Kusema uongo ni kila kauli inayopotoka kutoka kwenye haki kwenda batili. Ndani yake kunaingia kila neno la haramu kama kusema uwongo, kutukana, matusi, usengenyi, umbea na ushahidi wa uongo.

Kufanyia kazi uwongo ni kufanya kila kitendo kilichoharamishwa ambacho ni dhuluma kwa watu, kama vile udhalimu, usaliti, udanganyifu, kuchukua mali, kuwakera watu na mfano wa hayo. Pia ndani yake kunaingia kusikiliza au kuangalia yale aliyoharamisha Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala) kama nyimbo na vyombo vya muziki wa pumbao.

Ujinga ni upumbavu. Ni kule kwenda kinyume cha hekima katika maneno na vitendo.

Hakika swawm ni shule ya malezi inayofundisha uvumilivu, subira na ukweli. Aidha inahimiza maadili mema na sifa bora za maneno na matendo. Swawm ya Kishari´ah ni swawm ya viungo kutokana na madhambi, tumbo kutokana na chakula na kinywaji, tupu kutokana na mambo ya mke na mume na kuwa na mahusiano ya kimapenzi. Ikiwa hayo yatakamilika, basi swawm inatoa matunda na manufaa yake na kusababisha msamaha ulioahidiwa.

  • Muhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Minhat-ul-´Allaam fiy Sharh Buluugh-il-Maraam (05/39)
  • Imechapishwa: 12/02/2025