Shaykh-ul-Islaam Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab (Rahimahu Allaah) amesema:

Dalili ni Kauli Yake (Ta´ala):

وَقَالَ رَبُّكُمُ ادْعُونِي أَسْتَجِبْ لَكُمْ ۚ إِنَّ الَّذِينَ يَسْتَكْبِرُونَ عَنْ عِبَادَتِي سَيَدْخُلُونَ جَهَنَّمَ دَاخِرِينَ

“Mola wenu Amesema: “Niombeni, Nitakuitikieni. Hakika wale wanaotakabari na ‘Ibaadah Yangu, wataingia Motoni hali ya kudhalilika.”[1]

MAELEZO

Hii ndio dalili kutoka ndani ya Qur-aan ya kwamba du´aa ni ´ibaadah kwa sababu du´aa imeitwa kuwa ni ´ibaadah.

Du´aa iliyoamrishwa katika Aayah ni du´aa ´ibaadah na du´aa ya kuomba. Ikiwa du´aa ni ya ´ibaadah, basi kule kuitikiwa ni yale malipo yanayotoka kwa Allaah. Ikiwa du´aa ni ya maombi, basi kuitikiwa ni kule muombaji kuyafikia malengo yake na kulipwa pia. Kwa sababu kila mwenye kuomba, ijapo maombi yake ni mambo ya kidunia, basi analipwa thawabu kwa maombi yake. Akiomuomba Allaah amruzuku kipando kizuri, mke mwema na nyumba pana, haya ni miongoni mwa mambo ya kidunia ambayo anaburudika nayo duniani. Akimuomba Allaah basi kumuitikia Kwake (Subhaana) inakuwa kwa kumlipa thawabu, jambo ambalo linahakikiwa kwa kila mwombaji. Imepokelewa kutoka kwake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ya kwamba amesema:

“Asiyemuomba Allaah basi anamghadhibikia.”[2]

Kuhusu kufikia malengo yake ni jambo linaloweza kutokea na wakati mwingine halitokei kutegemea na hekima ya Allaah (´Azza wa Jall) katika kuhakikisha matakwa ya mja, kumuwekea akiba ya jambo hilo huko Aakhirah au kumzuilia sawa ya shari ya kile alichoomba au mfano wa kile alichoomba.

[1] 40:60

[2] at-Tirmidhiy (3373).

  • Mhusika: ´Allaamah ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah ar-Raajihiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Thalaathat-il-Usuwl, uk. 51
  • Imechapishwa: 07/02/2023