31. Du´aa ya Shaykh kwa kila anayekisoma, kukifahamu na kukitendea kazi kitabu hiki

Shaykh-ul-Islaam Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab (Rahimahu Allaah) amesema:

Tambua – Allaah akuongoze katika utiifu Wake 

MAELEZO

Hapa ni kama vile anaanza ujumbe wa tatu kwa sababu kumeshatangulia nyujumbe mbili; ujumbe wa kwanza ni yale masuala mane yaliyoko ndani ya Suurah “al-´Aswr”, ujumbe wa pili ni yale masuala matatu yaliyotangulia na ujumbe wa tatu ni haya hapa na yanakutana na masuala ya nne ambayo ni ile misingi mitatu.

Tambua – Tumekwishatangulia kuyataja na kubainisha maana yake na malengo ya kusema hivo.

Allaah akuongoze – Hii ni du´aa kutoka kwa Shaykh (Rahimahu Allaah) kwenda kwa kila anayesoma kitabu hiki, anajaribu kukielewa na anataka kukitendea kazi kwamba Allaah amwongoze. Uongofu ni kuelekezwa katika yale ya sawa na kuafikishwa katika elimu yenye manufaa na matendo mema. Uongofu ni kinyume na upotevu. Amesema (Ta´ala):

قَد تَّبَيَّنَ الرُّشْدُ مِنَ الْغَيِّ

“Imekwishabainika uongofu kutokamana na upotevu.”[1]

وَإِن يَرَوْا كُلَّ آيَةٍ لَّا يُؤْمِنُوا بِهَا وَإِن يَرَوْا سَبِيلَ الرُّشْدِ لَا يَتَّخِذُوهُ سَبِيلًا وَإِن يَرَوْا سَبِيلَ الْغَيِّ يَتَّخِذُوهُ سَبِيلًا

“Wakiona kila alama hawaiamini, na wakiona njia ya uongofu, basi hawaishiki kuwa ndio njia, na wanapoona njia ya upotevu, basi wanaishika kuwa ndio njia.”[2]

Uongofu ndio dini ya Uislamu. Upotofu ni dini ya Abu Jahl na watu mfano wake.

Allaah akuongoze katika utiifu Wake – Hii ni du´aa tukufu. Kwani muislamu akiongozwa na Allaah katika utiifu Wake basi amefaulu duniani na Aakhirah. Utiifu ni kutekeleza yale yaliyoamrishwa na Allaah na kujiepusha na yale Allaah aliyokataza. Huu ndio utiifu. Umtii Allaah katika maamrisho Yake ukayafanya na makatazo Yake ukajiepusha nayo hali ya kutekeleza amri ya Allaah na kutafuta uso wa Allaah (´Azza wa Jall) huku ukitarajia thawabu Zake na ukichelea adbabu Yake. Mwenye kuwafikishwa kumtii Allaah na akaongozwa kumtii Allaah basi huyo amefaulu duniani na Aakhirah.

[1] 02:256

[2] 07:146

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Thalaathat-il-Usuwl, uk. 69-70
  • Imechapishwa: 08/12/2020