31. Radd kwa mwenye kuona kumsalimisha mwenye kutamka shahaadah japokuwa atafanya mambo ya kufuru na shirki

Shaykh-ul-Islaam Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab (Rahimahu Allaah) amesema:

Washirikina wana shubuha nyingine. Wanasema: “Kwa hakika Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alimkemea Usaamah pindi alipomuua mtu aliyesema: “Hapana mungu wa haki isipokuwa Allaah”. Na akamwambia:

“Hivi kweli umemuua baada ya yeye kusema “Hapana mungu isipokuwa Allaah?”[1]

Amesema vilevile:

“Nimeamrishwa kuwapiga vita watu mpaka watakaposema “Hapana mungu isipokuwa Allaah”.”[2]

Na kuna Hadiyth zingine zinazozungumzia kumsalimisha yule mwenye kuitamka. Makusudio ya hawa wajinga ni kwamba mwenye kuitamka hawezi kukufuru wala hauawi, walau atafanya yakufanya.

Ndio maana inatakiwa kusemwa kuambiwa washirkina hawa wajinga: “Ni jambo linalojulikana ya kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) aliwapiga vita mayahudi na akawafunga ilihali na wao wanasema “Hapana mungu isipokuwa Allaah”. Na Maswahabah wa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) waliwapiga vita Baniy Haniyfah nao wanashuhudia “Hapana mungu wa haki isipokuwa Allaah na kwamba Muhammad ni Mtume wa Allaah”, wanaswali na kudai Uislamu. Hali kadhalika wale aliowaunguza ´Aliy bin Abiy Twaalib kwa moto. Na wajinga hawa wanakubali kuwa yule mwenye kupinga kufufuliwa anakufuru na kuuawa, hata kama atasema “Hapana mungu wa haki isipokuwa Allaah”, na kwamba yule mwenye kupinga chochote katika nguzo za Uislamu amekufuru na kuuawa, hata ikiwa ataitamka [Shahaadah]. Vipi basi isimfai ikiwa kapinga kitu katika mambo ya matawi, lakini imfae akipinga Tawhiyd ambayo ni msingi na asli ya dini ya Mitume? Lakini maadui wa Allaah hawakufahamu maana ya Hadiyth.

Ama Hadiyth kuhusu Usaamah, alimuua mtu ambaye alidai Uislamu kwa sababu alidhani ya kwamba anadai Uislamu kwa khofu tu ya kuuliwa na mali yake. Na mtu akidhihirisha Uislamu, basi ni wajibu kumwacha mpaka kubainike yanayokhalifu hilo. Allaah ameteremsha juu ya hilo:

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا إِذَا ضَرَبْتُمْ فِي سَبِيلِ اللَّـهِ فَتَبَيَّنُوا

”Enyi mlioamini! Mnapotoka katika njia ya Allaah hakikisheni.” (an-Nisaa´ 04 : 94)

Yaani “thibitisheni”. Aayah inatoa dalili ya kwamba ni wajibu kumsalimisha mpaka mtu athibitishe. Baada ya muda kukibainika kutoka kwake yanayokhalifu Uislamu, anauawa, kwa Kauli Yake (Ta´ala) “hakikisheni”. Na lau ingelikuwa hauawi kabisa akiitamka, basi kuhakikisha kungekuwa hakuna maana yoyote. Hali kadhalika Hadiyth nyingine na mfano wake. Maana yake ni haya tuliyoyataja; ya kwamba mwenye kudhihirisha Tawhiyd na Uislamu basi ni wajibu kumsalimisha isipokuwa ikibainika kutoka kwake yanayotengua hilo. Dalili ya hili ni kwamba Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) aliyesema:

“Hivi kweli umemuua baada ya yeye kusema “Hapana mungu isipokuwa Allaah?””[3]

Amesema vilevile:

“Nimeamrishwa kuwapiga vita watu mpaka watakaposema “Hapana mungu isipokuwa Allaah”.”[4]

ndiye huyo huyo aliyesema kuhusu Khawaarij:

“Popote mtapokutana nao waueni. Lau nitakutana nao, nitawaua kama walivyouawa kina ´Aad”[5],

pamoja na kuwa ni katika watu wenye kufanya ´Ibaadah sana, Tahliyl[6] na Tasbiyh[7]. Mpaka hata Maswahabah walikuwa wakizidharau swalah zao wakilinganisha na zao. Pia wamejifunza elimu kutoka kwa Maswahabah, hata hivyo haikuwafaa kitu “Hapana mungu wa haki isipokuwa Allaah”, wala wingi wa ´Ibaadah wala kudai kwao Uislamu pindi ilipodhihiri kwao kukhalifu kwao Shari´ah. Hali kadhalika kuhusu tuliyoyataja kupigwa vita mayahudi na Maswahabah kuwapiga vita Baniy Haniyfah. Hali kadhalika alitaka Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kuwavamia Baniy al-Mustwalaq baada ya kuambiwa na mtu kutoka katika wao ya kwamba wamekataa kutoa zakaah, mpaka Allaah akawa ameteremsha:

