28. Shubuha ya kwanza: “Shirki ni kuabudu masanamu tu” na majibu juu yake

Kuna shubuha wanazoleta waabudu makaburi na waabudu mawalii na watu wema hii leo ambazo kwazo wanawatatiza watu. Miongoni mwazo wanasema kwamba shirki ni kule kuyaabudu masanamu tu. Kuhusu yule mwenye kuabudu badala ya masanamu sio mshirikina, kama yule anayeabudu mawalii na watu wema. Wanasema kuwa sio shirki. Wanasema kuwa huku ni kufanya Tawassul kwa Allaah. Isitoshe Allaah (Ta´ala) amesema:

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا اتَّقُوا اللَّـهَ وَابْتَغُوا إِلَيْهِ الْوَسِيلَةَ

“Enyi walioamini! Mcheni Allaah na tafuteni njia ya kumkurubia.” (al-Maaidah 05:35)

Jibu juu ya shubuha hii ni kwamba wale ambao walipigwa vita na Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) wako ambao walikuwa wakiyaabudu masanamu, wako ambao walikuwa wakiabudu miti na mawe, wako ambao walikuwa wakiwaabudu Malaika, wako waliokuwa wakiwaabudu mawalii na waja wema. Amesema (Ta´ala):

وَيَعْبُدُونَ مِن دُونِ اللَّـهِ مَا لَا يَضُرُّهُمْ وَلَا يَنفَعُهُمْ وَيَقُولُونَ هَـٰؤُلَاءِ شُفَعَاؤُنَا عِندَ اللَّـهِ

”Wanaabudu asiyekuwa Allaah ambao hawawezi kuwadhuru wala kuwanufaisha na huku wanasema: “Hawa ni waombezi wetu mbele ya Allaah.” (Yuunus 10:18)

Kadhalika manaswara wamemuabudu al-Masiyh. Hawaabudu sanamu. Wanamuabudu al-Masiyh ambaye ni Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Je, mtu anaweza kusema ya kwamba sio washirikina kwa kuwa hawaabudu sanamu? Ni nani awezaye kusema hivi? Shirki ni kumuabudu asiyekuwa Allaah. Haijalishi kitu yule au kile kinachoabudiwa. Washirikina wa kale shirki yao haikuwa imekomeka katika kuyaabudu masanamu peke yake. Walikuwa ni wenye kutofautiana katika ´ibaadah zao. Kama alivokuwa amesema Shaykh katika kitabu chake “Kashf-ush-Shubuhaat” na “al-Qawaa´id al-Arba´ah” ya kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alijitokeza katika watu ambao walikuwa ni wenye kutofautiana katika ´ibaadah zao ambapo akawapiga vita na kuwaua wote na wala hakutofautisha kati yao. Hakutofautisha kati ya wale wenye kuabudu sanamu, mti, jiwe, Malaika, jini au mtu. Hili ni jambo lililo wazi.

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Nawaaqidh-il-Islaam, uk. 51-52
  • Imechapishwa: 02/08/2018