Masuala haya yanahusiana na kuwachukia makafiri na kutowapenda. Lakini hayapelekei kwetu kuwakata makafiri katika mambo na manufaa mbalimbali ya kidunia. Bali juu ya hayo kunavuliwa mambo yafuatayo:

1- Pamoja na kuwachukia kwetu na kuwajengea uadui ni lazima kwetu kuwalingania kwa Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala). Ni lazima kwetu kuwalingania kwa Allaah na tusiwaache na tukasema kuwa hawa ni maadui wa Allaah na maadui zetu. Ni lazima kwetu kuwalingania kwa Allaah huenda Allaah akawaongoza. Wasipoitikia basi tunawapiga vita tukiwa na uwezo. Ima waingie katika Uislamu au walipe kodi wakiwa ni mayahudi, manaswara au waabudia moto. Wanatakiwa kuitoa kwa unyenyekevu, wakinyenyekea hukumu ya Uislamu, basi waachwe katika yale wanayofanya. Lakini kwa sharti walipe kodi na wanyenyekee hukumu ya Uislamu. Mbali na Ahl-ul-Kitaab na waabudia moto kupokea kodi kutoka kwao wanachuoni wametofautiana juu ya suala hilo.

2- Hakuna neno kuwapaka mafuta makafiri wakati wa haja pindi waislamu watapohitajia kufanya hivo kwa sababu hawana uwezo wa kuwapiga vita na isitoshe kunakhofiwa juu ya waislamu shari yao. Katika hali hiyo hakuna neno kuwapaka mafuta mpaka pale waislamu watapokuwa na nguvu za kuwapiga vita au pindi wao watapohitajia kufanya hivo:

وَإِن جَنَحُوا لِلسَّلْمِ فَاجْنَحْ لَهَا وَتَوَكَّلْ عَلَى اللَّـهِ ۚ إِنَّهُ هُوَ السَّمِيعُ الْعَلِيمُ

“Na kama watalemea kwenye amani, basi nawe ielemee na mtegemee Allaah. Hakika Yeye ni Mwenye kusikia yote, Mjuzi wa yote.”[1]

Katika hali hiyo watapakwa mafuta. Lakini sio katika maisha yote. Inahusiana na upakaji mafuta wa muda maalum kutegemea na maoni ya kiongozi wa waislamu kutokana na yale yenye manufaa.

3- Hakuna neno kuwalipiza kwa wema wakiwafanyia wema waislamu. Hakuna neno kuwalipiza wema kwa wema wao. Allaah (Ta´ala) amesema:

لَّا يَنْهَاكُمُ اللَّـهُ عَنِ الَّذِينَ لَمْ يُقَاتِلُوكُمْ فِي الدِّينِ وَلَمْ يُخْرِجُوكُم مِّن دِيَارِكُمْ أَن تَبَرُّوهُمْ وَتُقْسِطُوا إِلَيْهِمْ ۚ إِنَّ اللَّـهَ يُحِبُّ الْمُقْسِطِينَ

“Allaah hakukatazeni kuwafanyia wema na uadilifu wale wasiokupigeni vita katika dini na wala hawakukutoeni kutoka majumbani mwenu. Hakika Allaah anapenda wenye kufanya uadilifu.”[2]

4- Ni lazima kwa mtoto muislamu kumtendea wema mzazi wake kafiri. Lakini hata hivyo asimtii katika ukafiri. Amesema (Ta´ala):

وَوَصَّيْنَا الْإِنسَانَ بِوَالِدَيْهِ حَمَلَتْهُ أُمُّهُ وَهْنًا عَلَىٰ وَهْنٍ وَفِصَالُهُ فِي عَامَيْنِ أَنِ اشْكُرْ لِي وَلِوَالِدَيْكَ إِلَيَّ الْمَصِيرُ وَإِن جَاهَدَاكَ عَلَىٰ أَن تُشْرِكَ بِي مَا لَيْسَ لَكَ بِهِ عِلْمٌ فَلَا تُطِعْهُمَا ۖ وَصَاحِبْهُمَا فِي الدُّنْيَا مَعْرُوفًا ۖ وَاتَّبِعْ سَبِيلَ مَنْ أَنَابَ إِلَيَّ ۚ ثُمَّ إِلَيَّ مَرْجِعُكُمْ فَأُنَبِّئُكُم بِمَا كُنتُمْ تَعْمَلُونَ

