30. Mwenye kumuomba asiyekuwa Allaah ni mshirikina na kafiri

Shaykh-ul-Islaam Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab (Rahimahu Allaah) amesema:

Dalili ni maneno Yake (Ta´ala):

وَأَنَّ الْمَسَاجِدَ لِلَّـهِ فَلَا تَدْعُوا مَعَ اللَّـهِ أَحَدًا

“Sehemu zote za kuswalia ni kwa ajili ya Allaah, hivyo basi msiombe yeyote pamoja na Allaah.”[1]

Mwenye kumtekelezea chochote katika hayo mwengine asiyekuwa Allaah ni mshirikina kafiri. Dalili ya hilo ni Kauli Yake (Ta´ala):

وَمَن يَدْعُ مَعَ اللَّـهِ إِلَـٰهًا آخَرَ لَا بُرْهَانَ لَهُ بِهِ فَإِنَّمَا حِسَابُهُ عِندَ رَبِّهِ ۚإِنَّهُ لَا يُفْلِحُ الْكَافِرُونَ

“Yeyote yule anayeomba pamoja na Allaah mungu mwengine hana ushahidi wowote juu ya hilo, basi hakika hesabu yake iko kwa Mola wake, kwani hakika hawafaulu makafiri.”[2]

Katika Hadiyth imekuja:

“Du´aa ndio kiini cha ´ibaadah.”[3]

 MAELEZO

Bi maana dalili ya kwamba ´ibaadah ni haki ya Allaah na kwamba mwenye kumtekelezea asiyekuwa Allaah ameingia ndani ya shirki na ukafiri. Shirki inayokusudiwa hapa ni ile kubwa na ule ukafiri wenye kumtoa mtu nje ya dini. Shaykh-ul-Islaam (Rahimahu Allaah) amesema:

“Hakika waislamu wameafikiana juu ya yale mambo yanayotambulika vyema katika Uislamu ya kwamba haijuzu kwa mja kumwabudu, kumuomba, kumtaka uokozi wala kumtegemea mwingine asiyekuwa Allaah, na kwamba ambaye atamwabudu Malaika aliye karibu au Mtume aliyetumwa au akamuomba au akamtaka uokozi basi huyo ni mshirikina.”[4]

Maneno Yake (Ta´ala):

وَمَن يَدْعُ مَعَ اللَّـهِ إِلَـٰهًا آخَرَ لَا بُرْهَانَ لَهُ بِهِ فَإِنَّمَا حِسَابُهُ عِندَ رَبِّهِ ۚإِنَّهُ لَا يُفْلِحُ الْكَافِرُونَ

“Yeyote yule anayeomba pamoja na Allaah mungu mwengine hana ushahidi wowote juu ya hilo, basi hakika hesabu yake iko kwa Mola wake, kwani hakika hawafaulu makafiri.”

Allaah amemuhukumu kuwa ni kafiri. Kwa hivyo yule mwenye kumuomba asiyekuwa Allaah ni kafiri na mshirikina. Allaah (Ta´ala) amesema:

وَالَّذِينَ تَدْعُونَ مِن دُونِهِ مَا يَمْلِكُونَ مِن قِطْمِيرٍ إِن تَدْعُوهُمْ لَا يَسْمَعُوا دُعَاءَكُمْ وَلَوْ سَمِعُوا مَا اسْتَجَابُوا لَكُمْ ۖ وَيَوْمَ الْقِيَامَةِ يَكْفُرُونَ بِشِرْكِكُمْ ۚ وَلَا يُنَبِّئُكَ مِثْلُ خَبِيرٍ

“Wale mnaowaomba badala Yake hawamiliki hata kijiwavu cha kokwa ya tende. Mkiwaomba, hawasikii maombi yenu, na hata wakisikia, hawatakuitikieni na siku ya Qiyaamah watakanusha ushirikina wenu na wala hakuna atakayekujulisha vyema kama Mwenye khabari zote za ndani.”[5]

Mtunzi (Rahimahu Allaah) amesema:

Katika Hadiyth imekuja:

“Du´aa ndio kiini cha ´ibaadah.”

Kiini cha kitu ni ule ubongo wake, mwisho wake na kile inachosimama juu yake. Maana yake ni kwamba ´ibaadah haisimami isipokuwa kwa du´aa. Ni kama ambavyo mtu hawi isipkuwa kwa ubongo kwa kule kumwelekea kwake Allaah na kuvipa mgongo vyengine vyote.

Dalili hii inafahamisha juu ya nafasi ya du´aa ukilinganisha aina nyinginezo za ´ibaadah. Hata hivyo ni Hadiyth dhaifu. Swahiyh ni ile isemayo:

“Du´aa ndio ´ibaadah.”[6]

[1] 72:18

[2] 23:117

[3] at-Tirmidhiy (3371).

[4] Majmuu´-ul-Fataawaa (03/272).

[5] 35:13-14

[6] Abu Daawuud (1479) na at-Tirmidhiy (2969) ambaye amesema:

“Hadiyth hii ni nzuri na Swahiyh.”

Vilevile ameipokea Ibn Maajah (3828).

  • Mhusika: ´Allaamah ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah ar-Raajihiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Thalaathat-il-Usuwl, uk. 49-50
  • Imechapishwa: 07/02/2023