31. Swalah katika miji ambayo usiku au mchana ni mrefu sana

Swali 31: Katika baadhi ya maeneo usiku au mchana unaweza kuendelea kwa kipindi kirefu na wakati mwingine vinaweza kuwa vifupi sana kwa kiasi cha kwamba havipati nafasi vile vipindi vya swalah tano. Ni vipi wakazi wake watatekeleza swalah zao[1]?

Jibu: Ni lazima kwa wakazi wa maeneo haya ambayo mchana au usiku wake unakuwa mrefu waswali zile swalah tano kwa makisio wakiwa hawana kuchomoza wala kuzama kwa jua kwa muda wa masaa ishirini na nne. Hivo ndivo imethibiti kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) katika Hadiyth ya an-Nawwaas bin Sam´aan iliopokelewa katika “as-Swahiyh” ya Muslim kuhusu siku ya ad-Dajjaal ambayo itakuwa ni kama mwaka. Maswahabah wakamuuliza Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) juu ya hilo ambapo akasema:

“Zikadirieni kiwango chake.”[2]

Vivyo hivyo ndivo alivohukumu siku ya pili ambayo itakuwa kama mwezi. Vivyo hivyo ile siku ambayo itakuwa kama wiki.

Kuhusu maeneo ambayo usiku unakuwa mfupi na mchana unakuwa mrefu au kinyume chake ndani ya masaa ishirini na nne, basi hukumu yake iko wazi; wataswali kama masiku mengine hata kama usiku au mchana utakuwa mfupi sana kutokana na kuenea kwa dalili.

[1] Majmuu´-ul-Fataawaa (10/394-395).

[2] Muslim (2937).

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Ahkaam-ul-Musaafir, uk. 47-48
  • Imechapishwa: 13/03/2022