31. Itazame dunia yako unayokusanya

165 – Muhammad bin Idriys al-Handhwaliy amenihadithia: Abu Ghassaan Maalik bin Ismaa´iyl amenihadithia: ´Abdus-Salaam bin Harb amenihadithia, kutoka kwa Yuunus, kutoka kwa al-Hasan, kutoka kwa ´Utayy, kutoka kwa Ubayy bin Ka´b, kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), ambaye amesema:

”Allaah ameipigia mfano dunia kwa chakula cha mwanadamu na akakipigia mfano chakula cha mwanadamu kwa dunia, ingawa kitatiwa viungo na chumvi.”

al-Hasan amesema:

”Mmeona jinsi wanavyokitia chakula viungo na harufu nzuri, kisha baadaye wanakitupa kule mnakokuona.”

166 – Abu Khaythamah ametuhadithia: Ismaa´iyl bin ´Ulayyah ametuhadithia, kutoka kwa Yuunus, kutoka kwa al-Hasan, kutoka kwa ´Utayy, kutoka kwa Ubayy bin Ka´b, ambaye amesema:

”Chakula cha mwanadamu kimepigiwa mfano wa dunia, ingawa kitatiwa chumvi na viungo. Mahali pake pa mwisho panajulikana fika.”

167 – Abu ´Aliy al-Marwaziy ametuhadithia: ´Abdaan bin ´Uthmaan ametukhabarisha: ´Abdullaah bin al-Mubaarak ametukhabarisha: Sufyaan ametukhabarisha, kutoka kwaa ´Aaswim, kutoka kwa Abu ´Uthmaan, aliyesema:

”Kuna bwana mmoja alikuja kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kuomba, ambapo akamwambia: ”Je, unacho chakula?” Akasema: ”Ndio.” Akasema: ”Unakipika, unakitengeneza, unakionja na kukitia viungo?” Akasema: ”Ndio.” Akasema: ”Unacho kinywaji?” Akasema: ”Ndio.” Akasema: ”Unakitia baridi, barafu na kukisafisha?” Akasema: ”Ndio.” Akasema: ”Unayakusanya yote hayo tumboni?” Akasema: ”Ndio.” Akasema: ”Kinaishilia wapi?” Akasema: ”Allaah na Mtume Wake ndio wanajua zaidi.” Akamwambia hivo mara tatu, ambapo akasema: ”Mahali pake pa mwisho kinapoishilia ni kama mwisho wa dunia. Umetembea nyuma ya nyumba yako na ukazuia pua yako kutokana na harufu yake mbaya.”

168 – Muhammad bin ´Abbaad bin Muusa amenihadithia: Ghassaan bin Maalik ametuhadithia, kutoka kwa Hammaad bin Salamah, kutoka kwa Muhammad bin as-Saa-ib, kutoka kwa Abu Swaalih, kutoka kwa Ibn ´Abbaas, aliyesema kuhusu maneno Yake (Ta´ala):

فَلْيَنظُرِ الْإِنسَانُ إِلَىٰ طَعَامِهِ

”Basi atazame mtu chakula chake.”[1]

”Bi maana kinyesi chake.”

169 – Ishaaq bin Ismaa´iyl ametuhadithia: Sufyaan bin ´Uyaynah ametuhadithia, kutoka kwa Ibn-ul-Murtafiy´, ambaye amesimulia kuwa amemsikia Ibn-uz-Zubayr akisema kuhusu maneno Yake (Ta´ala):

وَفِي أَنفُسِكُمْ ۚ أَفَلَا تُبْصِرُونَ

”Na katika nafsi zenu, je, hamuoni?”[2]

”Bi maana njia ya kinyesi na mkojo.”

170 – Baba yangu amenihadithia: Rawh bin ´Ubaadah ametukhabarisha: Sa´iyd bin ´Ubayd al-Jubayriy ametuhadithia, kutoka kwa Bakr bin ´Abdillaah al-Muzaniy, ambaye amesimulia kuwa bwana mmoja amemweleza:

”Nilitangamana na Ka´b al-Ahbaar kwa miaka kumi na moja. Wakati alipotaka kukata roho alisema: ”Mimi nimesuhubiana na wewe kwa miaka kumi na moja. Nataka kukuuliza jambo, lakini nakuogopa.” Akasema: ”Uliza unachotaka.” Akasema: ”Nieleze ni kwa nini mtu anaposimama baada ya kumaliza kukidhi haja yake, hukitazama.” Akasema: ”Naapa kwa Yule ambaye mkononi Mwake mna nafsi ya Ka´b! Umeuliza kitu ambacho Allaah amemteremshia Muusa kwenye Tawraat – Allaah amsifu, Muhammad na Manabii na Mitume Wake wengine wote, Malaika Wake na waja Wake wema – nacho ni: Itazame dunia yako unayokusanya!”

[1] 80:24

[2] 51:21

  • Mhusika: Imaam Abu Bakr ´Abdullaah bin Muhammad bin Abiyd-Dunyaa
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Kitaab-ul-Juu´, uk. 107-112
  • Imechapishwa: 25/07/2023