158 – Ukimsikia mtu anasema kuwa eti anamtukuza Allaah wakati anaposikia masimulizi ya Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), basi tambua kuwa huyo ni Jahmiy. Anachotaka ni kuyarudisha masimulizi ya Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na kuyatupilia mbali kwa maneno haya. Anadai kuwa anamuadhimisha Allaah na kumtakasa pale anaposikia Hadiyth kuhusu Kuonekana, Kushuka kwa Allaah na mfano wazo.  Je, mtu huyu hayarudishi nyuma masimulizi ya Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam)? Akisema kuwa  Allaah ametakasika kutokamana na kuhama kutoka sehemu moja kwenda sehemu nyingine, amedai kuwa yeye ni mjuzi zaidi juu ya Allaah kuliko wengine. Tahadhari na watu hawa, hakika wengi katika watu wasio wasomi na wengineo wako katika hali kama hii. Tahadharisha watu kutokamana nao!

159 – Akiwepo mtu anayetaka kuongoka atakuuliza kitu kilichomo ndani ya kitabu hiki, basi zungumza naye na umwelekeze. Hata hivyo endapo atakuja kutaka kujadiliana nawe, tahadhari naye. Hakika katika mijadala kuna ubishi, mabishano, ushindani, magomvi na kukasirika. Hakika wewe umekatazwa yote haya. Mambo kama haya yanamtoa mtu katika njia ya haki. Hatukupata khabari ya yeyote katika wanazuoni wetu ya kwamba alijadiliana, kubishana au kugombana. al-Hasan al-Baswriy amesema:

“Yule mwenye hekima habishani na wala hashindani. Ni mwenye kueneza hekima yake; ikikubaliwa anamuhimidi Allaah, na ikirudishwa anamuhimidi Allaah.”[1]

Kuna mtu alikuja kwa al-Hasan akamwambia:

“Nataka kujadiliana na wewe katika dini!” al-Hasan akasema: “Kuhusu mimi, naielewa dini yangu. Lakini kama dini yako imepotea, basi nenda ukaitafute.”[2]

Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) aliwasikia watu waliokuwa wamesimama nje ya chumba chake wakijadiliana. Mmoja wao anasema: “Je, Allaah hakusema kadhaa?” Mwengine naye akijibu: “Je, Allaah hakusema kadhaa?” Akatoka hali ya kukasirika na kusema:

“Je, haya ndio mliyoamrishwa? Nilitumwa kwenu kwa haya? Mnafanya sehemu ya Kitabu cha Allaah kugonga sehemu nyingine?”

Hivyo akakataza mijadala.

Ibn ´Umar alikuwa akichukia mijadala na hali kadhalika Maalik bin Anas na waliokuwa juu yao na waliokuwa chini yao, mpaka hii leo. Maneno ya Allaah (´Azza wa Jall) ni makubwa zaidi kuliko maneno ya viumbe. Allaah (Tabaarak wa Ta´ala) amesema:

مَا يُجَادِلُ فِي آيَاتِ اللَّـهِ إِلَّا الَّذِينَ كَفَرُوا

“Habishani katika Aayah za Allaah isipokuwa wale waliokufuru.”[3]

Kuna bwana mmoja alimuuliza ´Umar bin al-Khattwaab:

“Ni nini:

وَالنَّاشِطَاتِ نَشْطًا

“… wanaotoa kwa upole.”[4]?

Akamjibu: “Lau ungelikuwa umenyoa kipara, basi ningekata shingo yako.”[5]

Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Muumini habishani. Sintomshufaia mwenye kubishana siku ya Qiyaamah. Acheni ubishi, kutokana na uchache wa kheri yake.”[6]

[1] al-Ibaanah al-Kubraa (661) ya Ibn Battwah na wengineo.

[2] Ibn Maajah (85). Nzuri na Swahiyh kwa mujibu wa al-Albaaniy katika ”Swahiyh Sunan Ibn Maajah”.

[3] 40:04

[4] 79:02

[5] ad-Daarimiy (01/51) na wengineo.

[6] Hadiyth dhaifu mno kwa mujibu wa ar-Raajihiy katika “Sharh Kitaab-is-Sunnah lil-Barbahaariy” (15/8).

  • Mhusika: Imaam Abu Muhammad al-Hasan bin Khalaf al-Barbahaariy (kfk. 329)
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh-us-Sunnah, uk. 129-131
  • Imechapishwa: 30/12/2024