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا إِن جَاءَكُمْ فَاسِقٌ بِنَبَإٍ فَتَبَيَّنُوا

”Enyi mlioamini! Anapokujieni fasiki kwa khabari yoyote ile, basi hakikisheni.” (al-Hujuraat 49 : 06)

Hata hivyo ikaonekana ya kwamba mtu huyo amewasemea uongo[8]. Yote haya yanaonesha dalili ya kwamba makusudio ya Mtume (Swalla Allaah ´alayhi wa sallam) kwa Hadiyth ambazo wanatumia kama hoja ni haya tuliyoyataja.

MAELEZO

Haya ni masuala muhimu na makubwa ambayo mtunzi wa kitabu (Rahimahu Allaah) ameyaweka wazi. Yanahusiana na kutegemea kwa washirikina zile Hadiyth zilizoachwa na zilizoenea zinazozungumzia kumwacha yule mwenye kutamka kwamba hapana mwabudiwa wa haki isipokuwa Allaah. Hivo ni kama walivyofikiria kwamba mwenye kulitamka hakufuru japokuwa atafanya chochote kile. Baadhi ya wengine kwa sababu ya ujinga wao wamedhani kuwa anakufuru kwa kitu kilicho chini ya shirki. Maneno yake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kumwambia Usaamah:

“Hivi kweli umemuua baada ya yeye kusema “Hapana mungu isipokuwa Allaah?””

“Nimeamrishwa kuwapiga vita watu mpaka watakaposema “Hapana mungu wa haki isipokuwa Allaah”. Watapoyasema basi vimesalimika kwangu damu na mali yao isipokuwa kwa haki yake.”

ni dalili juu ya yale waliyopita juu yake Maswaahabah na wengineo juu ya kuwapiga vita wenye kuritadi. Maana ya hayo ni kwamba yule mwenye kudhihirisha Tawhiyd na Uislamu basi anatakiwa kuachwa mpaka pale kutapojulikana kutoka kwake yenye kwenda kinyume  na hayo. Yule ambaye aliuawa na Usaamah alifikiria kuwa ameyatamka kwa kutaka kujikinga na kwa sababu ya kuogopa silaha. Ndio maana alimuua. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akamtia makosani na akambainishia kwamba kilicho cha lazima ni kumwacha kwanza mpaka litazamwe jambo lake. Vivyo hivyo kila mtu ambaye hataki kutamka shahaadah kama mfano wa makafiri wa Quraysh ambao walikataa kuitamka wakati ambapo Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) aliwaambia:

“Semeni ´hapana mungu wa haki isipokuwa Allaah`.”

Wakasema:

أَجَعَلَ الْآلِهَةَ إِلَـٰهًا وَاحِدًا ۖ إِنَّ هَـٰذَا لَشَيْءٌ عُجَابٌ

“Amewafanya waungu kuwa ni mungu Mmoja?  Hakika hili ni jambo la ajabu mno!”[1]

أَئِنَّا لَتَارِكُو آلِهَتِنَا لِشَاعِرٍ مَّجْنُونٍ

”Je, sisi kweli tuache waabudiwa wetu kwa ajili ya mshairi mwendawazimu?”[2]

إِنَّهُمْ كَانُوا إِذَا قِيلَ لَهُمْ لَا إِلَـٰهَ إِلَّا اللَّـهُ يَسْتَكْبِرُونَ وَيَقُولُونَ أَئِنَّا لَتَارِكُو آلِهَتِنَا لِشَاعِرٍ مَّجْنُونٍ بَلْ جَاءَ بِالْحَقِّ وَصَدَّقَ الْمُرْسَلِينَ

“Hakika wao walipokuwa wakiambiwa “hapana mungu wa haki isipokuwa Allaah” wanafanya kiburi na wanasema: “Je, sisi kweli tuache waabudiwa wetu kwa ajili ya mshairi mwendawazimu? Bali amekuja kwa haki na amewasadikisha Mitume.”[3]

