Shaykh-ul-Islaam Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab (Rahimahu Allaah) amesema:

Mfano wa aina za ´ibaadah ambazo Allaah ameamrisha ni Uislamu, imani na ihsaan. Miongoni mwa hizo ni du´aa pia, khofu, matarajio, utegemeaji, shauku [raghbah] na woga [rahbah], unyenyekeaji, tisho, kurejea [inaabah],…

MAELEZO

Uislamu maana yake ni kujisalimisha kwa Allaah (Ta´ala) kwa kumpwekesha, kunyenyekea Kwake kwa kumtii na kujitenga mbali na shirki na watu wake.

Imani ni kule kusadikisha kwa moyo, kukubali kwa mdomo na matendo ya viungo vya mwili. Matendo yote haya yanaingia katika imani.

Ihsaan ni kule kumwabudu Allaah hali ya kujua kuwa anakuchunga. Hivyo unamwabudu kana kwamba unamuona na ikiwa wewe humuoni basi tambua kuwa Yeye anakuona.

Maneno yake mtunzi (Rahimahu Allaah):

“Miongoni mwa hizo ni du´aa pia, khofu, matarajio… ”

Bi maana miongoni mwa ´ibaadah ambazo Allaah ameamrisha ni pamoja na du´aa kwa mfano kusema:

يا أرحم الراحمين

“Ee Mwenye kurehemu mkubwa katika wanaorehemu!”

Khofu inayomaanishwa ni ile khofu ya aina ya ´ibaadah ambayo ni khofu ya kisiri. Kuhusu khofu ya kimaumbile kama mtu kuogopa wanyama wakali, moto na kuzama, mja hasimangwi kwa khofu kama hiyo. Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala) amesema kuhusu Muusa (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

فَأَصْبَحَ فِي الْمَدِينَةِ خَائِفًا يَتَرَقَّبُ

“Akapambaukiwa kuwa mwenye khofu katika mji ule anaangaza.”[1]

Lakini khofu hii ikipelekea kuacha jambo la lazima au kufanya jambo la haramu basi nayo inakuwa haramu. Kwa sababu kitu ambacho ni sababu ya kuacha jambo la lazima au kufanya jambo la haramu kinakuwa haramu. Dalili ya hilo ni maneno Yake (Subhaanahu wa Ta´ala):

فَلَا تَخَافُوهُمْ وَخَافُونِ إِن كُنتُم مُّؤْمِنِينَ

“Basi msiwakhofu – na nikhofuni Mimi – mkiwa ni waumini!”[2]

Kwa hiyo kuna khofu yenye kusifiwa na khofu isiyokuwa yenye kusifiwa.

Makusudio ya matarajio ni yale ambayo ni ya aina ya ´ibaadah. Mfano wa matarajio hayo ni kama vile mtu amtarajie maiti kumwingiza Peponi na kumkinga kutokana na Moto. Haya ndio aina ya matarajio ya ´ibaadah. Kuhusu matarajio ya kawaida ni mfano wa pale unapotaraji kutoka kwa mtu mwingine akusaidie. Mtunzi (Rahimahu Allaah) hakusudii matarajio aina hii.

Utegemezi ni kumwegemea Allaah. Yeye (´Azza wa Jall) ndiye Mwenye kufanya sababu zikafanya kazi.

Shauku inayokusudiwa ni kuwa na shauku kwa Allaah na zile thawabu zilizoko Kwake.

Makusudio ya woga ni kumuogopa Allaah na adhabu Yake.

Unyenyekeaji ni kule kutulia. Mara nyingi neno hili hutumiwa likiwa na maana ya utulivu.

Tisho ni kule kuwa na khofu iliombatana na ujuzi. Kwa hivyo tisho ni yenye kuenea zaidi kuliko khofu.

Kurejea ni kule kurudi kwa Allaah na kuacha maasi.

[1] 28:18

[2] 03:175

  • Mhusika: ´Allaamah ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah ar-Raajihiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Thalaathat-il-Usuwl, uk. 45-46
  • Imechapishwa: 07/02/2023