146 – Abul-´Abbaas as-Sarraaj  amesema katika kitabu chake “ar-Radd ´alaal-Jahmiyyah”: al-Husayn bin Yaziyd ametuhadithia: ´Abdus-Salaam bin Harb ametuhadithia, kutoka kwa Abu Khaalid ad-Daalaaniy, kutoka kwa al-Minhaal bin ´Amr, kutoka kwa ´Abdullaah bin al-Haarith, kutoka kwa Abu Hurayrah ambaye amesema:

”Watu watakusanywa hali ya kuwa peku, uchi, wakitembea na wakisimama. Miaka arobaini watalitazama juu wakisubiri kuhukumiwe. Jasho litawatoka mpaka kwenye midomo. Allaah atashuka chini kwenye vivuli vya mawingu katika ´Arshi ambapo aseme: ”Mvisheni nguo Ibraahiym.” Halafu Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akasema: ”Atavishwa nguo mbili katika nguo za Peponi. Nitasimama upande wa kulia wa ´Arshi. Hakuna mwingine atakayesimama mahali hapo isipokuwa mimi tu.”[1]

Upokezi unaotambulika umesimuliwa kutoka kwa al-Minhaal, kutoka kwa Abu ´Ubaydah, kutoka kwa Masruuq, kutoka kwa ´Abdullaah.

147 – al-A´mash amesimulia kutoka kwa Abu Swaalih, kutoka kwa Abu Hurayrah, kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ambaye amesema katika Hadiyth ndefu ya Kufufuliwa:

”Hatimaye kubaki waislamu peke yao. Kutasemwa: ”Je, si muondoke?” Wengine wote wameondoka.” Watasema: ”Mpaka aje Mola wenu.” Kutasemwa: ”Ni nani Mola wenu?” Watasema: ”Mola wenu ni Allaah – ambaye hana mshirika yeyote.” Aseme: ”Je, mnamjua?” Wataseme: ”Akijitambulisa, tutamjua.” Ndipo aseme: ”Mimi ni Mola wenu.” Waseme: ”Tunajilinda kwa Allaah kutokana nawe.” Ndipo awafunulie muundi ambapo wamporomokee kumsujudia. Kisha Aondoke na wao wamfuate.”[2]

148 – Abu ´Abdillaah bin Mandah amesema: al-Hasan bin Mansuur – imamu wa Himsw – ametuhadithia: ´Amr bin Ishaaq bin Ibraahiym ametuhadithia: Muhammad bin Ismaa´iyl bin ´Ayyaash ametuhadithia: Baba yangu amenihadithia: Swafwaan bin ´Amr ametuhadithia, kutoka kwa ´Abdur-Rahmaan bin Jubayr, kutoka kwa baba yake, kutoka kwa Mu´aadh, kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ambaye amesema:

”Wakati Mola atakaposhuka kutoka kwenye ´Arshi Yake siku ya Qiyaamah kwa ajili ya Hesabu, basi ataita mwitaji: ”Enyi watu! Mola wenu ameshuka na Malaika Wake na vivuli vya mawingu.” Ataita sauti kwa uwezo na ufalme Wake:

أَتَىٰ أَمْرُ اللَّـهِ فَلَا تَسْتَعْجِلُوهُ

”Amri ya Allaah inakuja, basi msiihimize!”[3]

Hadiyth hii ni yenye kupingana sana na zilizo Swahiyh.

149 – Mu´tamir bin Sulaymaan ameeleza, kutoka kwa ´Abdul-Jaliyl al-Qaysiy, kutoka kwa Abu Haazim, kutoka kwa ´Abdullaah bin ´Amr aliyesema:

”Atashuka wakati Ataposhuka. Kati yake Yeye na viumbe Wake kutakuwa kuna pazia 70.000, kukiwemo nuru, giza na maji. Maji yatatoa sauti ambayo kwenye giza itayozifanya nyoyo kusimama.”[4]

Ameipokea Abu ´Aliy al-Mawsiliy, kutoka kwa al-Muqaddamiy, kutoka kwake. Vilevile Abush-Shaykh ameipokea kutoka kwake. Cheni yake ya wapokezi ni njema.

150 – ´Uthmaan ad-Daarimiy amesema: ´Abdullaah bin Swaalih ametuhadithia: Ibn Lahiy´ah amenihadithia, kutoka kwa Yaziyd bin Abiy Habiyb, kutoka kwa Sinaan bin Sa´d, kutoka kwa Anas ambaye amesema:

”Siku ya Qiyaamah Allaah ataibadilisha ardhi kwa nyingine ya fedha ambayo haijawahi kufanyiwa madhambi. Baada ya hapo Allaah ashuke juu yake.”

Upokezi mgeni, unaopingana na maneno ya Swahabah.

151 – Ashal amesimulia kutoka kwa Ibn Abiy Yahyaa, kutoka kwa Mujaahid ambaye amesema kuhusu maneno Yake Allaah (Ta´ala):

هَلْ يَنظُرُونَ إِلَّا أَن يَأْتِيَهُمُ اللَّـهُ فِي ظُلَلٍ مِّنَ الْغَمَامِ وَالْمَلَائِكَةُ

”Je, wanangojea nini isipokuwa Allaah awajie katika vivuli vya mawingu pamoja na Malaika?”[5]

”Haya sio mawingu. Hakuna waliopata jambo hilo isipokuwa tu wana wa israaiyl wakati wa safari yao ya jangwani. Ndicho atachokuja nacho Allaah siku ya Qiyaamah.”

152 – ´Abdullaah bin Ahmad bin Hanbal amesema: Baba yangu amenihadithia: ´Abdur-Razzaaq ametuhadithia, kutoka kwa Ma´mar, kutoka kwa Qataadah ambaye amesema kuhusu maneno Yake (Ta´ala):

هَلْ يَنظُرُونَ إِلَّا أَن يَأْتِيَهُمُ اللَّـهُ فِي ظُلَلٍ مِّنَ الْغَمَامِ وَالْمَلَائِكَةُ

”Je, wanangojea nini isipokuwa Allaah awajie katika vivuli vya mawingu pamoja na Malaika?”[6]

”Allaah atawajia katika vivuli vya mawingu, na Malaika watawajia wakati wa mauti.”[7]

Shaybaan an-Nahawiy amepokea mfano wake kutoka kwa Qataadah.

153 – Hajjaaj amepokea kutoka kwa Ibn Jurayj ambaye amesema kuhusu maneno Yake Allaah (Ta´ala):

وَيَوْمَ تَشَقَّقُ السَّمَاءُ بِالْغَمَامِ وَنُزِّلَ الْمَلَائِكَةُ تَنزِيلًا

”Na Siku itakayofunguka mbingu kwa mawingu na Malaika watateremshwa mteremsho mkubwa wa mfuatano.”[8]

”Ambaye atakuja ni Allaah katika vivuli vya mawingu. Wanasema vitakuwa Peponi.”[9]

[1] at-Tirmidhiy (5/585).

[2] al-Bukhaariy (8/212) na (9/229).

[3] 16:1

[4] Jaamiy´-ul-Bayaan (19/11).

[5] 02:210

[6] 02:210

[7] as-Sunnah, uk. 187, na Jaamiy´-ul-Bayaan (2/191).

[8] 25:25

[9] Jaamiy´-ul-Bayaan (5/19).

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Imaam Shams-ud-Diyn Muhammad bin Ahmad adh-Dhahabiy (afk. 748)
  • Marejeo: al-Arba´iyn fiy Swifaati Rabb-il-´Aalamiyn, uk. 150-157
  • Imechapishwa: 23/06/2024