tasliym – Bi maana kwa kutoa Tasliym yale mambo yaliyokuwa haramu kwa mswaliji kwa kupiga Takbiyr katika maneno na vitendo vilivyo nje ya swalah yanakuwa ni halali kwake. Ni kama ambavyo yanakuwa halali kwa yule mwenye kuhirimia hajj pale anapoyamaliza yale ambayo yalikuwa ni haramu kwake[4].

Kisha baada ya hapo mtunzi (Rahimahu Allaah) akazungumzia du´aa ya kufungulia swalah. Maneno yake:

“Baada ya hilo… “

Bi maana baada ya Takbiyrat-ul-Ihraam. Maneno yake:

“… kunakuja du´aa ya kufungulia, ambayo ni Sunnah.”

Sunnah ni kile ambacho mtu analipwa thawabu kwa kukifanya na haadhibiwi kwa kukiacha[5].  Kusoma du´aa ya kufungulia swalah baada ya Takbiyrat-ul-Ihraam ni jambo limependekezwa. Mtu akiisoma, Allaah anamlipa thawabu, na akiiacha basi swalah yake ni sahihi na wala hapati dhambi. Imeitwa “du´aa ya kufungulia swalah” kwa sababu mtu anafungulia swalah baada ya Takbiyrat-ul-Ihraam. Du´aa ya kufungulia swalah inakuwa katika ile Rak´ah ya kwanza katika kila swalah ya faradhi au swalah iliyopendekezwa.

Du´aa sahihi zaidi iliopokelewa kuhusu kufungua swalah ni ile iliotolewa na al-Bukhaariy na Muslim kupitia kwa Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ´anh) ambaye ameeleza: “Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) baada ya kuleta Takbiyr alikuwa akinyamaza kitambo kidogo kabla ya kuanza kusoma. Nikasema: “Ee Mtume wa Allaah, namtoa fidia baba yangu na mama yangu kwa ajili yako, nimeona kunyamaza kwako baina ya Takbiyr na kisomo, nini unachosema?” Akasema:

اللَّهُمَّ بَاعِدْ بَيْنِي وَبَيْنَ خَطَايَايَ كَمَا بَاعَدْتَ بَيْنَ الْمَشْرِقِ وَالْمَغْرِبِ، اللَّهُمَّ نَقِّنِي مِنْ خَطَايَايَ كَمَا يُنَقَّى الثَّوْبُ الْأَبْيَضُ مِنَ الدَّنَسِ، اللَّهُمَّ اغْسِلْني مِنْ خَطَايَايَ، بِالثَّلْجِ وَالْماءِ وَالْبَرَدِ

“Ee Allaah! Niweke mbali mimi na makosa/dhambi zangu kama ulivyoweka mbali baina ya mashariki na magharibi. Ee Allaah! Nitakase na makosa/dhambi zangu kama Unavyoitakasa nguo nyeupe na uchafu. Ee Allaah! Nisafishe na makosa/dhambi zangu kwa theluji, kwa maji na kwa barafu.”[6]

Miongoni mwazo ni yale aliyonakili mtunzi (Rahimahu Allaah) kwa kusema:

سُبْحَانَكَ اللَّهُمَّ وَبِحَمْدِكَ وتَبَارَكَ اسْمُكَ وَتَعَالى جَدُّكَ وَلا إِله غَيْرُكَ

“Kutakasika ni Kwako, ee Allaah, kutokamana na kasoro zote na himdi zote ni Zako. Limetukuka jina Lako, ufalme Wako ni mkubwa na hapana mungu wa haki mwengine asiyekuwa Wewe.”[7]

Hii ndio du´aa bora ya kufungulia swalah kwa dhati yake; kwa sababu yote inamsifu, inamtakasa na kumhimidi Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala).

Mtunzi wa kitabu (Rahimahu Allaah) ameitaja na kuichagua kwa sababu ni nyepesi kuihifadhi na kutokana na kule kumsifu kwake Allaah. Mtunzi (Rahimahu Allaah) amefasiri sentesi yake.