Wale wanaopinga kutamka shahaadah wanapolitamka wanatakiwa kuachwa mpaka watazamwe kwanza litazamwe jambo lao. Wakinyooka, wakamwabudu Allaah pekee, wakamtakasia Yeye ´ibaadah na wakashikamana na Shari´ah ya Uislamu basi kutatimia kule kusalimishwa kwao. Lakini wale wenye kutamka shahaadah ilihali hawaamini maana yake na isitoshe wanamwabudu mwengine asiyekuwa Allaah – kama walivyokuwa wanafanya wanafiki na wafuasi wa Musaylamah ambao walikuwa wanaswali lakini wanaona kuwa Musaylamah ni Mtume – wamekadhibisha maneno Yake (Ta´ala):

مَّا كَانَ مُحَمَّدٌ أَبَا أَحَدٍ مِّن رِّجَالِكُمْ وَلَـٰكِن رَّسُولَ اللَّـهِ وَخَاتَمَ النَّبِيِّينَ

“Hakuwa Muhammad baba wa yeyote miongoni mwa wanaume wenu, lakini ni Mtume wa Allaah na ni mwisho wa Manabii.”[4]

Ni vipi atakuwa ni Mtume ilihali Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ndiye Mtume wa mwisho? Kwa ajili hiyo Maswahabah wakawapiga vita kwa sababu walidai kuwa Musaylamah ni Mtume, kitendo ambacho ni kufuru kwa maafikiano. Haijalishi kitu hata kama wanatamka shahaadah. Vivyo hivyo wale waliochomwa moto na ´Aliy bin Abiy Twaalib ambao walidai kuwa ni Allaah. Matokeo yake aliwachoma moto ilihali ni wenye kutamka shahaadah. Wanasema kwa ndimi zao yasiyoendana na matendo yao.

Kadhalika wanafiki wanatamka shahaadah na wakati huohuo wanaamini kuwa dini ni batili na kwamba haina uhakika wowote. Wanaitamka kwa kujionyesha na kwa kujikinga. Pamoja na haya Allaah amesema juu yao:

إِنَّ الْمُنَافِقِينَ فِي الدَّرْكِ الْأَسْفَلِ مِنَ النَّارِ

“Hakika wanafiki watakuwa katika tabaka la chini kabisa katika Moto.”[5]

Kutamka kwao shahaadah hakukuwafaa kitu. Kwa sababu wameisema kwa ndimi zao na wanakufuru maana yake kwa ndani:

إِنَّ الْمُنَافِقِينَ يُخَادِعُونَ اللَّـهَ وَهُوَ خَادِعُهُمْ وَإِذَا قَامُوا إِلَى الصَّلَاةِ قَامُوا كُسَالَىٰ يُرَاءُونَ النَّاسَ وَلَا يَذْكُرُونَ اللَّـهَ إِلَّا قَلِيلًا مُّذَبْذَبِينَ بَيْنَ ذَٰلِكَ لَا إِلَىٰ هَـٰؤُلَاءِ وَلَا إِلَىٰ هَـٰؤُلَاءِ

“Hakika wanafiki wanafikiri wanamhadaa Allaah na hali Yeye ndiye Mwenye kuwahadaa na wanaposimama kuswali basi husimama kwa uvivu, wakijionyesha kwa watu na wala hawamtaji Allaah isipokuwa kidogo tu. Wenye kuyumbayumba kati ya hayo, huku hawako wala huko hawako.”[6]

Hawana imani. Kadhalika kila mtu ambaye atatamka shahaadah ilihali anamwabudu Allaah, anapinga kufufuliwa na kukusanywa, uwajibu wa swalah, anaona kuwa uzinzi au pombe ni halali, anakufuru kwa matendo hayo kwa mujibu wa waislamu wote. Haijalishi kitu hata kama anatamka shahaadah. Kwa ajili hii wanachuoni katika kila madhehebu wametunga mlango unaosema “Mlango unaozungumzia hukumu ya mwenye kuritadi”. Kisha wakafafanua na kusema kwamba murtadi ni yule mwenye kukufuru baada ya kuingia katika Uislamu. Kwa msemo mwingine ni yule mwenye kufanya moja katika vitenguzi vya Uislamu. Mtu huyo anakufuru ijapokuwa atasema kwamba hapana mungu wa haki asiyekuwa Allaah. Kama atakuwa ni mwenye kuitamka, anaswali na anafunga lakini  pamoja na hivyo anasema kuwa uzinzi ni halali na anaona kwamba hakuna ubaya kwa mtu endapo atazini, anaona kuwa pombe au kuwaasi wazazi wawili ni halali anakufuru kwa mujibu wa wanachuoni wote.

[1] 38:05

[2] 37:36-37

[3] 37:35-37

[4] 33:40

[5] 04:145

[6] 04:142-143

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Kashf-ish-Shubuhaat, uk. 107-111
  • Imechapishwa: 26/10/2021