33. Maiti anaadhibiwa kwa familia yake kumlilia

Kuhusiana na maneno yake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) “Hakika maiti anaadhibiwa kwa familia yake kumlilia” na “Hakika maiti anaadhibiwa kwa kumfanyizia maombolezo… ” Salaf na waliokuja nyuma wametofautiana juu ya hilo.

Kuna kundi limesema ya kwamba Allaah anafanya kwa viumbe Wake anavyotaka na kwamba matendo ya Allaah hayahojiwi. Wanasema kuwa hakuna tofauti kwa kule kuadhibiwa kwa kuombolezewa na mengine anayonasibishiwa. Kwa kuwa Allaah ndiye muumba wa kila kitu na anawafanya watoto, wanyama na wendawazimu kuhisi maumivu pasi na kuwa wamefanya kitu.

Kundi lingine limesema ya kwamba Hadiyth hizi hazisihi kutoka kwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na kwamba ´Aaishah (Radhiya Allaahu ´anhaa) amezikataa na ametumia hoja kwa maneno Yake (Ta´ala):

وَلَا تَزِرُ وَازِرَةٌ وِزْرَ أُخْرَىٰ

“Mbebaji hatobeba mzigo wa mwengine.” 35:18

Aidha kuna Hadiyth zingine ´Aaishah (Radhiya Allaahu ´anhaa) alizitumia kama dalili ambazo hatukuzitaja. Moja wapo ni maneno ya ´Urwah:

“´Aaishah (Radhiya Allaahu ´anhaa) alifikiwa na khabari ya kwamba Ibn ´Umar (Radhiya Allaahu ´anhumaa) amesimulia kuwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema: “Hakika maiti anaadhibiwa kwa familia yake kumlilia.” ´Aaishah akawa amesema: “Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) hakusema kuwa anaadhibiwa kwa dhambi yake au kwa familia yake kumlilia hivi sasa.”? Ni kama mfano wa maneno ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kuwaambia washirikina waliokuwa wamelala shimoni “Wanasikia ninayoyasema hivi sasa.” Amekosea. Alichosema Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ilikuwa ni: “Hivi sasa wanajua yale niliyokuwa nawaambia ni haki.” Kisha akasoma:

وَمَا يَسْتَوِي الْأَحْيَاءُ وَلَا الْأَمْوَاتُ ۚ إِنَّ اللَّـهَ يُسْمِعُ مَن يَشَاءُ ۖ وَمَا أَنتَ بِمُسْمِعٍ مَّن فِي الْقُبُورِ

“Na wala hawalingani sawa walio hai na maiti. Hakika Allaah anamsikilizisha amtakaye na wewe huwezi kuwasikilizisha waliyomo makaburini.” 35:22

Amesema: “Wameshajiandalia mahala pao Motoni.”

Ameipokea al-Bukhaariy na Muslim.

´Abdullaah bin ´Ubaydillaah bin Abiy Mulaykah amesema:

“Alifariki msichana wa ´Uthmaan Makkah. Tukaja ili kushuhudia na mahala hapo alikuwepo Ibn ´Umar na Ibn ´Abbaas ambao mimi nilikaa baina yao. ´Abdullaah bin ´Umar akamwambia Ibn ´Abbaas: “Huwakatazi kulia? Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema: “Hakika maiti anaadhibiwa kwa familia yake kumlilia” Ibn ´Abbaas akasema: “´Umar alikuwa akisema sehemu ya hayo. Siku moja nilikuwa pamoja na ´Umar tukitokea Makkah. Tulipofika al-Baydaa´ tukaona msafara. Akanambia: “Tazama ni msafara wa nani.” Nikafanya hivo na nikaona kuwa Swuhayb yuko kwenye msafara huo. Nikarudi kumweleza. Akasema: “Niitikie naye.” Nikarudi kwa Swuhayb na kumwambia: “Panda tumuwahi kiongozi wa waumini.” Pindi ´Umar alipodungwa kisu Swuhayb akaanza kulia na kusema: “Ndugu yangu! Rafiki yangu!” ´Umar akasema: “Ee Swuhayb! Unalia ilihali Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema “Hakika maiti anaadhibiwa kwa familia yake kumlilia.”? ´Umar alipofariki nikamweleza hayo ´Aaishah. ´Aaishah akasema: “Allaah amrehemu ´Umar. Ninaapa kwa Allaah kwamba Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) hakusema amesema “Hakika maiti anaadhibiwa kwa familia yake kumlilia”. Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alichosema ni kwamba: “Allaah anamzidishia adhabu kafiri kwa familia yake kumlilia.” Yanakutoshelezeni yale yaliyo katika Qur-aan:

وَلَا تَزِرُ وَازِرَةٌ وِزْرَ أُخْرَىٰ

“Mbebaji hatobeba mzigo wa mwengine.” 35:18

Baada ya hapo Ibn ´Abbaas akasoma:

وَأَنَّهُ هُوَ أَضْحَكَ وَأَبْكَىٰ

“Yeye ndiye Anayesababisha kicheko na Yeye ndiye Anayesababisha kilio.” 53:43

Ibn Abiy Mulaykah akasema:

“Ninaapa kwa Allaah Ibn ´Umar hakusema kitu tena.”

Ameipokea al-Bukhaariy na ni upokezi wake na Muslim vilevile amepokea ya kwamba ´Aaishah alipata khabari kwamba ´Umar na Ibn ´Umar wanasema: Hakika maiti anaadhibiwa kwa wale waliohai kumlilia.” Ndipo akasema: “Nyinyi mnanieleza kutoka kwa watu wawili wasiosema uongo wala hawatuhumiwi uongo, lakini usikizi unakosea.” Katika upokezi mwingine alisema: “Allaah amsamehe Abu ´Abdir-Rahmaan. Hakusema uongo, lakini amesahau na kukosea. Mambo yalivyo ni kwamba Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alipita karibu na mwanamke myahudi anayeliliwa. Akasema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam): “Wanamlilia na anaadhibiwa ndani ya kaburi lake.”

Kundi la tatu limesema kuwa maiti anaadhibiwa kwa familia yake kumuombolezea endapo atawausia kuomboleza au alikuwa hawakatazi kuomboleza iwapo ilikuwa ni mazowea yao. Anaacha anawausia kuomboleza jambo ambali lilikuwa ni la kawaida kwa waarabu. Mmoja wao amesema:

Nitapofariki niombolezee kwa njia ninayostahiki

Ee msichana wa Ma´bad! Zirarue nguo zako

Kundi la tatu likasema kwamba hili linahusiana na mtu anayetoka katika watu wenye mazowea ya kulia na kuomboleza na ambao hakuwakataza kufanya hivo kabla ya kufa kwake. Kutowakataza ni dalili yenye kuonyesha kuwa anaridhika na kitendo chao. Ibn-ul-Mubaarak ana maoni haya. Maoni haya na yaliyo kabla yake ni moja. Abul-Barakaat bin Taymiyyah amesema:

“Moni haya ndio sahihi zaidi. Ikiwa ana dhana ya nguvu kwamba wataomboleza na asiwakataze, hiyo ina maana kwamba ameridhia kitendo chao. Katika hali hii anakuwa kama mtu ambaye anaweza kukataza maovu lakini asifanye hivo. Lakini endapo atawakataza lakini hata hivyo wakapuuza, Allaah ni mkarimu zaidi kwa kumuadhibu kwa hilo.”

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Muhammad al-Hanbaliy al-Manbajiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Tasliyatu Ahl-il-Maswaa-ib, uk. 54
  • Imechapishwa: 14/10/2016