Shaykh-ul-Islaam Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab (Rahimahu Allaah) amesema:

…kutaka msaada, kutaka kinga, kutaka kuokolewa, kuchinja, kuweka nadhiri na aina nyinginezo zote miongoni mwa aina za ´ibaadah ambazo Allaah ameamrisha.

Zote ziwe kwa ajili ya Allaah pekee. 

MAELEZO

Kutaka msaada ni kule kuomba msaada.

Makusudio ya kutaka kinga ni kuomba ulinzi kutokana na yale yanayochukiza. Ni mamoja anayeombwa ulnzi dhidi yake ni adui wa kibinadamu au shaytwaan.

Kutaka kuokolewa ni kule kuomba du´aa kutokamana na dhiki.

Kuchinja ni kule kuichukua roho kwa kumwaga damu kwa njia maalum. Hilo linaweza kufanyika kwa njia nyingi:

1 – Lifanyike kwa njia ya ´ibaadah kwa njia ya kwamba mtu akusudie kumtukuza yule anayemchinjia, kujidhalilisha na kujikurubisha kwake. Aina kama hii haiwi kwa mwingine isipokuwa Allaah pekee.

2 – Lifanyike kwa ajili ya kumtukuza mgeni, kumkirimu mgeni, karamu ya harusi na mfano wake. Aina hii imeamrishwa ima kwa njia ya ulazima au ya mapendekezo. Amesema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Yule anayemwamini Allaah na siku ya Mwisho basi amkirimu mgeni wake.”[1]

Alisema kumwambia ´Abdur-Rahmaan bin ´Awf:

“Fanya karamu ya ndoa japo kondoo mmoja.”[2]

3 – Lifanyike kwa njia ya kufurahia kula nyama, biashara na mfano wake. Aina hii inaingia katika zile sampuli zilizoruhusiwa. Msingi wake ni uhalali. Amesema (Ta´ala):

أَوَلَمْ يَرَوْا أَنَّا خَلَقْنَا لَهُم مِّمَّا عَمِلَتْ أَيْدِينَا أَنْعَامًا فَهُمْ لَهَا مَالِكُونَ وَذَلَّلْنَاهَا لَهُمْ فَمِنْهَا رَكُوبُهُمْ وَمِنْهَا يَأْكُلُونَ

“Je, hawaoni kwamba Sisi tumewaumbia kutokana na yale iliyofanya Mikono Yetu; wanyama wa mifugo – basi wao wanawamiliki? Na Tumewadhalilisha kwao, basi baadhi yao humo ni vipando vyao na wengine humo wanawala?”[3]

Inaweza kuwa ni jambo linalotakikana au lenye kukatazwa kutegemea na ile njia inayopelekea.

Nadhiri ni kule mtu kujilazimisha jambo ambalo kwa mujibu wa Shari´ah hakimlazimu. Kwa mfano mtu aseme kuwa ni lazima kwake kumfungia Allaah siku tano mfululizo ikiwa atamponyeshea mgonjwa wake. Hiyo ndio nadhiri.

Mtunzi wa kitabu (Rahimahu Allaah) ametaja aina hizi kumi na nne kwa njia ya kupigia mfano wa ´ibaadah na si kwa njia ya kufupiliza.

Maneno yake mtunzi (Rahimahu Allaah):

“Zote ziwe kwa ajili ya Allaah pekee.”

Bi maana ´ibaadah zote hizi atekelezewe Yeye pekee. Mtu akimuomba, akimchinjia, akimuwekea nadhiri, akimtaka msaada au akimtaka uokozi mwingine asiyekuwa Allaah anakuwa ameingia kwenye shirki.

[1] al-Bukhaariy (6018) na Muslim (47).

[2] al-Bukhaariy (5153) na Muslim (1427).

[3] 36:71-72

  • Mhusika: ´Allaamah ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah ar-Raajihiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Thalaathat-il-Usuwl, uk. 47-48
  • Imechapishwa: 07/02/2023