Shaykh-ul-Islaam Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab (Rahimahu Allaah) amesema:

Dalili ya khofu ni Kauli Yake (Ta´ala):

فَلَا تَخَافُوهُمْ وَخَافُونِ إِن كُنتُم مُّؤْمِنِينَ

“Basi msiwakhofu – na nikhofuni Mimi, mkiwa ni waumini.”[1]

MAELEZO

Kama tulivyotangulia kusema khofu inayokusudiwa ni ile ya aina ya ´ibaadah. Kwa mfano mtu amukhofu aliye ndani ya kaburi kwa njia ya kwamba akakhofu kumzuia asiingie Peponi, akamukhofu asimwingize Motoni au akakhofu adui yake asimshambulie katika siri yake na si kitu kilicho dhahiri. Kuhusu kumukhofu adui aliye mbele yako na isitoshe pengine yuko na silaha au pia ukakhofu wanyama wakali, hiyo ni khofu ya kimaumbile. ash-Shawkaaniy (Rahimahu Allaah) amesema:

وَخَافُونِ

“… na nikhofuni Mimi.”

kwa kuyafanya yale niliyokuamrisheni na kujiepusha yale niliyokukatazeni. Huyo ndio ukweli wa kuniogopa na kuchuga maamrisho na makatazo Yangu. Kwani kheri na shari vyote viko mikononi Mwangu.”[2]

Mitume ndio walikuwa viumbe wanaomukhofu Allaah zaidi. Nuuh (´alayhis-Salaam) alisema kuwaambia watu wake:

يَا قَوْمِ اعْبُدُوا اللَّـهَ مَا لَكُم مِّنْ إِلَـٰهٍ غَيْرُهُ إِنِّي أَخَافُ عَلَيْكُمْ عَذَابَ يَوْمٍ عَظِيمٍ

“Enyi watu wangu! Mwabuduni Allaah, kwani hakika hamna mungu wa haki asiyekuwa Yake. Hakika mimi nakukhofieni adhabu ya Siku kubwa mno.”[3]

Shu´ayb (´alayhis-Salaam) alisema kuwaambia watu wake:

قَالَ يَا قَوْمِ اعْبُدُوا اللَّـهَ مَا لَكُم مِّنْ إِلَـٰهٍ غَيْرُهُ ۖ وَلَا تَنقُصُوا الْمِكْيَالَ وَالْمِيزَانَ ۚ إِنِّي أَرَاكُم بِخَيْرٍ وَإِنِّي أَخَافُ عَلَيْكُمْ عَذَابَ يَوْمٍ مُّحِيطٍ

“Enyi watu wangu! Mwabuduni Allaah, kwani hakika hamna mungu wa haki asiyekuwa Yake na wala msipunguze kipimo na mizani. Hakika mimi nakuoneni mko kwenye kheri na hakika mimi nakukhofieni adhabu ya siku yenye kuzingira.”[4]

Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

قُلْ إِنِّي أَخَافُ إِنْ عَصَيْتُ رَبِّي عَذَابَ يَوْمٍ عَظِيمٍ مَّن يُصْرَفْ عَنْهُ يَوْمَئِذٍ فَقَدْ رَحِمَهُ ۚ وَذَٰلِكَ الْفَوْزُ الْمُبِينُ

“Sema: “Hakika mimi nakhofu, ikiwa nitamuasi Mola wangu, adhabu ya Siku kuu. Yule atakayeepushwa nayo Siku hiyo, basi kwa hakika [Allaah] amemrehemu – na huko ndiko kufuzu kuliko wazi.”[5]

Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikuwa akiswali na huku kifuani mwake akitokwa na sauti ya kilio kama ya chungu kinachochemka maji[6]. Kila ambavyo mtu anamtambua Allaah zaidi ndivo anamuogopa zaidi. Ibn Mas´uud (Radhiya Allaahu ´anh) amesema:

“Inatosha mtu akamtambua Allaah kwa kule kumuogopa na inatosha ujinga mtu akaghurika na Allaah.”[7]

Mtu kupungukiwa na khofu ya Allaah inatokana na kupungua utambuzi wa mja juu ya Mola Wake. Kwa hivyo watu wanaomtambua Allaah zaidi ndio wanaomcha Allaah zaidi. Anayemtambua Allaah zaidi khofu, hayaa na mapenzi yake yanakuwa makubwa zaidi Kwake. Kila ambavyo utambuzi wa mja unavyokuwa mkubwa zaidi ndivo yanavyozidi hayaa, khofu na mapenzi yake. Khofu na woga unakuwa kwa kiwango cha ujuzi na utambuzi wa mja. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Mimi ndiye ninayemjua Allaah zaidi na kumuogopa zaidi.”[8]

Shaykh-ul-Islaam (Rahimahu Allaah) amesema:

“Kumkhofu Allaah kunapelekea kuwa na ujuzi juu Yake, ujuzi juu Yake unapelekea kumukhofu na kumukhofu kunapelekea kumtii.”[9]

Kumukhofu ni miongoni mwa sababu za kutengemaa kwa moyo. Shaykh-ul-Islaam (Rahimahu Allaah) amesema:

“Mipaka ya Allaah haikuchungwa, yale aliyoharamisha na wakamfikia wale waliomfikia kwa mfano wa kumukhofu, kumtaraji na kumpenda. Pindi moyo unapokuwa mtupu kutokamana na mambo haya matatu, basi unaharibika uharibifu ambao hakutarajiwi kutengemaa kamwe. Na pale kunapodhoofika kitu katika mambo haya, basi imani yake inadhoofika kwa kiwango chake.“[10]

[1] 03:175

[2] Fath-ul-Qadiyr (01/459).

[3] 07:59

[4] 11:84

[5] 06:15-16

[6] Abu Daawuud (904) na an-Nasaa´iy (1214).

[7] at-Twabaraaniy katika ”al-Kabiyr” (09/189) na al-Bayhaqiy katika “Shu´ayb-ul-Iymaan” (02/32).

[8] al-Bukhaariy (6101) na Muslim (2356).

[9] Majmuu´-ul-Fataawaa (15/24).

[10] Majmuu´-ul-Fataawaa (15/21).

  • Mhusika: ´Allaamah ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah ar-Raajihiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Thalaathat-il-Usuwl, uk. 52-53
  • Imechapishwa: 07/02/2023