30. Mtu akitubia juu ya jambo la ukafiri na shirki Allaah anamsamehe

Mtu akifanya tawbah ya kweli basi Allaah anamsamehe. Akifanya ukafiri kwa ujinga abainishiwe na hakufuru, kama walivyofanya wale walioomba kufanyiwa Dhaat Anwaatw na wale waliosema:

اجْعَل لَّنَا إِلَهًا كَمَا لَهُمْ آلِهَةٌ

“Tufanyie mungu kama ambavyo wao wako na miungu!”[1]

Walifikiri kuwa kitendo hichi ni kizuri na ni cha sawa. Wakabainishiwa, wakatubia na wakarejea na hawakufanya yale Allaah aliyowakataza.

Kwa kifupi ni kwamba muislamu mwenye kuswali na mwenye kufunga akifanya jambo lenye kukufurisha ilihali ni mwenye kujinasibisha na Uislamu hakumzuii kukufuru japo atakuwa anaswali au anajinasibisha na Uislamu. Kwa ukafiri wake huu mpya anakuwa ni murtadi na matendo yake yanaporomoka:

قَدِمْنَا إِلَىٰ مَا عَمِلُوا مِنْ عَمَلٍ فَجَعَلْنَاهُ هَبَاءً مَّنثُورًا

”Tutayaendea yale waliyoyatenda katika matendo, Tutayafanya kuwa ni vumbi lililotawanyika.”[2]

Imepokelewa katika Hadiyth:

“Mwenye kubadilisha dini yake muueni.”[3]

Mlango huu ni wenye kutambulika. Huyo ni yule muislamu mwenye kukufuru baada ya Uislamu wake. Haijalishi kitu hata kama atakuwa ni miongoni mwa watu wenye kumwabudu Allaah kwa wingi. Mwenye kumtukana Allaah, Mtume Wake, akafanya mungu badala ya Allaah ambaye akawa anamuomba, anamuomba msaada, akapinga uwajibu wa swalah, zakaah, akapinga uharamu wa uzinzi, pombe au mfano wa hayo katika mambo ya jinai kama hayo matendo yake yote yanaporomoka na anakufuru kwa kitendo hicho. Matendo yake yote yanaharibika. Mwenye kufanya kitu chenye kukufurisha matendo yake yanaharibika na yanakuwa ni kama vumbi lililotawanyika:

وَلَوْ أَشْرَكُوا لَحَبِطَ عَنْهُم مَّا كَانُوا يَعْمَلُونَ

“Lau wangemshirikisha bila shaka yangeporomoka yale waliyokuwa wakitenda.”[4]

وَلَقَدْ أُوحِيَ إِلَيْكَ وَإِلَى الَّذِينَ مِن قَبْلِكَ لَئِنْ أَشْرَكْتَ لَيَحْبَطَنَّ عَمَلُكَ وَلَتَكُونَنَّ مِنَ الْخَاسِرِينَ

“Hakika umefunuliwa Wahy na kwa wale walio kabla yako kwamba: “Ukifanya shirki bila shaka yataporomoka matendo yako na hakika utakuwa miongoni mwa waliokhasirika.”[5]

وَمَن يَكْفُرْ بِالْإِيمَانِ فَقَدْ حَبِطَ عَمَلُهُ وَهُوَ فِي الْآخِرَةِ مِنَ الْخَاسِرِينَ

”Yeyote atakayekanusha imani, basi yameporomoka matendo yake naye Aakhirah atakuwa miongoni mwa waliokhasirika.”[6]

Ni lazima kwa muislamu kutahadhari na yale maasi yote aliyokataza Allaah na tahadhari yake juu ya shirki iwe kubwa zaidi. Asiseme kuwa yeye amefahamu Tawhiyd na amefahamu Uislamu. Asijiaminishe. Wako watu ambao wanasema kuwa wamefahamu Tawhiyd ilihali bado ni wajinga mpaka hii leo. Jengine hata kama atakuwa ni mwenye kufahamu na kuielewa anatakiwa kujichunga na asijiaminishe. Anapaswa kumuomba Allaah uimara, ajifunze dini na amuombe Mola Wake asije kupinda. Ni watu wangapi ambao wamesoma na wakaelewa kisha baadaye wakapondoka?

[1] 07:138

[2] 25:23

[3] al-Bukhaariy (2016).

[4] 06:88

[5] 39:65

[6] 05:05

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Kashf-ish-Shubuhaat, uk. 103-104
  • Imechapishwa: 26/10/2021