Mu´aawiyah bin Abiy Sufyaan (Radhiya Allaahu ´anhumaa) amesema:

“Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) amekataza kujitelezesha.”[1]

´Iysaa bin Yuunus amesema:

“Kujitelezesha ni yale mambo ambayo mtu hayahitajii katika kuulizia vipi.”[2]

al-Khatwaabiy amesema:

“Kunafahamisha kwamba inachukiza kupekua yale mambo ambayo mtu hayahitajii na uwajibu wa kusimama kwa yale ambayo muulizwaji hana elimu kwayo.”[3]

Allaah (Tabaarak wa Ta´ala) hajawaamrisha waja Wake wala kuwaamrisha kupekua namna zilivyo sifa Zake – wala hajawataka wao kufanya hivo wala kuwajaalia njia ya kuliendea jambo hilo. Ibn Taymiyyah amesema:

“Kwa ajili hiyo wakati Maalik na wengineo katika Salaf walipoulizwa kuhusiana na maneno Yake (Ta’ala):

الرَّحْمَـٰنُ عَلَى الْعَرْشِ اسْتَوَىٰ

”Mwingi wa rehema amelingana juu ya ´Arshi.”[4]

walisema: “Kulingana juu kunatambulika. Namna haitambuliki. Ni wajibu kuamini hilo na kuuliza juu ya hilo ni Bid´ah.”

Kadhalika Rabiy’ah, ambaye ni mwalimu wake Maalik, alisema hivo hapo awali: Kulingana juu kunatambulika. Namna haitambuliki. Ujumbe ni wenye kutoka kwa Allaah, ni juu ya Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) kufikisha na ni juu yetu kuamini.”

Kwa hivyo akabainisha kuwa kulingana juu kunatambulika na kwamba namna haitambuliki. Hayo mara nyingi yanapatikana kwenye maneno ya Salaf na maimamu. Ndani yake wanakanusha utambuzi wa waja kujua namna zilivyo sifa za Allaah na wanathibitisha kwamba hakuna anayejua namna Allaah alivyo isipokuwa Yeye tu. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Siwezi kukusifu vya kutosha. Wewe ni kama Ulivyojisifu Mwenyewe.”[5]

Imekuja Katika Hadiyth nyingine:

“Nakuomba kwa kila jina ambalo ni Lako, Umejiita kwalo, Umeliteremsha ndani ya Kitabu Chako, Umemfunza yeyote katika waja Wako au umelificha katika elimu ya ghaibu Kwako.”[6]

Hapa anaeleza kuwa Allaah yuko na majina ambayo ameyahifadhi katika elimu ya ghaibu Kwako Mwenyewe.”[7]

[1] Ahmad (5/435) na Abu Daawuud (3656). Dhaifu kwa mujibu wa al-Albaaniy katika “Dhwa´iyf Sunan Abiy Daawuud” (3656).

[2] Ibn Battwah (1/401).

[3] Ma´aalim-us-Sunan (5/250).

[4] 20:5

[5] Abu Daawuud (1427), at-Tirmidhiy (3566), an-Nasaa’iy (1748), Ibn Maajah (1179) na Ahmad (751) kupitia kwa ´Aliy (Radhiya Allaahu ´anh).

[6] Ahmad (1/391) na al-Haakim (1/509). Swahiyh kwa mujibu wa al-Albaaniy katika “Swahiyh-ul-Kalim at-Twayyib” (102).

[7] Majmuu´-ul-Fataawaa (3/58).

  • Muhusika: Shaykh ´Abdur-Razzaaq bin ´Allaamah ´Abdil-Muhsin al-´Abbaad al-Badr
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-Athar al-Mash-huur ´an-il-Imaam Maalik fiy Swifat-il-Istiwaa’, uk. 55-56
  • Imechapishwa: 02/12/2025