Mmefikiwa na kumi la mwisho wa Ramadhaan. Ndani yake kuna kheri na ujira mkubwa. Humo mna fadhilah zilizotangaa na sifa za kipekee zinazotajwa.

Miongoni mwa sifa zake za kipekee ni kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikuwa akijitahidi kufanya matendo zaidi kuliko anavofanya wakati mwingine. Muslim amepokea katika “as-Swahiyh” yake kupitia kwa ´Aaishah (Radhiya Allaahu ´anhaa) aliyesimulia:

“Mtume  (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikuwa akijitahidi katika masiku kumi ya mwisho zaidi na anavyojitahidi katika masiku mengine.”

al-Bukhaariy na Muslim wamepokea katika “as-Swahiyh” zao kupitia kwa huyohuyo aliyesimulia:

“Mtume  (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ilikuwa zinapoingia zile siku kumi za mwisho basi hufunga vizuri kikoi chake, anahuisha usiku wake na anaiamsha familia yake.”

Katika “al-Musnad” imepokelewa kupitia kwake huyohuyo:

“Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikuwa akizichanganya siku ishirini katika swalah na usingizi. Zitapofika zile siku kumi basi anajipinda na kukaza vizuri kikoi chake.”

Katika Hadiyth hizi kuna dalili juu ya fadhilah za siku hizi kumi, kwa sababu Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikuwa akijitahidi ndani yake zaidi kuliko anavyojitahidi wakati mwingine. Hili linakusanya kujitahidi katika aina zote za ´ibaadah kukiwemo swalah, Qur-aan, kufanya Dhikr, swadaqah na mengineyo. Kwa sababu Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikuwa akikaza kikoi chake, ikiwa na maana kuwaepuka wakeze, kwa ajili ya kupata muda wa kuswali na kufanya Dhikr. Jengine ni kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikuwa akihuisha usiku wake kwa kusimama usiku, kusoma Qur-aan, kufanya Dhikr kwa moyo, mdomo, viungo vyake vya mwili  kutokana na utukufu wa nyusiku hizi na kutafuta usiku wa makadirio ambao yule atakauyesimama kwa imani na kwa matarajio, basi Allaah atamsamehe madhambi yake yaliyotangulia.

Udhahiri wa Hadiyth hizi ni kwamba yeye (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikuwa akiziuisha nyusiku zote katika kumwabudu Mola wake kama vile kumtaja, kusoma Qur-aan, kuswali, kujiandaa kwa ajili ya hilo, kula daku na mengineyo. Kwa hivo ndio yanakusanywa baina yake na yale yaliyomo ndani ya “as-Swahiyh” ya Muslim kupitia kwa ´Aaishah (Radhiya Allaahu ´anhaa) aliyesimulia kwa kusema:

“Sitambui yeye (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kusimama usiku wowote mpaka asubuhi.”

Kwa sababu kuhuisha usiku kulikothibiti katika yale masiku kumi kunakuwa kwa kusimama usiku kuswali na aina mbalimbali za ´ibaadah. Yeye alichokanusha ni kusimama usiku kuswali peke yake – na Allaah ndiye mjuzi zaidi.

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Majaalis Shahr Ramadhwaan, uk. 154-155
  • Imechapishwa: 07/03/2024