32. Haniyfiyyah ndio ilikuwa dini ya Mitume wote

Shaykh-ul-Islaam Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab (Rahimahu Allaah) amesema:

kwamba Haniyfiyyah ndio dini ya Ibraahiym; 

MAELEZO

Haniyfiyyah – Unachotakiwa kujua ni kwamba Haniyfiyyah ni mila ya Ibraahiym. Maana ya al-Hanaf katika lugha ni kumili. Maana yake ni kwamba Haniyfiyyah ni mila yenye kumili kutoka katika shirki na kwenda katika Tawhiyd. Ibraahiym (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikuwa ni Haniyfah na muislamu. Kwa msemo mwingine alikuwa ni mwenye kujiengua kutokamana na shirki na mwenye kuielemea Tawhiyd. Ibraahiym (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikuwa ni Haniyfah na muislamu. Kwa msemo mwingine alikuwa ni mwenye kujiengua kutokamana na shirki, akiipa mgongo na akiielemea Tawhiyd na kumtakasia nia Allaah (´Azza wa Jall). Amesema (Ta´ala):

إِنَّ إِبْرَاهِيمَ كَانَ أُمَّةً قَانِتًا لِّلَّـهِ حَنِيفًا وَلَمْ يَكُ مِنَ الْمُشْرِكِينَ

”Hakika Ibraahiym alikuwa ni mfano mwema, mnyenyekevu kwa Allaah na mwenye kuelemea Tawhiyd na kujiengua na shirki; hakuwa miongoni mwa washirikina.”[1]

al-Haniyf ni moja katika sifa za Ibraahiym (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Hiyo ina maana kwamba alikuwa ni mwenye kuipuuza shirki na kujiengua nayo kikamilifu, akiielekea Tawhiyd, akiuelekeza uso wake kikamilifu kwenda katika Tawhiyd na kumtakasia ´ibaadah Allaah (´Azza wa Jall). Allaah (Ta´ala) amesema:

ثُمَّ أَوْحَيْنَا إِلَيْكَ أَنِ اتَّبِعْ مِلَّةَ إِبْرَاهِيمَ حَنِيفًا

 “Kisha Tukakufunulia Wahy kwamba fuata imani ya Ibraahim iliyo safi na kutakasika.”[2]

مَا كَانَ إِبْرَاهِيمُ يَهُودِيًّا وَلَا نَصْرَانِيًّا وَلَـٰكِن كَانَ حَنِيفًا مُّسْلِمًا وَمَا كَانَ مِنَ الْمُشْرِكِينَ

“Ibraahiym hakuwa myahudi wala mnaswara – lakini alikuwa ni mwenye kuelemea Tawhiyd na kujiengua na shirki na tena muislamu; na hakuwa miongoni mwa washirikna.”[3]

Hizi ndio sifa za Ibraahiym (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Miongoni mwazo ni kwamba alikuwa ni Haniyf na kwamba mila yake ya Haniyfiyyah ndio mila takasifu kwa Allaah (´Azza wa Jall) ambayo imesalimika na shirki. Allaah amemwamrisha Mtume Wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kuifuata mila hii pale aliposema:

ثُمَّ أَوْحَيْنَا إِلَيْكَ أَنِ اتَّبِعْ مِلَّةَ إِبْرَاهِيمَ حَنِيفًا ۖ وَمَا كَانَ مِنَ الْمُشْرِكِينَ

 “Kisha Tukakufunulia Wahy kwamba fuata imani ya Ibraahim iliyo safi na kutakasika na hakuwa miongoni mwa washirikina.”[4]

Vilevile akatuamrisha sisi pia kuifuata mila ya Ibraahiym (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) pale aliposema:

هُوَ اجْتَبَاكُمْ وَمَا جَعَلَ عَلَيْكُمْ فِي الدِّينِ مِنْ حَرَجٍ ۚ مِّلَّةَ أَبِيكُمْ إِبْرَاهِيمَ ۚ هُوَ سَمَّاكُمُ الْمُسْلِمِينَ

“Yeye ndiye amekuteueni na hakukufanyieni ugumu wowote ule katika dini. Mila ya baba yenu Ibraahiym. Yeye ndiye amekuiteni waislamu.”[5]

Hii ndio dini ya Mitume wote.

Lakini kwa sababu Ibraahiym (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ndiye Mtume bora baada ya Mtume wetu Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikutana na adhabu na mitihani ambayo haikumkuta mwengine wakati alipokuwa akilinganmia katika Tawhiyd. Akasubiri juu ya hayo. Sababu nyingine yeye ndiye baba wa Mitum. Mitume wote waliokuja baada yake wanatokana na kizazi chake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Kwa hiyo Haniyfiyyah ndio mila ya Mitume wote. Inahusiana na kulingania katika Tawhiyd na kukemea shirki. Hii ndio mila ya Mitume wote. Lakini pale ilipokuwa kwamba Ibraahiym ndiye aliyekuwa na msimamo maalum juu ya mila hii ndipo akanasibishiwa nayo na kwa wale waliokuja baada yake.

Mitume wote waliokuja baada yake walikuwa katika mila ya Ibraahiym ambayo ni mila ya Tawhiyd na kumtakasia ´ibaadah Allaah (´Azza wa Jall). Ni mila ipi hiyo ambayo Mtume wetu (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ameamrishwa kuifuata na tukaamrishwa sisi pia kuifuata? Ni lazima kwetu kuijua. Kwa sababu ni lazima kwa muislamu kujua ni yepi yale ambayo Allaah ameyawajibisha kwake ili aweze kuyatekeleza na ili asiyaharibu. Haitoshi kujinasibisha bila ya kuijua. Haitoshi kujinasibisha na Uislamu ilihali haujui, hajui ni vipi vichenguzi vya Uislamu, Shari´ah za Kiislamu na hukumu za Kiislamu. Haitoshi kwako kujinasibisha na mila ya Ibraahiym pasi na kuijua na unapoulizwa juu yake unajibu kuwa hujui. Hili ni jambo lisilofaa. Ni lazima kwako kuijua ujuzi mzuri ili uweze kupita juu yake kwa ujuzi na wala usiharibu chochote katika hayo.

[1] 16:120

[2] 16:123

[3] 03:67

[4] 16:123

[5] 22:78

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Thalaathat-il-Usuwl, uk. 70-73
  • Imechapishwa: 08/12/2020