34. Maana ya maiti anaadhibiwa kwa kule kumlilia

Tambua ya kwamba Hadiyth hizi hazihitaji kufasiriwa kwa njia hizi ndefu na wala haziendi kinyume na maandiko dhahiri ya Qur-aan, msingi wa Kishari´ah wala mtu mwingine kuadhibiwa kwa madhambi ya mwengine. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) hakusema: “Hakika maiti anaadhibiwa kwa familia yake kumlilia” na “Hakika maiti anaadhibiwa kwa kumfanyizia maombolezo… ” Alisema kuwa anateswa. Haina shaka kwamba hayo yanamuumiza na kumtesa. Mateso ni maumivu yanayomfika na yameenea zaidi kuliko adhabu. Kilichoenea hakipelekei katika kilicho maalum. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Safari ni sehemu ya mateso.”

Kuteseka huku kunamfika muumini na kafiri. Maiti hufikwa na maumivu ndani ya kaburi lake ikiwa amezikwa karibu na Ahl-ul-Bid´ah na watenda madhambi kama ambavyo aliye hai anaudhiwa na jirani yake. Imaam Ahmad amesema kuwa maiti huudhika na maasi yanayofanywa kwenye makaburi yao. Familia ya maiti wakimlilia yule maiti kilio cha haramu na wakajipiga kwenye mashavu, wakachana nguo, kujitia makucha usoni na kuzipaka rangi nyeusi, kukokota nywele na kuita wito kwa njia za kishirikina – na yote haya yanapatikana kwa wajinga wengi wa zama hizi – maiti huhisi maumivu kwa sababu ya hilo. Maumivu haya ni adhabu anayohisi kwa kule kumlilia. Haya ndio maoni ya Shaykh-ul-Islaam Ibn Taymiyyah.

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Muhammad al-Hanbaliy al-Manbajiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Tasliyatu Ahl-il-Maswaa-ib, uk. 57-58
  • Imechapishwa: 14/10/2016