32. Msimamo wa bosi kazini juu wafanyikazi wasiokuwa waislamu

Swali 32: Mmiliki wa kampuli ana wafanyikazi wasiokuwa waislamu. Je, inafaa kwake kuwakataza kula na kunywa mbele ya wafanyikazi wengine ambao ni waislamu ndani ya kampuni hiyohiyo kipindi cha mchana wa Ramadhaan?

Jibu: Mosi tunasema kuwa haitakikani kwa mtu kutumia wafanyikazi wasiokuwa waislamu pamoja na kwamba anao uwezo wa kuwatumia ambao ni waislamu. Waislamu ni wabora kuliko wasiokuwa waislamu. Allaah (Ta´ala) amesema:

وَلَعَبْدٌ مُّؤْمِنٌ خَيْرٌ مِّن مُّشْرِكٍ وَلَوْ أَعْجَبَكُمْ

”Mtumwa muumini ni bora kuliko mshirikina, japo akikupendezeni.”[1]

Lakini haja ikipelekea kutumia wafanyikazi wasiokuwa waislamu basi hakuna neno kwa kiasi cha haja peke yake.

Ama kula na kunywa kwao mchana wa Ramadhaan mbele ya wafungaji waislamu ni jambo halina ubaya. Kwa sababu mfungaji muislamu anamshukuru Allaah (´Azza wa Jall) kumwongoza katika Uislamu ambao ndio kuna furaha ya duniani na Aakhirah na pia anamshukuru Allaah kwa kumlinda kutokamana na yale ambayo Allaah amewatahini kwayo hawa ambao hawakuongozwa na uongofu wa Allaah (´Azza wa Jall). Yeye, hata kama atazuiwa kula na kunywa katika michana ya Ramadhaan katika dunia hii kwa mujibu wa Shari´ah, basi atapokea malipo yake siku ya Qiyaamah pale atakapoambiwa:

كُلُوا وَاشْرَبُوا هَنِيئًا بِمَا أَسْلَفْتُمْ فِي الْأَيَّامِ الْخَالِيَةِ

“Kuleni na kunyweni kwa furaha kwa yale mliyoyatanguliza katika siku nyingi zilopita.”[2]

Lakini mmiliki anatakiwa kuwazuia wasiokuwa waislamu kudhihirisha ulaji na unywaji katika maeneo ya umma kwa sababu ya kitendo hicho kupingana na muonekano wa Kiislamu katika nchi.

[1] 02:221

[2] 69:24

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: 48 mas-alatu fiy Swiyaam, uk. 30
  • Imechapishwa: 23/04/2021