“Tumemuusia mwanaadamu kwa wazazi wake wawili – mama yake ameibeba mimba yake kwa udhaifu juu ya udhaifu na kumwachisha ziwa katika miaka mwili – ya kwamba: unishukuru Mimi na wazazi wako; kwani Kwangu ndio pa kuishia. Lakini wakikung´ang´ania kuwa unishirikishe na ambayo huna elimu nayo, basi usiwatii na tangamana nao kwa wema duniani na fuata njia ya anayerudi kutubia Kwangu. Halafu Kwangu ndio marejeo yenu na nitakujulisheni yale mliyokuwa mkiyatenda.”[3]

Mzazi ana haki ijapokuwa ni kafiri. Lakini asimpende mapenzi ya kimoyo. Amtendee wema kwa vile alimlea, mzazi ana haki. Amlipe wema kwa hayo.

5- Kubadilishana nao mambo ya kimanufaa na kufanya nao biashara. Kununua bidhaa kutoka kwao, kuingiza bidhaa nchini na silaha kutoka kwao. Hakuna ubaya kufanya hayo. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikuwa akifanya kazi pamoja na makafiri na vivyo hivyo (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) aliwafanyisha kazi mayahudi wa Khaybar ya kulima ardhi kwa sehemu katika vile vinavyotoka humo. Huku sio katika kupenda na kuwafanya marafiki. Huku ni kubadilishana mambo ya manufaa. Ni lazima kuyajua mambo haya na kwamba hayaingii katika kupenda na kwamba hayakukatazwa.

Vilevile kuchukua mkopo kutoka kwao. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alichukua mkono kutoka kwa myahudi na akaiweka kwake rehani nguo yake ya vita na amekufa (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na nguo yake ya vita imewekwa rehani kwa myahudi kwa sababu ya chakula alichowanunulia familia yake. Hakuna ubaya wa mambo hayo kwa sababu hayo ni mambo ya kidunia na manufaa. Hayafahamishi mapenzi na kuwafanya marafiki ndani ya moyo.

Ni lazima kupambanua kati ya hayo mawili. Kwani baadhi ya watu wanaposikia dalili za kuwachukia makafiri na kutowapenda wanaweza kufahamu makosa kwamba haifai kufanya nao kazi, mtu asiwe na mahusiano nao kabisa na kwamba mtu anatakiwa awakate kabisa. Sivyo hivyo. Haya yana mipaka yake kwa hukumu na kwa sharti zake zinazotambulika na wanachuoni zilizochukuliwa kutoka katika Qur-aan na Sunnah.

6- Allaah amehalalisha kuwaoa wanawake wa Ahl-ul-Kitaab kwa sharti wawe ni wenye kujichunga katika heshima zao. Vilevile Allaah ametuhalalishia kula vichinjwa vyao.

7- Hakuna neno kuitikia mwaliko wao na kula chakula chao cha halali. Hayo yamefanywa na Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam).

8- Kuwafanyia wema majirani makafiri. Kwa sababu wana haki ya ujirani.

9- Haijuzu kuwadhulumu. Amesema (Ta´ala):

وَلَا يَجْرِمَنَّكُمْ شَنَآنُ قَوْمٍ عَلَىٰ أَلَّا تَعْدِلُوا ۚ اعْدِلُوا هُوَ أَقْرَبُ لِلتَّقْوَىٰ

“Na wala chuki ya watu isikuchocheeni kutokufanya uadilifu. Fanyeni uadilifu; hivyo ni karibu zaidi na kumcha Allaah.”[4]

[1] 08:61

[2] 60:08

[3] 31:14-15

[4] 05:08

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Thalaathat-il-Usuwl, uk. 66-69
  • Imechapishwa: 08/12/2020