100- Sunnah ni kumwingiza maiti kupitia kule mwishoni mwa kaburi. Hilo ni kutokana na Hadiyth ya Abu Ishaaq ambaye amesema:

“Haarith aliacha anausia aswaliwe na ´Abdullaah bin Yaziyd na akafanya hivo. Kisha akamwingiza kwenye kaburi kupitia upande wa miguu yake ya kaburi. Halafu akasema: “Kufanya hivo ndio Sunnah.”

Ameipokea Ibn Abiy Shaybah katika “al-Muswannaf” (04/130), Abu Daawuud (02/69) kupitia kwa al-Bayhaqiy (04/54) na akasema:

“Cheni ya wapokezi ni Swahiyh. Maneno yake:

“Kufanya hivo ndio Sunnah.”

ina maana kwamba ni yenye kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam).”

Kisha akaipokelea shawahidi kutoka katika Hadiyth ya Ibn ´Abbaas na wengineo na akasema:

“Hiki ndio kilichotangaa kwa watu wa Hijaaz.”

Kisha akataja Hadiyth mbili juu ya kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) aliingizwa ndani kupitia upande wa Qiblah na akazidhoofisha, mambo ni kama alivosema. ash-Shaafi´iy (Rahimahu Allaah) ameitia kasoro Hadiyth ya pili katika hizo mbili kwa upande wa matini yake kwa hoja kwamba ni jambo lisilowezekana kiutendaji. Amesema katika “al-Umm” (01/241):

“Nimepewa khabari na marafiki zangu waaminifu kwamba kaburi la Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) lilikuwa upande wa kulia wa kuingilia nyumbani na limeambatana na ukuta na ukuta ambao kulikuwa kuna mwanandani ilikuwa ni upande wa Qiblah na mwanandani wake ulikuwa chini ya ukuta. Ni vipi basi ataingizwa kwa mapana ilihali ukuta umekamatana na ukuta? Hakusimami juu yake chochote na wala haliyumkiniki isipokuwa kuingizwa katika ule upande wa Qiblah au kuingizwa kinyume na Qiblah. Mambo ya wafu na kuingizwa kwao ni miongoni mwa mambo yanayotambulika kwetu kwa kule vifo kuwa vingi, kuhudhuria maimamu na waaminifu. Isitoshe ni miongoni mwa mambo yaliyoenea ambayo kunatoshelezeka Hadiyth. Hadiyth juu ya mambo hayo zinakuwa ni kama kulazimisha kutokana kule kuenea utambuzi wa watu. Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), Muhaajiruun na Answaar wako kati yetu kwa kule watu wote kunukuu kutoka kwa watu wote. Hawatofautiani katika jambo hilo kwamba maiti anaingizwa kule mwishoni mwa makaburi. Kisha anajitokeza mtu[1] kutoka katika mji usiyokuwa wetu anatufundisha namna ya kumwingiza maiti[2] ilihali hajui (hivi ndivo ilivyokuja katika asili).” Imekuja katika “al-Majmuu´” kuna nukuu kutoka katika “al-Umm”: “Ilihali hajaridhia” na pengine hii ndio ya sawa. Kisha akapokea kutoka kwa Hammaad bin Ibraahiym kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) aliingizwa ndani kwa mapana.”

“Kisha ash-Shaafi´iy akasimulia Hadiyth kupitia kwa Ibn ´Abbaas na wengineo kwamba Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) aliingizwa upande wa kichwa chake.”

Wapokezi wake ni waaminifu ni wapokezi wa al-Bukhaariy na Muslim isipokuwa tu mwalimu wa ash-Shaafi´iy ambaye hamtambuliki kwa sababu hakumtaja. Kwa sababu ash-Shaafi´iy amesema:

“Wametukhabarisha mwaminifu kutoka kwa ´Amr kutoka kwa ´Atwaa kutoka kwake.”

Ibn Siyriyn amesema:

“Nilikuwa pamoja na Anas katika mazishi akaamrisha maiti aingizwe upande wa miguu ya kaburi.”

Ameipokea Ahmad (4081) na Ibn Abiy Shaybah (04/130) na cheni ya wapokezi wake ni Swahiyh.

101- Maiti atalazwa upande wake wa kulia na huku uso wake umeelekezwa upande wa Qiblah. Uso wake na miguu yake itakuwa imeelekea upande wa kulia wa Qiblah na kushotoni mwake. Kutokana na haya ndivo kimepita kitendo cha waislamu kuanzia wakati wa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) mpaka hii leo. Hivi ndivo yanavofanya makaburi yote ulimwenguni. Hivi ndivo imekuja katika “al-Muhallaa” (05/173) na venginevyo.