[1] Abu Daawuud (61), at-Tirmidhiy (3), Ibn Maajah (275) na Ahmad (01/123) kutoka katika Hadiyth ya ´Aliy bin Abiy Twaalib (Radhiya Allaahu ´anh). an-Nawawiy amesema:

”Hadiyth hii ameipokea Abu Daawuud, at-Tirmidhiy na wengineo kwa cheni ya wapokezi Swahiyh. Isipokuwa tu ndani yake yuko ´Abdullaah bin Muhammad bin ´Aqiyl.” (al-Majmuu´ (03/240)).

at-Tirmidhiy amesema:

”Hadiyth hii ndio Swahiyh zaidi juu ya maudhui haya au nzuri. ´Abdullaah bin Muhammad bin ´Aqiyl ni mkweli. Baadhi ya wanachuoni wamemtia walakini kabla ya hifdhi yake. Abu ´Iysaa amesema: ”Ahmad bin Hanbal, Ishaaq bin Raahuuyah na al-Humaydiy walikuwa wakijengea hoja kwa Hadiyth ya ´Abdullaah bin Muhammad bin ´Aqiyl.” Ahmad amesema: ”Hadiyth zake  ni njema.”

[2] Abu Daawuud (775), at-Tirmidhiy (243) na Ibn Maajah (806) kutoka katika Hadiyth ya ´Aiashah (Radhiya Allaahu ´anhaa).

at-Tirmidhiy:

”Hadiyth hii hatuijui kutoka katika Hadiyth ya ´Aaishah isipokuwa kwa wajhi hii. Haarithah ametiwa dosari kabla ya hifdhi yake.”

al-Haakim amesema:

”Hadiyth hii ni yenye cheni ya wapokezi Swahiyh na hakuitoa [al-Bukhaariy].” (al-Mustadrak (01/360)).

an-Nawawiy amesema:

”Ameipokea at-Tirmidhiy, Abu Daawuud na Ibn Maajah kwa cheni ya wapokezi dhaifu. Ameidhoofisha Abu Daawuud, at-Tirmidhiy, al-Bayhaqiy na wengineo. Pia ameipokea Abu Daawuud, at-Tirmidhiy, an-Nasaa´iy, Ibn Maajah na al-Bayhaqiy kupitia kwenye upokezi wa Abu Sa´iyd al-Khudriy na ameidhoofisha.” (al-Adhkaar, uk. 360). Vilevile tazama “al-Majmuu´ (03/265).

[3] an-Nihaayah (01/373) ya Ibn Athiyr.

[4] an-Nihaayah (01/429).

[5] Tazama maelezo ya ”al-Kawkab-ul-Muniyr” (01/402-403) ya al-Futuuhiy.

[6] al-Bukhaariy (744) na Muslim (598) na tamko ni lake.

[7] Abu Daawuud (775), at-Tirmidhiy (243) na Ibn Maajah (806) kutoka katika Hadiyth ya ´Aiashah (Radhiya Allaahu ´anhaa).

at-Tirmidhiy:

”Hadiyth hii hatuijui kutoka katika Hadiyth ya ´Aaishah isipokuwa kwa wajhi hii. Haarithah ametiwa dosari kabla ya hifdhi yake.”

al-Haakim amesema:

”Hadiyth hii ni yenye cheni ya wapokezi Swahiyh na hakuitoa [al-Bukhaariy].” (al-Mustadrak (01/360)).

an-Nawawiy amesema:

”Ameipokea at-Tirmidhiy, Abu Daawuud na Ibn Maajah kwa cheni ya wapokezi dhaifu. Ameidhoofisha Abu Daawuud, at-Tirmidhiy, al-Bayhaqiy na wengineo. Pia ameipokea Abu Daawuud, at-Tirmidhiy, an-Nasaa´iy, Ibn Maajah na al-Bayhaqiy kupitia kwenye upokezi wa Abu Sa´iyd al-Khudriy na ameidhoofisha.” (al-Adhkaar, uk. 360). Vilevile tazama “al-Majmuu´ (03/265).

  • Mhusika: ´Allaamah ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah ar-Raajihiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Shuruwt-is-Swalaah, uk. 55-58
  • Imechapishwa: 14/03/2022