29. Shubuha ya pili: “Sisi tunawaabudu mawalii ili watuombee kwa Allaah” na majibu juu yake

Miongoni mwa shubuha zao ni kwamba wanasema sisi hatuwaabudu mawalii na watu wema kwa kuwa eti wananufaisha na kudhuru, isipokuwa tunawaabudu ili tu waweze kutuombea mbele ya Allaah. Wanajikurubisha kwao kwa kuchinja, kuwawekea nadhiri na kuwataka msaada ili wawaombee kwa Allaah. Ama washirikina wa kale walikuwa wanaamini kuwa vitu hivi vinanufaisha na kudhuru badala ya Allaah (´Azza wa Jall). Wanasema kwamba wao hawaitakidi hivyo na kwamba wao wanatambua kwamba hawanufaishi wala hawadhuru lakini tunawachukua na kuwafanya tu kama waombezi wao.

Jibu ni kwamba haya ndio yaleyale aliyoyataja Allaah kuhusu washirikina wa kale. Amesema (Ta´ala):

وَيَعْبُدُونَ مِن دُونِ اللَّـهِ مَا لَا يَضُرُّهُمْ وَلَا يَنفَعُهُمْ وَيَقُولُونَ هَـٰؤُلَاءِ شُفَعَاؤُنَا عِندَ اللَّـهِ

”Wanaabudu asiyekuwa Allaah ambao hawawezi kuwadhuru wala kuwanufaisha na huku wanasema: “Hawa ni waombezi wetu mbele ya Allaah.” (Yuunus 10:18)

Hakuna tofauti kati ya shirki ya watu hawa na shirki ya wa kale. Wote wanakusudia uombezi na kwamba waabudiwa wao wawaombee. Uombezi ni haki, lakini hii sio njia yake. Ina njia zake za zilizowekwa katika Shari´ah ambazo Allaah kazibainisha Mtume wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amezibainisha. Sio katika njia zake ya kwamba muombeaji afanywe kuwa ni mungu badala ya Allaah ambapo akachinjiwa, akawekewa nadhiri, akaombwa msaada n.k. Haya ndio matendo ya washirikina wa mwanzo. Hakuna tofauti kabisa.

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Nawaaqidh-il-Islaam, uk. 52
  • Imechapishwa: 02/08/2018