[1] Ni Hammad bin Sulaymaan ambaye ni miongoni mwa waalimu wa Abu Haniyfah kama ilivyokuja katika ”Fath-ul-Qadiyr” na vyenginevyo. Bali lililo wazi ni kwamba ni Abu Haniyfah mwenyewe kwa dalili ya maneno ya ash-Shaafi´iy ifuatayo: “Mpaka akatusimulia kutoka kwa Hammaad”. Haya yanaonyesha wazi kwamba sio Hammaad na kwamba ni Abu Haniyfah.

[2] Yale yaliyotujulisha Hadiyth hii yenye kutoka kwa Swahabah kisha Hadiyth iliyo kabla yake ambayo ni yenye kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ndio madhehebu ya Ahmad na ndivo wanavoonelea wenzake wengi, kama ilivyokuja katika “al-Inswaaf” (02/544) tofauti na Hanafiyyah kama ilivyotangulia katika maneno ya ash-Shaafi´iy. Ibn Humaam akajengea hoja kwa Hadiyth ya Ibn ´Abbaas ya kwamba (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) aliingia kaburi… akaipokea kutokea upande wa Qiblah… Ameipokea at-Tirmidhiy na akasema: “Hadiyth hiyo ni nzuri.” Ibn Humaam amesema (01/470):

“Pamoja na kwamba ndani yake yumo Hajjaaj bin Arattwah na Minhaal bin Haliyfah ambao wanazuoni wametofautiana juu yao. Akasema: “Hilo linaifuta Hadiyth kutoka katika ngazi ya usahihi lakini sio uzuri (Hasan).”

Bali hilo linaifuta kutoka katika ngazi ya uzuri pia. Kwa sababu Hajjaaj ni mbabaishaji na amesimulia sana kwa kutotaja majina ya wapokezi. Hadiyth iliyopokelewa kwa kutotaja majina ya wapokezi si yenye kukubaliwa kutoka kwa wanazuoni. Hiyo ni moja ya Hadiyth mbili ambazo ameidhoofisha al-Bayhaqiy, hayo yametanguliwa kuashiriwa mwanzoni mwa masuala. Kwa ajili hiyo ndio maana an-Nawawiy (05/295) akampinga at-Tirmidhiy kwa kule kumfanya kwake mzuri na akasema:

“Maneno ya at-Tirmidhiy kwamba ni nzuri hayakubaliwi. Kwani Hadiyth ya Hajjaaj bin Arattwah ni dhaifu kwa makubaliano ya wanazuoni wa Hadiyth.”

az-Zayla´iy (02/300) amesema baada ya kusimulia maneno ya at-Tirmidhiy:

“Kule kumpinga kwake ni kwa sababu Hadiyth hiyo inazungukia kwa Hajjaaj bin Arattwah ambaye ni mbabaishaji na wala hajataja kule kusikia kwake. Isitoshe Minhaal amedhoofishwa na Ibn Ma´iyn… “

Hii ndio haki kwa yule ambaye ni mwadilifu juu ya kwamba Hadiyth hii ni dhaifu na upande mwingine Hadiyth ya ´Abdullaah bin Zayd ni Swahiyh. Miongoni mwa mambo ya kushangaza ni kwamba Ibn Hamaam amejisalimisha kule kusihi kwake licha ya kwamba ameipinga ule msingi wake kwa hoja kwamba ni kitendo cha Swahabah aliyedhania kuwa jambo hilo ni Sunnah. Hivi pamoja na kwamba madhehebu yake ni kuwa maneno ya Swahabah anaposema “Sunnah ni kufanya hivi” iko katika maana ya Hadiyth ambayo imeungana cheni ya wapokezi wake (Musnad), kama tulivyokwishanakili kutoka kwake katika masuala ya 77, ukurasa wa 120. Rejea katika masuala ya 73, ukurasa wa 109-100. Humo mna majibu aina nyingine ya ushabiki na kuwatia makosani Maswahabah pasi na hoja yoyote.

  • Mhusika: Imaam Muhammad Naaswir-ud-Diyn al-Albaaniy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Ahkaam-ul-Janaa-iz wa Bid´ahaa, uk. 190-192
  • Imechapishwa: 14/03/2022