30. Swalah ya ijumaa kwa msafiri anayeishi nchi ya kikafiri

Swali 30: Je, swalah ya ijumaa inatuwajibikia katika nchi hii ya Uhispania pamoja na kuzingatia kwamba hakuna msikiti? Tumekuja katika nchi hiyo kwa sababu ya masomo[1].

Jibu: Wanazuoni wamesema kwamba hakukulazimuni nyinyi wala watu mfano wenu kusimamisha swalah ya ijumaa. Bali ni jambo linalotakiwa kuangaliwa vyema kuhusu kusihi kwake. Kinachokulazimuni ni swalah ya Dhuhr. Kwani nyinyi mmefanana na wasafiri na wale wakazi wa mashambani. Swalah ya ijumaa inawalazimu wale wanaoishi mijini. Dalili ya hilo ni kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) hakuwaamrisha nayo wasafiri wala wale wanaoishi mashambani. Wala yeye hakuiswali katika safari zake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) wala Maswahabah zake (Radhiya Allaahu ´anhum). Imethibiti katika Hadiyth Swahiyh ya kwamba (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) katika hajj ya kuaga aliswali Dhuhr katika ´Arafah siku ya ijumaa na wala hakuswali ijumaa. Wala hakuwaamrisha mahujaji kufanya hivo kwa sababu wana hukumu moja kama wasafiri. Wala sitambui tofauti kutoka kwa wanazuoni wa Kiislamu juu ya suala hili. Isipokuwa tofauti ambayo ni nyonge inayotoka kwa baadhi ya wanafunzi wa Maswahabah na wala haitakiwi kuitegemea. Lakini wakipatikana waislamu wenyeji wanaoswali swalah ya ijumaa basi imesuniwa kwenu na watu mfano wenu ambao ni wakazi wanaokaa katika mji kwa muda fulani kwa ajili ya kusoma, kufanya biashara na mengineyo kuswali pamoja nao kwa ajili ya kuweza kupata fadhilah za ijumaa.

[1] Majmuu´-ul-Fataawaa, uk. 486.

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Ahkaam-ul-Musaafir, uk. 46-47
  • Imechapishwa: 13/03/2022